Kauli hiyo ilitolewa na baadhi ya wana Kamati na wananchi wa
shehia ya Muyuni “B” iliyo tofautiana wakati wakimueleza Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika Msitu huo kuangalia maeneo ya
Hifadhi ya Msitu ambayo baadhi ya wahusika hao wameamua kuyatumia kwa
kuendeleza kilimo.
Eneo hilo la ardhi lililokubalika kutumiwa kuwa hifadhi ya Msitu
na Wananchi wote wa Shehia Tatu za Muyuni A,B na C kwa takriban
miaka 10 limekuwa na mgogoro wa matumizi kwa miaka minane sasa tokea
kutolewa uamuzi wa kila shehia iunde Kamati yake ya Uhifadhi badala ya ile ya
pamoja ya shehia hizo.
Wana Kamati hao pamoja na wananchi ambao mpaka ziara hiyo
inamazliza wakihitilafiana walisema baadhi yao wamekuwa na malengo ya kuyatumia
maeneo hayo na baadae kuyauza kwa vile tayari yamekuwa rasilmali kubwa katika
masuala ya uwekezaji vitege uchumi vya sekta ya Utalii.
Walisema tabia ya baadhi ya wananchi wenzao ya kuanza kilimo cha
minazi na miti mengine ya matunda na biashara pamoja na kisingizio cha sababu
za kushutumiana kwa itikadi za kisiasa imechangia kuvuruga eneo kubwa la
hifadhi hiyo muhimu kwa hatma yao na vizazi vijavyo.
Akitoa nasaha zake kwa wana Kamati pamoja na Wananchi hao wa
Muyuni “ B “ Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushauri kuhusiana na mgogoro huo wa hifadhi ya
Msitu wa Muyuni hapo baadaye.
Balozi Seif alisema utaratibu maalum utaandaliwa katika
kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa kuhusisha Viongozi wa Taasisi
za Kilimo, Ardhi na Maingira ambapo wahusika hao watakuwa na uamuzi wa kuwaita
watu waliohusika na mgogoro huo katika kuwahoji na kutaka ufafanuzi.
Alisema nia ya Serikali Kuu ni kuona hifadhi ya Msitu wa Muyuni
inaendelea kubakia kwa maslahi ya Wananchi wa eneo hilo pamoja na Taifa zima
kwa vile eneo hilo tayari limeshatangazwa ndani ya Gazeti la Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi hao
kwamba Zanzibar ikiwa niongoni mwa baadhi ya Mataifa ya Bara la Afrika
imebahatika kuwa na rasilmani nzuri za maumbile lakini baadhi ya watu wamekuwa
na tabia mbaya ya kuharibu kwa makusudi rasilmali hizo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Mali asili
Zanzibar Dr. Bakar Ased alisema eneo hilo la hifadhi hivi sasa baadhi ya sehemu
linatumika kwa shughuli za kilimo kinyume na lengo lililokusudiwa kwa
makubaliano ya Wananchi wenyewe na idhini ya Serikali.
Dr. Ased aliwatanabahisha Wananchi hao kwamba licha ya eneo hilo
kulengwa kuwa hifadhi ya misitu lakini pia wataalamu wa mazingira na hali
ya hewa wamefanya utafiti na kutoa ripoti iliyoeleza kwamba Ukanda wa
Kusini ni eneo zima lenye Hewa safi.
Alisema kuvurugwa kwa hifadhi hiyo kwa shughuli
nyengine za kilimo kunaweza kukasababisha kuwa chanzo cha uchafuzi wa
hali ya mazingira na matokeo yake ni athari kwa viumbe hapo baadaye.
Kuna sehemu kubwa ya Eneo la hifadhi ya misitu la Muyuni ambayo
kwa sasa in atumika kwa shughuli za kilimo mchanganyiko kama miembe, Minazi,
Mivinje ,Migomba pamoja na mazao madogo madogo ya mizizi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
29/11/2015.
0 comments:
Post a Comment