April 12, 2016



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed amesema ni vyema kwa Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo kujenga tabia ya kukubali kukosolewa na wafanyakazi walio chini yao zinapotokea hitilafu za kiutendaji wakati wanapotekeleza majukumu yao ya  kazi.
Mh. Aboud amesema hayo katika kikao cha kwanza alipokutana na Viongozi wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Ofisi hiyo mara baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar kushika wadhifa wa kuiongoza Wizara hiyo Kikao kilichofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Amesema Wananchi wameanza kujenga matumaini yanayotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa kipindi cha Pili cha Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mh. Aboud ameeleza kwamba Miaka mitano ijayo itakuwa ya kasi katika utendaji wa Serikali kuu iliyojikita zaidi kuimarisha uchumi na kusimamia Maendeleo kwa kutegemea rasilmali  na vianzio vyake vya mapato.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea matumaini yake kutokana na umakini wa Viongozi walioanza kukabidhiwa majukumu ya kusimamia Taasisi za Umma katika maeneo mbali mbali.
Akizungumzia suala la udhibiti na matumizi sahihi ya fedha pamoja na Vifaa vya Serikali Mh. Aboud amewakumbusha Viongozi wa Taasisi hizo kuhakikisha suala hilo wanalisimamia kwa nguvu zao zote kwa kuzingatia  taratibu na kanuni za kazi.
Amesema udhibiti na usimamizi wa matumizi sahihi ya fedha za Serikali ni kitu cha msingi kinachopaswa kushirikisha watendaji na viongozi wa ngazi zote za Taasisi na mashirika ya Umma.
Mapema Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ahmad Kassim amesema watendaji wa Ofisi hiyo wamepata faraja kubwa kutokana na imani ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein kwa kumteuwa tena Mh. Aboud kushika wadhifa huo.
Ahmad amesema watendaji wanaamini kwamba kasi ya utendaji kwa Taasisi na mashirikia yaliyo chini ya Ofisi hiyo itaongezeka kutokana na uhusiano na maingiliano ya muda wa miaka mitano iliyopo kati ya Kiongozi huyo na watendaji hao.

0 comments:

Post a Comment