STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
22 Aprili , 2014
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameipongeza Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Zanzibar kwa kuweza kufikia malengo yaliyowekwa ya kukusanya mapato katika
kipindi cha miezi tisa iliyopita kuanzia mwezi Julai 2013 hadi Machi 2014.
Bodi
ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 133.9
lakini imevuka lengo na kukusanya jumla ya shilingi bilioni 134.6 ambacho ni
sawa na asilimia 100.51 ya lengo.
Kwa
upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar ilipanga kukusanya jumla ya
shilingi milioni 127.6 na imeweza kukusanya jumla ya shilingi milioni 110.5
ambazo ni asilimi 90.
Akizungumza
katika kikao maalum cha kujadili utekelezaji wa mpango kazi na bajeti ya Wizara
ya Fedha kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2013 hadi Machi 2014, Dk.
Shein amesema kwa ujumla ameridhishwa na utendaji kazi wa Wizara hiyo na hasa
taasisi zinazokusanya mapato kwani amesema bila ya kukusanya kodi ipasavyo,
inakuwa vigumu kutekeleza majukumu ya serikali.
“Hatuwezi
kuendesha serikali bila ya kuwa na fedha, fedha haziwezi kupatikana bila ya
kuwa na mipango mizuri ya kuzikusanya, serikali zote duniani zinaendeshwa
kutokana na kukusanya kodi”, alisema Dk. Shein.
Aidha,
aliipongeza kamati ya ukomo ya bajeti kwa kuweza kuzigawa vizuri fedha
zinazokusanywa kwa ajili ya kufanyiwa matumizi kulingana na vipaumbele
vilivyowekwa na serikali.
“Naipongeza
pia “ceiling committee” kwa kazi nzuri iliyofanya katika kuzigawa fedha
zilizokusanywa kwa mujibu wa vipaumbele tulivyoviweka, tumekusanya vizuri na
tumezigawa vizuri na hivyo utekelezaji katika kipindi cha miezi tisa umekwenda
vizuri” aliongeza.
Rais
wa Zanzibar amesema hali ya ukusanyaji wa mapato Zanzibar imekuwa ikiendelea
kuleta matumaini hasa ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo alisema mwaka
2010/2011 ukusanyaji wa mapato ulikuwa kati ya shilingi bilioni 13 na 14 kwa
mwezi ikionesha tofauti kubwa na sasa ambapo makusanyo yanafikia wastani wa
shilingi bilioni 29 na 30 kwa mwezi.
Mapema
akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo, Katibu Mkuu wizara ya Fedha Ndugu Khamis
Mussa Omar amesema katika kipindi cha miezi tisa Julai 2013 hadi Machi 2014,
Wizara ya Fedha kama zilivyo taasisi nyengine za Serikali imeweza kukusanya
jumla ya shilingi 3,117 milioni sawa na asilimia 52.9 ya makadirio ya mwaka ya
shilingi 5,891 milioni.
Aidha,
amesema katika kipindi hicho hicho Idara ziliweza kutumia jumla ya shilingi
4,220.84 milioni kati ya shilingi 6,874.13 milioni zilizotengwa kwa kazi za
kawaida kwa mwaka 2013/2014 ambazo ni sawa na asilimia 61.4 ya makadirio ya
mwaka mzima.
Kwa
upande wa kazi za maendeleo jumla ya shilingi 1,147.06 milioni zilitumika
kwenye miradi mbali mbali ya maendeleo ikilinganishwa na shilingi 2,540.00
milioni zilizoombwa kwa robo tatu za mwaka ambazo ni sawa na asilimia 45.2 ya
maombi au asilimia 13.6 ya makadirio ya mwaka.
Malengo
ya msingi ambayo Wizara hiyo ilijiwekea katika kipindi cha miezi tisa iliyopita
ni pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kufikia kiwango cha
asilimia 20 ya pato la taifa, kwa kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato na
kuendeleza elimu kwa walipa kodi.
Vile
vile Wizara hiyo ilidhamiria kuendelea na udhibiti wa matumizi ya serikali na
kuhakikisha kuwa kunakuwepo na thamani halisi ya matumizi yanayofanywa “value
for money” katika utekelezaji wa shughuli na serikali pamoja na kuendelea
kulipa mishahara na mafao ya wastaafu kwawakati mambo ambayo yote
yametekekelezwa kama yalivyopangwa.
Wizara
ya Fedha ilieleza taarifa hiyo imeendelea kufanya uhakiki wa mali za serikali
sambamba na kuwaandalia wafanyakazi mazingira bora na hivyo kuweza kutoa huduma
bora za kiufundi na kiutawala zinazosimamiwa na idara mbalimbali za Wizara
hiyo.
Mkutano
huo ambao pia ulihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad
na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi ni mfululizo wa vikao vya Wizara
mbali mbali vinavyoafanyika Ikulu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein vinavyotathmini
utekelezaji wa mipangokazi na bajeti kwa kipindi cha miezi tisa Julai 2013 hadi
Machi 2014.
said ameir ikuluz anzibar
0 comments:
Post a Comment