Vijana wametakiwa kujitambua na kuacha
kuchezewa kiakili kunakosababisha kujiingiza katika wimbi la matatizo ya
kimaisha.
Mkurugenzi na muasisi wa Jumuiya ya kuelimisha
jamii katika masuala ya maendeleo na ustawi wa Jamii Zanzibar {Wide} Bi Rehema
Mwinyi amesema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa kimaisha uliopo sasa kundi
hilo hasa wale wanaopata elimu wanapaswa kutumia taaluma yao katika kutafuta
maisha kupitia mfumo wa ujasiri amali badala ya kusubiri ajira chache zilizopo
Serikalini.
Bibi Rehema Mwinyi ameeleza hayo alipokuwa akizungumza
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika
kujitambulisha rasmi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar akiuongozana Ujumbe wa
Viongozi Watatu wa Jumuiya hiyo.
Amesema mradi wa kuleta shukrani kwa jamii
kufuatia wanajumuiya hiyo kufaidika na misaada ya Serikali katika
kuwaandaa Kitaaluma umelenga kuyajengea uwezo wa kiujasiri amali makundi
ya Wanawake na Vijana hapa Zanzibar.
Amesema wapo Vijana na akina mama wengi
mitaani waliobarikiwa kuwa na vipaji vya kujiendesha kimaisha lakini
wanashindwa kuvitumia ipasavyo kutokana na ufinyu wa Taaluma pamoja na mitaji
ya kuanzia miradi wanayoamua kuianzisha.
Mkurugenzi huyo wa Wide Zanzibar Bibi Rehema
ameeleza kwamba mradi huo umelenga kuanzisha matamasha kwa ajili ya kuibua
vipaji hivyo katika Nyanja mbali mbali ili kuwatengeneza kwa faida yao ya
baadae.
Naye Mshauri wa Jumuiya ya Wide Zanzibar Bwana
Said Alawi alisema ipo mipango ya muda mrefu ya Jumuiya hiyo katika kutoa elimu
ya kuliendeleza bonde la Uwanja wa Farasi liliopo Kwahani Mjini Zanzibar
lengo likiwa ni kulirejeshea hadhi yake ya
asili ya kuwa sehemu za Burdani na si kuwa eneo hatarishi.
“ Eneo hilo lilipata umaarufu wa kuitwa uwanja
wa Farasi kutokana na watu wengi kulitumia kwa burdani ya michezo ya Farasi
miaka mingi iliyopita ”. amesema.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Jumuiya ya Wide inapaswa kuendelea kuwaongoza
Vijana njia yenye muelekeo sahihi wa maisha yao.
Akigusia suala la mazingira ambalo limo ndani
ya mpango kazi wa Jumuiya hiyo Balozi Seif amesema mazingira yaliyopo
nchini hivi sasa yamechafuka katika maeneo mengi kutokana na usimamizi mbovu wa
watendaji wa Halmashauri za Wilaya pamoja na Serikali za Mitaa.
Alisema ipo tabia ya baadhi ya watu kutafuta
nafasi ndogo zilizomo ndani ya mitaa na kuzitumia katika kuanzisha miradi
inayochafua mazingira na hatimae kusumbua jamii.
0 comments:
Post a Comment