December 10, 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemuagiza Mmiliki wa Kiwanja kinachotaka kujengwa Nyumba ya Ghorofa katika Mtaa wa Mlandege  Anuari Abdulla kusitisha mara moja ujenzi huo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko makubwa yaliyotolewa na wakaazi wa Mtaa huo wakimshutumu Mmiliki huyo kuvamia eneo la wazi katika sehemu hiyo.
Balozi Seif alimuonya Mmiliki huyo iwapo ataendelea kukaidi agizo alilopewa na taasisi zinazosimamia na kushughulikia masuala ya Ujenzi  Serikali italazimika kumchulia hatua za kisheria dhidi yake.
“ Tumebaini unaendelea kwenda kinyume na maamuzi uliyopewa ya kusitisha ujenzi wa Jengo lako sasa iwapo utaendelea kufanya hivyo Serikali italazimika kukuchukulia hatua za kisheria zinazofaa “. amesema Balozi Seif.
Amefahamisha kuwa wakaazi wa Mtaa wa Mlandege kuzingatia matakwa yaliyokubalika katika uhifadhi wa eneo la Mji Mkongwe lililopata hadhi ya kuwa Urithi wa Kimataifa ambapo mtaa huo pia umo ndani ya mji huo wa Kihistoria.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar   Issa Sarboko Makarani ameeleza kuwa Mmiliki wa kiwanja hicho amekuwa akikaidi maamuzi anayopewa kuyatekeleza na mamlaka husika katika ujenzi huo.
“ Kibali cha Ujenzi wa Jengo hili kinachodaiwa kutolewa na Baraza la Manispaa Zanzibar kimefutwa kwa pamoja na wakurugenzi Wanne wa Idara za Ardhi, Mamlaka ya Mji Mkongwe, Baraza la Manispaa pamoja na Idara ya Ujenzi na Mipango Miji “. amefafanua   Sarboko.
Amesema Anuari ameamua kuendeleza ujenzi huo kwa kutumia kibali  kilichofutwa alichopewa na Mmoja wa Afisa wa Baraza la Manispaa kwa vile hakikuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.


0 comments:

Post a Comment