STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 08 Januari, 2016
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein ametoa changamoto kwa
watendaji wa mahkama za watoto nchini kuongeza kasi, ari na kubuni mbinu bora
zaidi zitakazowezesha mahkama hizo kumaliza kesi zao haraka.
Katika hotuba yake
mara baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Mahkama ya watoto huko Mahonda katika
mkoa wa Kaskazini Unguja leo, Dk. Shein amesema pale ambapo ushahidi wa kesi
hizo upo hakuna sababu za mahkama kuchelewesha kesi hizo.
Hata hivyo alikiri
kuwa uendeshaji wa kesi za udhalilishaji watoto umekuwa ukikumbana na mazingira
magumu hasa pale watu wanaopaswa kutoa ushahidi mahkamani wanapokataa kufanya
hivyo.
“Naamini mahakimu
hawana nia ya kuchelewesha kesi hizo lakini ukweli ni kuwa kesi hizo zina mambo
mengi magumu ikiwemo mashahidi kukataa kufika mahkamani kutoa ushahidi” Dk.
Shein alisema.
Alifafanua kuwa ni
kweli ucheleweshaji kesi za udhalilishaji watoto na wanawake unasababisha
manung’uniko kutoka kwa wananchi na taasisi zinazofuatilia kesi hizo lakini
amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendeleza jitihada zake kuhakikisha
haki za mtoto zinalindwa kwa mujibu Sheria ya Mtoto ya Zanzibar, Namba 6 ya
mwaka 2011 pamoja na mikataba mingine ya kimataifa kuhusu haki za watoto.
Alibainisha kuwa
ujenzi wa mahkama hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Miaka Mitano
(2013-2018) wa Mapitio na Marekebisho ya Sheria ya Watoto ambao umelenga
kulinda haki za watoto wenye matatizo ya kisheria.
Kwa hivyo “natoa wito
kwa taasisi zote zinazohusika katika utekelezaji wa Mkakati huo kutekeleza
wajibu wao ili waende sambamba na azma ya serikali ya kuimarisha utawala wa
sheria na dhana ya utawala bora hasa suala la zima la kulinda haki za watoto
kwa mujibu wa Sheria Namba 6 ya mwaka 2011” Dk. Shein alisisitiza.
Katika hotuba yake
hiyo Dk. Shein aliipongeza Idara ya Mahkama kwa kushirikiana na taasisi
nyingine zinazoshughulikia kesi za udhalilishaji watoto kwa kuchukua hatua
mbalimbali za kuhakikisha kuwa kesi hizo zinashughulikiwa haraka na kutolewa
hukumu.
“Nimevutiwa sana na
utaratibu wa Mahkama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Jeshi la Polisi
kukutana kabla ya kesi kuanza ili kuangalia mazingira halisi ya kesi kwa
dhamira ya kufanikisha uendeshaji wa kesi mahkamani” alisema Dk. Shein.
Aidha Dk. Shein
alisifu jitihada zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na serikali na taasisi
zisizo za kiserikali za kuelimisha jamii kuhusu vita dhidi ya udhalilishaji
watoto na wanawake na kwamba matokeo ya jitihada hizo ni kuongezeka kwa utoaji
wa taarifa dhidi ya vitendo vya udhalilishaji katika vyombo husika.
Hata hivyo alisisitiza
kuwa “bado kuna kazi kubwa mbele yetu ya kuendelea kuelimishana juu ya kupiga
vita udhalilishaji watoto na wanawake ikiwa ni pamoja na kusisitiza malezi bora
ya asili kwa watoto wetu”
Katika maelezo yake
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mheshimiwa Omar Othman
Makungu alieleza kuwa ujenzi wa mahkama hiyo kunafanya idadi za mahkama za
watoto kufikia 3 ambapo moja ni ya Vuga katika mkoa wa Mjini Maghribi na Chake
Chake ambayo itakuwemo katika jengo la Mahkama mjini Chake Chake katika mkoa wa
Kusini Pemba.
Alisema ujenzi wa
mahkama hiyo ambao umefadhiliwa na Shiriki la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Watoto UNICEF kwa gharama ya shilingi milioni 77 pamoja na vifaa kwa makisio ya
awali unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2016.
Hata hivyo alibainisha
kuwa kufuatia gharama za ujenzi kupanda watahitaji fedha nyingine zaidi
shilingi milioni 30 kumalizia jengo na kuiomba serikali kuwapatia fedha hizo
pamoja na samani ili mahkama hiyo iweze kufanya kazi mara tu itakapomalizika.
Akizungumzia kuhusu
uendeshaji kesi Jaji Mkuu alisema changamoto nyingi walizokuwa wakipambana nazo
hivi sasa zimepungua kufuatia hatua mbali mbali zilizochukuliwa na idara yake
na washirika wengine.
Alizitaja hatua hizo
kuwa ni pamoja na ushirikiano na idara nyingine kumeharakisha uendeshaji wa
kesi, kuwepo kwa kituo cha urekebishaji wa tabia kwa watoto waliopatikana na
makosa (community Rehabilitation Centre), kuanza kutumika kwa kanuni za
uendeshaji wa sheria ya mahkama za watoto na kukamilika kwa utaratibu wa
kukusanya ushahidi.
Alizitaja hatua
nyingine kuwa ni kupatiwa mafunzo mahakimu wa mikoa juu ya uendeshaji wa kesi
za aina hii na kuwepo wakili kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria kusaidia watoto
wanaoshtakiwa mahkamani.
Jaji Mkuu aliishukuru
UNICEF kwa msaada wake huo pamoja na Kituo cha Masaada wa Sheria Zanzibar kwa
kuhudumia hafla hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa serikali na mashirika ya kimataifa wakiongozwa na Makamu wa Pili
wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.
0 comments:
Post a Comment