Jumla ya wanafunzi 16,744 wamechaguliwa
kuendelea masomo ya kidatu cha tatu kati ya wanafunzi 24,051
walioandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha pili katika skuli za
Unguja na Pemba mwaka jana.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema kiwango hicho cha
ufaulu ni sawa na asilimia 69.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.0 ukilinganisha
na matokeo ya mwaka jana.
Waziri Shamhuna amesema idadi ya
wanafunzi wa kike waliofaulu ni kubwa zaidi ukilinganisha na
wanaume ambapo wanawake ni 9,794 na wanaume 6,950.
Kwa upande wa matokeo ya Darasa la saba Waziri
Shamhuna amesema jumla ya wanafunzi 24,235 kati ya wanafunzi 30,179
walioandikishwa wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza sawa na asilimia
84.5, wanafunzi 51 wamechaguliwa kujiunga na madarasa ya vipawa na
wanafunzi 621 wamechaguliwa kujiunga na madarasa ya michepuo
Akitoa tathmini kwa wanafunzi wa Darasa la
sita Waziri wa Elimu amesema kuwa jumla ya wanafunzi 25,773 wamechaguliwa
kuiungia kidato cha kwanza sawa na asilimia 99.6 ambapo wanafunzi 44
wamechaguliwa kujiunga na madarasa ya vipawa.
Akitaja Skuli zilizofanya vizuri zaidi
kidato cha pili Waziri Shamhuna amesema ni pamoja na Madungu ‘A’,
Mauwani na Mahonda . Darasa la saba ni Skuli ya
Alikhamis Camp, Mjimbini na Kangani na darasa la sita ni
Kibweni, Mkunazini na Konde.
Amezitaja Skuli zilizofanya vibaya
kitaifa kwa kidato cha pili ni Mfurumatonga, Uzi, na Mchangani,
skuli ya Chambani, Kandwi , Mwambe shamiani, Mfurumatonga, Chambani na Mahonda
wamefanya vibaya darasa la sita na saba .
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali amesema
katika mitihani hiyo kesi nne za udanganyifu zilijitokeza zote kwa wanafunzi wa
darasa la sita.
Aliwataja wanafunzi waliofanya vizuri zaidi
kidato cha pili ni Philip William Panduka kutoka Skuli ya Mikunguni,
darasa la saba ni Farid Ali Hamad kutoka Ziwani na darasa la sita ni Seif
Khamis Nassor kutoka Skuli ya Madungu ‘A’.
Waziri Shamhuna amewataka wazazi na
walezi wa wanafunzi ambao hawakufaulu mitihani hiyo kutovunjika moyo na badala
yake amewashauri kuwapeleka vituo vya kujiendeleza.
Waziri huyo wa Elimu ameahidi kufanya utafiti
na kuzifuatilia skuli zilivyofanya vibaya ili kuweza kufahamu tatizo
na kulitafutia ufumbuzi unaofaa.
Maelezo Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment