March 28, 2016




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MKUTANO WA MWANZO WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na taratibu za uendeshaji wa Baraza la Wawakilishi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na mahala pa kufanyika Mkutano wa mwanzo wa Baraza jipya. Kutokana na msingi huo wa kikatiba, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ameitisha Mkutano wa Mwanzo wa Baraza Jipya la Tisa la Wawakilishi tarehe 30 Machi, 2016 katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Zanzibar.
Usajili wa Wajumbe wote
Kabla ya kuanza rasmi shughuli za mkutano wa Kwanza wa Baraza jipya, kutakuwa na usajili wa wajumbe wote siku ya Jumatatu ya tarehe 28 March, 2016 zowezi ambalo litaenda sambamba na upigaji picha kwa ajili ya Vitambulisho vya wajumbe hao.
Mikutano ya Vyama (Parties Caucus) na Briefing ya Wajumbe wote.
Kwa kawaida kabla ya kufanyika mkutano wowote wa Baraza kunakuwa na Mikutano ya vyama ya siasa pamoja na Briefing ya wajumbe wote. Katika Mkutano huu wa Kwanza wa Baraza Jipya shughuli hiyo itafanyika siku ya Jumanne ya tarehe 29 March, 2016.
Shughuli za Mkutano wa Kwanza wa Baraza Jipya la Tisa la Wawakilishi
Ndugu waandishi wa habari,
Madhumuni ya kuzungumza nanyi ni kuwafahamisha nyinyi na kupitia kwenu kuwafahamisha wananchi kwa ujumla kuhusu kuanza kwa Baraza la Tisa la Wawakilishi na shughuli zinazotarajiwa kufanywa na Baraza hilo katika mkutano wake wa Kwanza, kwa mujibu wa Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012.
Uchaguzi wa Spika wa Baraza la Wawakilishi
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na Kanuni za Baraza la Wawakilishi (Toleo 2012), uchaguzi wa Spika ndio shughuli ya mwanzo kufanyika katika mkutano wa mwanzo wa Baraza jipya na kwamba hakuna shughuli yoyote itakayofanyika katika Baraza wakati nafasi ya Uspika iko wazi, isipokuwa uchaguzi wa Spika.
Kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kinaweza kusimamisha mgombea wa nafasi ya Spika. Mtu anayeweza kugombea nafasi ya Uspika wa Baraza la Wawakilishi anapaswa ama awe Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi au awe na sifa za kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Hadi kufikia tarehe ya mwisho ya vyama kuwasilisha majina ya wagombea wao katika Tume ya Uchaguzi ni Mjumbe mmoja ambae amewasilisha jina lake ambapo tayari Tume ya Uchaguzi imeshawasilisha jina lake kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Kuapishwa kwa Wajumbe wa Baraza
Mara baada ya kuapishwa kwa Spika wa Baraza, naye ataawapisha Wajumbe wote wa Baraza Kiapo cha Uaminifu, mmoja baada ya mwengine. Wajumbe hao wanapaswa kula kiapo cha uaminifu kabla ya kutekeleza shughuli yoyote ya Baraza kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar isipokuwa wanaweza kumchagua Spika hata kabla hawajaapishwa.
Uchaguzi wa Naibu Spika
Shughuli nyengine inayotarajiwa kufanywa katika Mkutano wa Kwanza wa Baraza jipya la Tisa ni uchaguzi wa Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi. Wenye sifa za kugombea nafasi hiyo ya Naibu Spika ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pekee. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, nafasi hiyo inatakiwa ijazwe katika Mkutano wa Mwanzo wa Baraza jipya.
Rais kulihutubia Baraza la Wawakilishi
Katika Mkutano huu wa Baraza, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi anatarajiwa kulihutubia Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Kikatiba. Taarifa ya Rais kulihutubia Baraza la Wawakilishi itatolewa rasmi na Spika wa Baraza la Wawakilishi baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka kwa Mhehimiwa Rais. Wajumbe wanaweza kutoa hoja kutaka hotuba hiyo ya Rais ijadiliwe katika Baraza la Wawakilishi, ingawa kwa mujibu wa Kanuni za Baraza la Wawakilishi, hotuba hiyo itajadiliwa katika mkutano wa Baraza unaofuata.
Uchaguzi wa Wajumbe wa Tume ya Bajeti ya Baraza
Aidha katika Mkutano huu wa mwanzo wa Baraza la Tisa, Wajumbe wa Baraza wanatarajiwa kufanya uchaguzi wa Wajumbe wanaoingia katika Tume ya Bajeti ya Baraza. Tume hii ndiyo yenye mamlaka ya kuidhinisha Bajeti ya mwaka ya Baraza la Wawakilishi. Kwa kuzingatia kuwa, matayarisho ya Bajeti kwa mwaka 2016/2017 yanapaswa kukamilika muda mfupi ujao, kuna umuhimu wa kufanya uchaguzi wa Wajumbe watano wanaoingia katika Tume hii kutoka miongoni mwa wajumbe wasio Mawaziri au Naibu Mawaziri, ili hatimaye Tume hiyo iweze kutafakari na kuidhinisha Bajeti ya Baraza la Wawakilishi.
Kimsingi hizo hasa ndiyo shughuli za mkutano wa Mwanzo wa Baraza jipya zinazotarajiwa kufanywa na Baraza la Tisa la Wawakilishi. Hata hivyo, Kanuni za Baraza la Wawakilishi zinaruhusu kufanywa kwa shughuli nyengine kwa ajili ya kukamilisha kuundwa kwa Baraza jipya kwa ukamilifu, kwa maana ya kujaza nafasi zote zilizo wazi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012. Shughuli hizo zinaweza kuhusisha uchaguzi wa Wenyeviti wawili wa Baraza na Uchaguzi wa wajumbe watano watakaoingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

(Dkt. Yahya Khamis Hamad)
Katibu,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.
Tarehe 27 March, 2016

0 comments:

Post a Comment