December 12, 2015

Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar imebaini kuwepo mianya ya rushwa inayotumika katika baadhi ya taasisi za umma za serikali.

Kutokana na hali hiyo imejaribu kutoa ushauri wa kuimarisha mifumo ya utendaji wa taasisi hizo ikiwemo Idara ya usafiri na Leseni, Halmashauri ya wilaya ya Magharibi na Idara ya vizazi na vifo ili kuondosha vitendo vya ubadhirifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa katika taarifa ya taasisi hiyo kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya siku ya mapambano ya kuzia rushwa duniani yenye kauli mbiu “Kata minyororo ya rushwa” imefanikiwa kupokea  malalamiko 125, sitini na sita kati yao yamefanyiwa uchunguzi na 10  yamefikishwa afisi  ya mkurugenzi wa mashtaka ili kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika malalamiko hayo pia tuhuma 45 zimefutwa kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya vitendo hivyo.
Taarifa hiyo ilotiwa saini na Mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo Mussa Haji Ali imeeleza kuwa  bado tatizo la rushwa ni kubwa na inadumaza maendeleo ya jamii na taifa huku taasisi hiyo ikikabiliwa na changamoto kadhaa katika mapambano yake Zanzibar.
Moja ya changamoto iliyotajwa ni ushiriki wa mdogo wa jamii kutokana na uelewa wao mdogo juu ya athari za rushwa huku wakiwa na matumani ya kupata mabadiliko makubwa ya kulimaliza hasa tatizo hilo baada ya kuanzishwa taasisi hiyo.
Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar ameeleza kuwa wameandaa mpango makakati wa miaka mitano wa maadili ya kuzuia rushwa utakao sisitiza wajibu wa taasisi za serikali ili  kufanikisha vita dhidi ya tatizo hilo nchini.

0 comments:

Post a Comment