Mgogoro wa uchaguzi visiwani Zanzibar umeingia katika sura
nyengine baada Wawakilishi na Madiwani wateule wa Chama Cha Wananchi CUF
kufikiria kwenda mahakamani kutetea uongozi wao.
Wamesema tayari viongozi hao walishachaguliwa na kukabidhiwa hati
zao za ushindi kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, na hadi
sasa hakuna mgombea wa nafasi hizo kutoka chama chochote aliyekwenda mahakamani
kupinga uteuzi wao.
Msimamo huo wa CUF umetolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim
Seif Sharif Hamad, katika mkutano maalum wa Chama hicho uliofanyika viwanja vya
“nngoma hazingwa” Chake Chake Pemba.
Mkutano huo umewajumuisha viongozi wa Wilaya, Majimbo na Jumuiya
za Chama hicho Kisiwani humo ambapo pia teyari ulishafanyika jana kwa upande wa Unguja.
Maalim Seif aliekuwa mgombea Urais wa Chama hicho amesema viongozi
hao waliochaguliwa na wananchi na kupewa shahada zao, watakwenda mahakamani
kutetea nafasi zao, na kutoruhusu viongozi wengine wa ngazi hizo kuchaguliwa
tena kwa vile wao wanavyo vielelezo vyote vya kuchaguliwa kwao.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi yaliyobandikwa katika vituo vya
kupigia kura na kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo, majimbo
yote 18 ya uchaguzi Kisiwani Pemba yalichukuliwa na CUF, sambamba na wadi zote
32 za uchaguzi.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amewapa matumaini wafuasi wa
Chama hicho kwamba atatangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na
hatimaye kuiongoza Zanzibar.
Amerejea kauli yake kuwa wanachokifanya watawala hivi sasa ni
kuchelewesha kumtangaza, lakini hakuna namna yoyote ya CCM kuendelea kuongoza
Zanzibar baada ya uchaguzi wa 2015 na kwamba uongozi uliopo sasa ni batili kwa
mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Amesema Jumuiya na waangalizi wote wa uchaguzi wa kitaifa na
kimataifa wameshuhudia uchaguzi huo na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru, haki na
wa uwazi na wanaendelea kushikilia msimamo wao kutaka mshindi wa uchaguzi huo
atangazwe.
Amesisitiza kuwa Chama chake hakitoshiriki uchaguzi wa marudio
uliopangwa kufanyika tarehe 20/03/2015, kauli ambayo pia imeungwa mkono na
wafuasi wa Chama hicho kisiwani Pemba, kama ilivyokuwa kwa upande wa Unguja.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui,
amemtaja Maalim Seif kuwa kiongozi aliyebobea kisiasa na anayejali maslahi ya
Wazanzibari.
0 comments:
Post a Comment