November 30, 2015

Serikali imezungumzia tishio la Serikali ya Marekani la kusitisha misaada kwa Serikali ya Tanzania kutokana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kukamatwa kwa maofisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Ofisi ya Ikulu jana amesema masharti yaliyotolewa na Serikali ya Marekani yanatekelezeka na yatamalizwa kabla ya kikao cha Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) kukaa Desemba, mwaka huu.
Wiki iliyopita, Serikali ya Marekani iliitaka Serikali ya Tanzania kumaliza haraka mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, vinginevyo upo uwezekano wa kusitishwa msaada wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni 999.4), za awamu ya pili ya fedha za MCC la nchi hiyo.
Mambo ambayo Serikali ya Marekani iliitaka Tanzania kumaliza haraka ni suala mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar pamoja na kupata ufafanuzi wa watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana amesema suala hilo haliisumbui serikali na ni tatizo dogo  ambalo linatatuliwa.
Amesema serikali ina uhakika wa kumaliza masuala hayo kabla ya kikao hicho cha Bodi ya MCC kukaa yatakuwa yameshatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Amesema Bodi ya MCC ilikaa kikao chake cha kwanza Septemba, mwaka huu na inatarajia kukaa tena kikao chake Desemba, mwaka huu.
Balozi Sefue ameongeza kuwa suala la sheria ya makosa mtandaoni, kuna watu walikamatwa na watafikishwa mahakamani na mahakama yenyewe ndiyo itakayotoa hukumu na kama wana makosa watahukumiwa na kama hawatakutwa na makosa basi wataachiwa huru.
Kuhusu mgogoro wa Zanzibar, Balozi Sefue amesema kuna vikao vinavyoendelea vya kupata muafaka na mgogoro huo nao utamalizwa kwa haraka zaidi.

0 comments:

Post a Comment