Kampuni ya simu Zantel, imeendelea kuipa
msukumo sekta ya elimu Zanzibar, mara hii ikitoa msaada wa shilingi milioni
kumi kwa Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar kwa ajili ya kununulia vitabu na
uendeshaji wa shughuli zake.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika
leo katika jengo la maktaba hiyo Maisara mjini Zanzibar, Ofisa Mtendaji Mkuu wa
kampuni hiyo Benoit Janin, amesema msaada huo unalenga kusaidia upatikanaji wa
maarifa miongoni mwa jamii ya Wazanzibari.
Janin amesema, ni miongoni mwa majukumu
na wajibu wa Zantel, kuhakikisha inatoa huduma bora na zenye ufanisi
zinazokidhi mahitaji ya wakaazi wanaoishi mijini na vijijini na kurahisisha
upatikanaji wa taarifa za elimu, habari, utamaduni na burudani.
“Upatikanaji wa maarifa kwa wanajamii ni
jambo la muhimu na suluhisho la changamoto hii ni kuhakikisha tunatoa fursa
sawa kwa kuwezesha kukua kwa maktaba za jamii,” amesema Janin.
Aidha ameeleza kuwa, ni fahari kwa kampuni yao
kusaidiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuchangia ukuaji na ustawi wa
jamii.
“Tunaamini kwamba kujifunza ni muhimu
kwa maendeleo ya elimu kama moja maeneo ya shughuli zake za kusaidia jamii,” ameeleza
Ofisa huyo.
Akitoa shukurani zake kwa Zantel, Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Abdalla Mzee, ameipongeza
kampuni hiyo kwa mchango wao wa miaka mingi katika kukuza maendeleo ya elimu
Zanzibar.
“Tunafarijika na mchango wa Zantel katika
kusaidia maendeleo ya elimu nchini, na msaada huu uliotolewa leo kwa maktaba
yetu kuu utasaidia kurahisisha upatikanaji wa vitabu na hivyo kuimarisha
mazingira ya utoaji maarifa miongoni mwa Wazanzibari,” ameeleza.
Hata hivyo, ameiomba kampuni hiyo kuangalia
uwezekano wa kusaidia maeneo mengine ya kielimu yanayokabiliwa na changamoto
kadhaa, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa baadhi ya madarasa uliokwama, pamoja na
madawati.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma
za Maktaba Zanzibar Sichana Mussa Foum, ameishukuru Zantel kwa msaada huo,
akisema ni muhimu kwa wateja wa maktaba zake Unguja na Pemba.
Amefahamisha kuwa, pamoja na jitihada za
serikali kuziendeleza maktaba hizo, mchango wa taasisi nyengine unahitajika
kutoana na ongezeko la wanafunzi na wananchi wanaohitaji huduma za
maktaba.
:Maelezo
0 comments:
Post a Comment