Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amesema Vijana wanapaswa kuelewa kazi kubwa
ya chama cha siasa ni kushinda uchaguzi ili kushika Dola kama inavyoelezwa
katika Katiba na kanuni za Chama cha Mapinduzi.
Akilifungua Kongamano la Vijana wa CCM wa vyuo
Vikuu kuadhimisha miaka 39 tangu kuzaliwa kwa CCM Mjini Zanzibar amesema Viongozi pamoja na
Wanachama hicho CCM wanataka kuona Chama kinaendelea kubakia kuwa kimbilio la
Wanawake.
Amesema Chama chochote kitakachojenga tabia ya
kudharau kundi la Wanawake ambalo ndio kubwa katika Jamii hakitokuwa na nafasi
ya kushinda uchaguzi kwa sasa na hata hapo baadaye.
“ Wanawake ni zaidi ya nusu ya Watanzania.
Sasa ukilidharau kundi hili maana yake umejidharau mwenyewe na dhambi hiyo
kubwa na isifikie wakati akatafutwa
mchawi wa kulaumiwi”. alisema Balozi Seif.
Balozi Seif amelitaja kundi jengine kubwa la
Vijana ambalo chama cha Siasa kinapaswa kuwa na Sera na mfumo bora
utakaowavutia Vijana wengi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kushinda
uchaguzi na huo ndio mtazamo wa Chama cha Mapinduzi.
Amesema Chama kinategemea kazi hiyo ya
kuwavutia Vijana kujiunga kwa wingi itasimamiwa na kufanywa na Vijana hao wa CCM
wa Vyuo Vikuu ambao changamoto inayowakabili kwa sasa ni kutoa mbinu ili
malengo yaliyokusudiwa yafikiwe mapema iwezekanavyo.
Amewashauri Vijana hao wa Vyuo Vikuu kujidhatiti
zaidi katika ujenzi wa Chama chao kama walivyofanya Vijana Wasomi wa Chama cha
zamani cha ASP wa Young African Social Union {YASU} waliokuwa wakiwakusanya
vijana na kuwapatia elimu nyakati
za jioni.
Balozi Seif amefahamisha kuwa kundi la Vijana wa Afro Shirazy Party {Yasu}
lilikuwa na mipango mizuri ya kujenga Chama chao na kupelekea kuanzisha
Magazeti ya Kipanga na Tai pamoja na kujenga Jumba la ghorofa maarufu Yasu
liliopo Mtaa wa Miembeni Mjini Zanzibar.
Akizungumzia uimara wa Chama cha Mapinduzi
katika kipindi cha miaka 39 iliyopita tokea kilipoasisiwa mwaka 1977 Balozi
Seif amesema zipo faida nyingi zilizoimarika kupitia CCM ikiwemo uimarishaji wa
Muungano, Uongozi wa pamoja , Uchumi pamoja na Demokrasia.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM amefahamisha kuwa historia ya Demokrasia Nchini Tanzania
ikiandikwa haitokamilika bila ya kutoa nafasi ya pekee kwa CCM
kutokana na juhudi zake za kufungua milango ya Demokrasia Nchini.
Balozi Seif alisema Demokrasia madhubuti ndani
ya CCM ndio iliyoanzisha Mjadala wa haja ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya
Kisiasa na kupelekea kufunguliwa milango ya Demokrasia mwaka 1992.
Ameeleza kwamba ufunguzi huo wa milango ya
Demokrasia Nchini chini ya Chama cha Mapinduzi umewezesha kuibuka kwa zaidi ya
vyama 18 vya siasa Nchini Tanzania na kupata usajili wa kudumu kutoka msajili
wa vyama vya Siasa Tanzania.
Kuhusu hali ya amani inayoendelea kuwepo
Nchini Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa amesema kwa vile Amani ni itikadi
iliyoota mizizi ndani ya Chama cha Mapinduzi kila mfuasi wa chama hicho
anatakiwa kuikumbatia kwa mahaba yake yote itikadi hiyo muhimu kwani bila ya hali
hiyo Taifa halitaweza kuleta Maendeleo.
Akitoa Taarifa Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho
la Vyuo Vikuu Tanzania Hamid Saleh Muhina amesema shirikisho hilo limeundwa kwa
lengo la kuwaandaa Vijana katika
mazingira ya kisasa ya sayansi na Teknoloji ili wawe viongozi bora wa hapo baadaye.
Amesema mpango huo ndio njia pekee
itakayoliwezesha Taifa kuwa na hazina kubwa ya vijana wasomi watakaokuwa na
uwezo wa kutekeleza majukumu yao katika mfumo wa mtandao wa mawasiliano ya
kisasa.
Akielezea suala la kufutwa kwa uchaguzi Mkuu
Mwenyekiti huyo wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Nchini Tanzania amevitaka vyama vya siasa ambavyo bado
havijaamua kushiriki uchaguzi wa marejeo kutafakari kwa makini maamuzi yao ili
wananchama wao wasipoteze haki yao ya Kidemokrasia ya kuchagua Viongozi
wanaowataka.
Washiriki hao wa Kongamano la maadhimisho ya
kutimia miaka 39 ya Chama cha Mapinduzi wameuhakikishia Uongozi wa Juu wa Chama
hicho kuwa mbali ya kusimamia uchaguzi wa marejeo ifikapo Tarehe 20 Mwezi wa Machi
pia watashiriki vyema kupiga kura kwenye uchaguzi huo ili kukamilisha haki yao
ya Kidemokrasi.
Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
4/2/2016.
0 comments:
Post a Comment