February 12, 2016

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameithibitishia rasmi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kujiondoa kuwania wadhifa huo katika Uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu.
Mbali na Maalim Seif, wagombea wote wa chama hicho wa nafasi ya Uwakilishi na Udiwani wamejiondoa kwa kuwasilisha barua rasmi kuwa hawatoshiriki uchaguzi huo wa marudio wa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, amesema Maalim Seif amewasilisha waraka wa barua wa kujiondoa kwa Zec, Febuari 8, mwaka huu.
Amesema hatua aliyochukuwa mgombea huyo ni utekelezaji wa wa azimio la Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kutoshiriki uchaguzi mkuu wa marudio visiwani hapa.
Shehe alisema kuwa Zec imetakiwa kutotumia jina wala picha za Maalim Seif  na taarifa zozote katika karatasi za wapigakura kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Alisema kuwa katika Barua yake Maalim seif amesisitiza kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana ulikuwa uchaguzi huru na wa haki na Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha salim Jecha hakuwa na mamlaka ya Kikatiba na sheria kufuta matokeo ya Uchaguzi huo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Salum Kassim alisema jana kuwa ni mapema kueleza vyama vingapi vimekamilisha kuthibitisha wagombea wake kama wapo hai na watashiriki uchaguzi kabla ya kufanyika Machi 20, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment