Wafuasi wa Chama Cha Wananchi CUF, wameunga mkono tamko
lililotolewa na Baraza Kuu la Uongozi la Chama hicho la kutoshiriki uchaguzi wa
marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20/03/2016 Visiwani Zanzibar.
Wanachama hao kupitia viongozi wao wa Wilaya na Majimbo ya Unguja,
wameunga mkono tamko hilo baada ya kupata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu
wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye mkutano maalum uliofanyika
ukumbi wa Majid Kiembe Samaki Zanzibar.
Wamesema hakuna sababu ya kushiriki uchaguzi huo ambao wamesema ni
wa kulazimisha na hauwezi kuwa huru na wa haki.
Wameeleza kuwa uchaguzi halali, huru na wa haki ulishafanyika
Oktoba 25, 2015 na wananchi wengi walimchagua mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif
Hamad lakini ulifutwa bila ya kuwepo sababu za msingi.
Mapema akizungumza na viongozi hao wa CUF ngazi ya Wilaya na
Majimbo kwa upande wa Unguja, Maalim Seif amesema Chama hicho hakitorudi nyuma
katika kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba 2015.
Amesema licha ya Chama hicho kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa
marudio, juhudi mbali mbali zinaendelea kufanywa kuhakikisha kuwa Chama Cha
Mapinduzi CCM kinaondoka madarakani.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar Maalim Seif amesema siasa za
nguvu na kimabavu zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi hazitoisaidia Zanzibar
na badala yake zinaweza kuzidisha mgogoro uliopo.
Maalim Seif ameishutumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuingilia
uchaguzi wa Zanzibar na kupelekea kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na
kikatiba.
Maalim Seif pia amewashutumu baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini
wanaojaribu kupotosha ukweli na kuunga mkono uamuzi batili wa kurejewa uchaguzi
uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu vikao vya kutafuta muafaka wa mkwamo wa
kisiasa vilivyokuwa vikifanyika Ikulu ya Zanzibar, Maalim Seif amesema katika
vikao hivyo walijadiliana na kukubaliana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
imepoteza sifa ya kusimamia uchaguzi, lakini ameshangazwa na kitendo cha Tume
hiyo hiyo kutangaza uchaguzi wa marejeo, huku viongozi wa CCM walioshiriki
mazungumzo hayo wakiunga mkono.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF Ismali Jussa
Ladhu,
akizungumza na viongozi hao
wa Wilaya na Majimbo ya Unguja |
Baadhi ya viongozi wa Wilaya na Majimbo wa CUF upande wa Unguja,
wakijitokeza kumsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho
Maalim Seif Sharif Hamad, huko ukumbi wa Majid Kiembe Samaki.
|
0 comments:
Post a Comment