February 12, 2016

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kuendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu waliohusika na tukio la kuchoma moto  Mashamba Matatu ya Mikarafuu yenye ukubwa wa Ekari Tisa huko katika Shehia ya Mzambarauni Mtambwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema wahusika hao wa kuhujumu uchumi wa Taifa wanapaswa kupambana na mkondo wa dola kutokana na vitendo vyao vinavyorejesha nyuma mbali ya Maendeleo ya Taifa kwa jumla  lakini pia kuviza vipato vya Wananchi wanaotegemea mashamba hayo.
Balozi Seif Ali Iddi ametoa agizo hilo mara baada ya kuyakagua mashamba hayo yaliyopata kadhia hiyo karibu Wiki moja iliyopita na  kusababisha hasara yenye thamani inayokisiwa kufikia shilingi Milioni 24, 525,000/-.
Ameisema tabia ya baadhi ya watu kuendelea kufanya vitendo vya hujuma kwa kufikiria kwamba wanaikomoa Serikali Kuu waelewe kwamba wanakwenda kinyume na maamrisho ya Dini kwa vile vitendo vya vimekuwa vikileta hasara kwa Wananchi wenzao katika maeneo yao.
Amesema Jeshi la Polisi linapaswa kusimaia ipasavyo udhibiti wa vitendo viovu zinavyoonekana kushamiri katika baadhi ya maeneo vikihusihwa zaidi na itikadi za Kisiasa ambazo hazina msingi wala hatma njema kwa jamii na Taifa kwa pamoja.
Ametahadharisha kwamba zao la Karafu bado linaendelea kuwa muhimili wa Uchumi wa Visiwa vya Zanzibar. Hivyo vitendo vya watu hao vinaashiria wazi vikilenga kuhujumu mapato ya Taifa.
“ Hii ni hujuma iliyofanywa kwa makusudi na watu wasiyoitakia mema nchi yetu hasa ikilinganishwa  na mazingira  halisi ya mashamba yenyewe”. amesema Balozi Seif.
Mapema Mwakilishi wa Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo na Maliasili Kisiwani Pemba ambae pia ni Afisa Misitu Idris Hassan Abdulla amesema hujuma hiyo imeathiri jumla ya Mikarafuu 151ambapo kati ya hiyo Mikarafuu  36 haitofufuka tena kutokana na moto huo.
amesema Mikarafuu 115 katika mashamba hayo Matatu ambayo moja linamilikiwa na Serikali inaweza kuendelea kuzaa karafuu si zaidi ya miaka Mitatu kulingana na hali halisi ya mazingira ya miti hiyo kwa vile ina maji maji ya mafuta.
Amesema ukanda wa Kaskazini ya Kisiwa cha Pemba bado una  mashamba mengi ya Serikali yenye mikarafuu ambayo yamekuwa yakihudumiwa na baadhi ya wananchi ambao tayari wameshawasilisha maoni Serikalini kwa kutaka kumilikishwa rasmi.
Naye Mmoja wa Wananchi wanaosimamia huduma za mashamba hayo Mzee Khamis Chande ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa mkusaidia nguvu katika juhudi za kuyaendeleza mashamba hayo kwa vile tayari ameshatumia fedha nyingi katika kuhusisha miti ya Mikarafuu.
Mzee Khamis amesema kutokana na hujuma hiyo ya moto ndani ya mashamba hayo kwa sasa anahitaji msaada wa ziada katika kuona juhudi alizochukuwa za kuyaendeleza mashamba hayo zinaendelea kama kawaida licha ya hujuma hiyo.
Amesema tayari ameshatumia zaidi ya shilingi Milioni Moja na Nusu katika kuyafanyia usafi pamoja na kuotesha miti mipya ya Mikarafuu na ameushukuru Uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, Idara ya Misitu pamoja na Uongozi wa Serikali ya Mkoa huo kwa kumpa mashirikiano makubwa baada ya kutokea kwa hujuma hizo.
Amesema kitendo hicho kimempa faraja kubwa jambo ambalo aliahidi kuendeleza jitihada hizo baada ya kuelewa faida na umuhimu wa kuimarisha zao la Karafuu ambalo kwa sasa ndio utio wa Mgongo wa Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman amemueleza Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali ya Mkoa wake itajipanga katika kuona Eneo hilo linaimarishwa na kurejea katika haiba yake ya asili.
Mh. Omar amesema mipango hiyo italengwa zaidi kwenye siku ya Mazingita Duniani kwa kuwashirikisha Watendaji wa Taasisi za Maingira, Wanafunzi, Wananchi pamoja na Wakulima washirikia vyema katika upandaji Miti mipya ya Mikarafuu katika eneo hilo lililoathirika kwa moto.
Hadi sasa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linamshikilia Mtu Mmoja akituhumiwa kuhusika na vitendo vya utiaji Mtoto mashamba hayo ya Mikarafuu Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mzee Khamis Chande Mkaazi wa Mzambarauni anayeshughulikia 
Mashamba ya Serikali ya Mikarafuu  aliiomba Serikali kupitia 
Balozi Seif isaidie nguvu za uwezeshaji wa mashamba hayo baada ya 
kutumia nguvu  nyingi za Fedha katika kuyahuisha mashamba hao.






Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/2/2016.

0 comments:

Post a Comment