February 03, 2016

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewatahadharisha watumiaji wa simu za mikononi kuhakikisha simu wanazotumia zinakidhi viwango vinavyohitajika  kwani zile zote bandia zitafungwa na kukosa mawasiliano hadi Juni 17 mwaka huu.
Meneja mawasiliano wa TCRA makao makuu Tanzania Innocent Mungi amesema simu hizo pamoja na vifaa vyengine vya mawasiliano vya mikononi vina namba maalum inayovitambulisha iwapo ina viwango au laa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar amesema mfumo huo mpya wa kutambua rajisi za namba za simu unalengo la kuhakikisha watumiaji wa simu wanakuwa salama ikiwemo kuepuka wizi wa simu na itakuwa haiwezi kutumika tena iwapo itaibiwa ama kuokotwa na mtu mwengine.
kila kifaa cha mawasiliano ya mkononi kina namba maalum inayojulikana kama IMEI iliyopo katika mifumo ya viwango vya mawasiliano vya kimataifa  inayokitambulisha kama ni bandia au halisi” amesema.
 Meneja Mungy amefahamishakuwa lengo la kuwepo kwa mfumo huo ni kuhakikisha wanafuatilia kwa urahisi vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano ili visiweze kufanya kazi katika mitandao ya mawasiliano.
Amesema kifungu cha 84 cha sheria mawasiliano ya kielectroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 kinataka kuwepo kwa mfumo huo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano ya mkono.
“Sheria hiyo katika kanuni zake za mwaka 2011 kuhusu mfumo wa rajis ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano hayo inawataka watoa huduma kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vinavyotumika kwenye mitandao yao.” amesema Mungy.
Akitoa ufafanuzi ameongeza kuwa mfumo wa urajisi utakuwa na aina tatu za kumbukumbu  ambazo ni orodha ya namba tambulishi zinazoruhusu vifaa vyake, orodha ya namba tambulishi zilizotolewa taarifa kuwa zimefungiwa na namba tambulishi zilizofungiwa kwa muda au kuruhusiwa kwa muda.
“Ikitokea simu ya mtumiaji imefungiwa kimakosa anatakiwa kutoa taarifa kwa mtoa huduma wake ili iweze kufunguliwa kwani simu zote zilizofungwa kimakosa baada ya wahusika kujiridhisha zitatakiwa zifunguliwe ndani ya masaa 24”. ameeleza  Meneja huyo.
Amezitaja faida za matumizi ya mfumo huo kuwa ni pamoja na kuwepo utii wa sheria kifungu cha 128 cha EPOCA kinachomtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa simu au laini kwa watoa huduma wa makampuni ya simu ili wachukue hatua za haraka kutatua tatizo hilo.
Amesema faida nyingine ni kuthibiti wizi wa simu, iwapo mtu atapoteza au kuibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma simu hiyo itafungwa ili isitumike katika mtandao wowote.
 Nae Naibu mkurugenzi masuala ya watumiaji huduma za mawasiliano, Thadayo Ringo amesema ili kutambua namba tambulishi ya simu ya kiganjani au vifaa vya mawasiliano ya mkononi , mtumiaji anatakiwa aandike tarakimu *#06# kwa kutumia kifaa chake na baada ya kufanya hivyo itakuja namba ndefu anayotakiwa kuitunza.
Ringo ameongeza kuwa baada ya hapo mtumiaji atahitajika kutuma ujumbe mfupi wa namba hiyo tambulishi kwenye namba 15090 atapokea ujumbe utakaomjulisha hali halisi ya simu yake  kupitia ujumbe mfupi” Kama IMEI haioani na aina ya simu yako, wasiliana na aliyekuuzia na  usipoweza ,ibadilishe kabla ya juni 2016 kwani simu hiyo inaweza kuwa bandia.
Kaimu Meneja Mkuu wa TCRA Kanda ya Zanzibar, Seif Waziri amesema mamlaka hiyo ina mikakati ya kuhakikisha wananchi wanatumia vifaa vya mawasiliano ya kielectoroniki vyenye  salama katika matumizi.
 Pamoja na hayo ameviomba vyombo vya habari na taasisi zingine za kutoa elimu kuendelea kuwaelimisha wananchi kufuata utaratibu huo  uliowekwa na TCRA kwa lengo la kuweka matumizi mazuri ya mawasiliano kwa maslahi ya wananchi wote.
Kwa mujibu wa tafiti ndogo iliyofanyika TCRA kwa baadhi ya mikoa mbali mbali Tanzania  inaonyesha kuwa Zaidi ya asilimia 38 hadi 40 ya simu zinazotumika nchini ni bandia na hazifai kwa matumizi ya mawasiliano Tanzania.

Kaimu Meneja Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Zanzibar
TCRA Ndg Seif  S Waziri akizungumza wakati wa mkutano
wa waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa
hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar





Naibu Mkurugenzi Masuala ya Watumiaji wa Huduma
 za Mawasiliano Thadayo Ringo akionesha mfano wa simu
orijino kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano huo .

Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya TCRA Innocent Mungy,
 akitowa maelezo kwa waandishi wa habari baada ya kuangalia
 simu zao baada ya kuingiza namba hizo na kugunduwa kuwa
uhalisia wa simu zao



Mwandishi Amour Mussa akiuliza suali
katika mkutano huo wa TCRA

0 comments:

Post a Comment