Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limekanusha
uvumi ulionea kwamba litasitisha huduma ya kuuza umeme kwa siku kadhaa na
kusababisha ghofu kwa wateja na kupelekea msongamano katika vituo vya
kununulia umeme vya Shirika hilo katika siku za karibuni.
Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini
kwake Makadara, Meneja Mkuu wa ZECO ndugu Hassan Ali Mbarouk amesema kuongezeka
kwa wateja katika vituo vya kuuzia umeme vya Shirika hilo kumesababishwa
kukosekana huduma hiyo kwa kutumia simu za mkononi za Zantel kwa Easy pesa.
Ndugu Mbarouk amesema huduma ya kununua umeme
katika vituo vyote vya ZECO itaendelea kama kawaida kwa siku zote na hakutakuwa
na kuzimika wala kusita kuuza umeme katika vituo hivyo.
Hata hivyo amesema huduma ya kununua umeme
kwa kutumia simu za mkononi kwa njia ya easy pesa itaendelea
kukosekana na amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati huu ambapo ZECO
na Zantel wanaendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo lililojitokeza.
Amesema kukosekana huduma hiyo kwa
njia ya easy pesa imesababishwa na mfumo huo kupata matatizo
kuanzia tarehe 20 mwezi uliopita.
Amewahakikisha watumiaji wa umeme kwamba tatizo
hilo litapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho kwani mkataba wa mwanzo
wa miaka miwili wa ZECO na Zantel utakapo malizika mkataba mpya utatoa
fursa kwa mashirika mengine ya simu kuingia mkataba wa kuuza umeme.
Akizungumzia zoezi linaloendelea la
kubadilisha mita za zamani na kuweka mita za Tukuza, Menaja Mkuu amesema
Shirika limepanga itakapofika mwishoni mwa mwaka 2017 wateja
wote wa umeme watakuwa wanatumia mita za Tukuza.
Amesema pamoja na mafanikio makubwa waliyopata
ya kubadilisha mita za zamani wanawasi wasi kwa baadhi ya wateja wasiowaaminifu
kuzihujumu mita za Tukuza na kulikosesha fedha shirika kwani mita hizo
zinachukua muda mkubwa kukaguliwa baada ya kuwekwa tafauti na mita za zamani
ambazo hukaguliwa kila mwezi.
Meneja Biashara wa Shirika la umeme Zanzibar
ndugu Thabit Salum Khamis amewaeleza waandishi wa habari kuwa usambazaji umeme
katika visiwa vya Unguja na Pemba umefikia asilimia 86 lakini watumiaji umeme
ni chini ya asilima 50.
Ndugu Thabit amewataka wananchi kubadili mfumo
wa maisha kwa kutumia zaidi umeme kwani ni rahisi kwa
matumizi ya nyumbani ikilinganishwa na nishati ya kuni na mkaa.
:Maelezo Zanzibar
:Maelezo Zanzibar
0 comments:
Post a Comment