Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ameagiza kufutwa mikataba yote ya makubaliano ya ukodishwaji wa
Nyumba za Serikali zilizojengwa maalum kwa kuwasaidia Wananchi wa kipato cha
Chini unayofanywa kijanja na baadhi ya watu pamoja na
Kampuni binafsi.
Alisema tabia hiyo iliyojengeka kwa muda mrefu sasa inatumiwa na
wajanja hao wanaokodishwa Nyumba na Serikali na baadaye kubuni mikataba
mipya ya kuwakodisha watu wengine kwa nia ya kupata faida kubwa zaidi (Maarufu
kilemba).
Balozi Seif Ali Iddi ametoa Kauli hiyo alipofanya ziara fupi ya
kufuatilia Mikataba ya Wafanyabiashara waliokodishwa milango ya Maduka
katika Jumba la Maendeleo Nambari Kumi Michenzani Mjini Zanzibar ambayo
baadhi ya waliokodishwa milango hiyo na Serikali tayari wameshaikodisha
kwa watu wengine.
Amesema tabia ya baadhi ya Watu hao kutumia mali za Serikali
walizopewa kwa misingi ya kupunguza ukali wa maisha na kuwauzia au
kuwakodisha watu wengine waelewe kwamba wanafanya dhulma na dhambi kubwa.
Balozi Seif ameupongeza Uongozi wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC)
kwa uamuzi iliyochukuwa ya kuwafutia mikataba wajeta wake wa mwanzo iliyowapa
milango la Maduka na wakaamua kuikodisha kwa watu wengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameonya kwamba tabia
kama hiyo imejengeka pia katika Nyumba zilizowekwa Wakfu na kuishauri Kamisheni
ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar kufanya utafiti na kuwabaini wapangaji wake
wenye tabia kama hiyo.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Zanzibar Moh’d
Hafidh Rajab amesema Watendaji wa Shirika hilo wameanza ukaguzi Maalum wa
kuzipitia Nyumba zote za Serikali zilizokodishwa kwa watu na Taasisi tofauti
hapa Nchini.
Hafid amesema ukaguzi huo utatoa fursa kwa Uongozi wa Shirika
hilo kufanya marekebisho ya kodi zilizofungwa katika mikataba ya zamani
ili iende na wakati na soko liliopo hivi sasa.
Amesema Shirika la Nyumba la Zanzibar lililoasisiwa hivi
karibuni baada ya kupata baraka za Baraza la Wawakilishi Zanzibar linahitajika kujitegemea
wenyewe badala ya kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu.
Akitoa shukrani zake Mmoja wa wamiliki wa Maduka yaliyopo
Michenzani ambae ni Meneja wa Kampuni ya A l – Salam na Seib Ruila Yussuf
Juma Msanif ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika
lake la Nyumba kwa uamuzi wake wa kukagua majengo yake mbali mbali.
Yussuf amesema uamuzi huo wa busara na hekima umewapa faraja wao
binafsi na Kuliomba Shirika la Nyumba kufikiria upya kodi zake inazotoza
kwa lengo la kuwapa tahfifu Wafanyabiashara wachanga ili kuwa na uwezo mzuri wa
kulipa kodi.
Mlango mmoja wa Duka hapo Michenzani ulikuwa ukikodishwa Mteja
kutoka Serikalini kwa Shilingi elfu Thamanini kwa Mwaka wakati mkodishwa huyo
anaamuwa kukodisha tena kwa Mtu wa Pili wa Dola za Kimarekani mia
450 kwa mwaka sawa na Shilingi Laki Tisa na Thamanini (980,0000) za
Kitanzania.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alikutana na Kamati ya Taifa ya Sherehe za Maulidi ya kuzaliwa
Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW }.
Kamati hiyo aliyokutana nayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wake Sheikh Sherali Shamsi alimuelezea
matayarisho yanayoendelea ya Maulidi hayo yanayofanyika Kitaifa kila mwaka hapa Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
11/12/2015.
0 comments:
Post a Comment