Kikosi Maalum cha uchunguzi wa Miripuko cha
Jeshi la Polisi Tanzania kinaendelea kufanya uchunguzi wa kina kufuatia mripuko
wa bomu uliotokea kwenye Kontena na Maskani ya Chama cha Mapinduzi ya
Kisonge iliyopo Mtaa wa Michenzani Mjini Zanzibar majira ya saa
sita usiku wa kuamkia leo.
Mripuko wa bomu hilo kwa hatua za awali
linalokisiwa kutengenezwa kienyeji ulileta mtafaruk mkubwa kwa wakaazi wa eneo
zima la nyumba za Maendeleo Michenzani pamoja na mitaa jirani.
Mmoja wa miongoni mwa watu walioshuhudia
mripuko huo Bwana Shaaban Said alisema kwamba aliona kikundi cha vijana
wasiopungua Sita waliovalia kanzu na vitambaa vyeupe kichwani wakiwa
ndani ya gari ndogo aina ya Keri wakionekana kulizunguuka Kontena hilo.
Bwana Shaaban alisema dakika mbili baadaye
aliiona gari hiyo ikiondoka kwa mwendo wa kasi na kufuatia na mlio mkubwa wa
mripuko pembezoni mwa Kontena hilo uliosababisha baadhi ya vioo vya madirisha
ya nyumba za michenzani kupasuka pasuka.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya
Taifa ya CCM ambae pi ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alifika eneo la tukio hilo kujionea hali halisi ya tukio hilo la kusikitisha.
Katibu wa Maskani ya CCM Kisonge Ndugu Mzee
Yunus alimueleza Balozi Seif kwamba vipo baadhi ya vifaa vilivyoathirika
kutokana na mripuko huo kwenye kontena hilo wanalolitumia zaidi kama stoo kwa
ajili ya kuhifadhia vitu vyao licha ya kutofafanua zaidi gharama halisi
iliyotokana na mripuko huo.
Nd. Yunus kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliiomba Serikali kuimarisha zaidi ulinzi katika maeneo ya Umma ili
kusaidia kupunguza matukio ya hujuma yanayofanywa na baadhi ya watu ambazo
hujuma nyengine zina muelekeo wa chuki za Kisiasa.
Akitoa pole kwa Viongozi na Wanachama wa Chama
cha Mapinduzi Maskani Kaka ya Kisonge Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema uchochezi huo wa hujuma
haiufai na ni mbaya hasa wakati huu Taifa likielekea kwenye uchaguzi.
Balozi Seif alielezea masikitiko yake kutokana
na vitendo hivyo vya kihuni vinavyofanywa na baadhi watu katika baadhi ya
maeneo hapa nchini ambavyo havitoi sura nzuri mbele ya uso wa Dunia.
Akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali aliviagiza
Vyombo vya ulinzi kufanya uchaguzi wa kina wa tukio hilo la hujuma na kuwabaini
wahusika wa tukio hilo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Balozi Seif aliendelea kusisitiza kwamba nia
ya Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi
ya Zanzibar ni kuona kwamba Wananchi wote wanaishi katika hali ya amani
na utulivu.
0 comments:
Post a Comment