Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu Nchini kuacha kugugumizi katika
utoaji wa haki ili kuondoa au kupunguza zaidi muda mrefu unaochukuliwa katika
kutoa hukumu kwa kesi zinazopelekwa Mahakamani.
Amesema kigugumizi hicho mbali ya kulalamikiwa
kwa kipindi kirefu na Wananchi walio wengi lakini pia kinachangia
sana kuuondolea heshima yake Muhimili huo ukiwa miongoni mwa
Mihimili Mitatu ya Dola.
Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito huo wakati
akizungumza na Majaji, Wanasheria na Mahakimu ndani ya Jumla la Sheria Zanzibar
baada ya kuyaongoza Matembezi ya maadhimisho ya Siku ya sheria yaliyoanzia
Mahakama Kuu Vuga kupitia Benbella, Michenzani, Kituo cha Polisi madema na
kumalizikia katika Viwanja vya Michezo vya Maisara Mjini Zanzibar.
Amesema zipo kesi zinazolalamikiwa na Wananchi
walio wengi kama Dawa za kulevya na udhalilishaji wa Kijinsia unaowakumba zaidi
watoto wadogo na wanawake zinazopelekwa Mahakamani lakini hatma yake inaishia
hewani na wahusika kuwaona wakiendelea kutanua mitaani.
Balozi Seif ameeleza kwamba ushahidi wa wazi
katika baadhi ya kesi zinazopelekwa kwa Mahakimu hutolewa na wahusika lakini
kinachojitokeza kwa baadhi ya Majaji na Mahakimu kueleza kuwa ushahidi bado
haujakamilika.
Katika kukabiliana na vitendo hivyo Balozi
Seif amewakumbusha watendaji wa Mahakama kubeba jukumu lao kwa kuchukuwa hatua
za haraka za kutoa maamuzi ili kupunguza mrundikano wa majalada ya kesi
yaliyopo mezani kwao.
“ Majaji na Mahakimu wanapaswa kujiepusha na
malalamiko ya mrundikano wa mashauri yanayowahusu ambayo yamekuwa
yakilalamikiwa sana na Wananchi ”. Amesema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la mazoezi Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitahadharisha kwamba kitendo cha watumishi wa
Sheria kukaa maofisini kwa muda mrefu na baadae kuishia nyumbani bila ya
kufanya mazoezi ni hatari kwa afya zao.
Amesema ni vyema kwa watumishi hao kujipangia
utaratibu muwafaka wa kufanya mazoezi ya viungo hata kwa siku moja ndani ya
wiki ikiwezekana sio mbaya kuyafanyia nyumbani iwapo muda wa kufanya hivyo
umekuwa finyu.
Balozi Seif alieleza kwamba mazoezi ni afya
kubwa inayomsaidia Jaji, Mwanasheria na Hakimu kufikiri vyema katika
utekelezaji wa jukumu lake zito kwa Umma.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi katika falya
hiyo Jaji Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar Othman Makungu maadhimisho ya Wiki ya
Sheria Zanzibar yameamua kuingiza matembezi kwa mara ya kwanza katika
ratiba yake ili kutoa fursa kwa watendaji wa taasisi hiyo.
Jaji Mkuu Makungu alisema miili inahitaji
mazoezi na hata matembezi na ilionekana na Uongozi wa Mahakama Kuu kutokana na
watendaji waliowengi wanakaa muda mrefu maofisini jambo ambalo ni hatari kwa
afya zao.
Alisema changamoto hii ya ukosefu wa kufanya
mazoezi kwa baadhi ya watendaji wa Sekta ya Sheria itatoa ushawishi kwao kuanza
ukurasa mpya wa kuamua kujiingiza kwenye eneo hilo muhimu.
Baadhi ya Vikundi vya
mazoezi vikipasha mwili katika
Viwanja vya Maisara Suleiman baada ya
kukamilisha
matembezi ya siku ya Sheria Zanzibar.
|
0 comments:
Post a Comment