Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba misingi ya ufundishaji wanafunzi Maskulini
itaendelea kukosekana iwapo idadi kubwa ya Wanafunzi itapindukia kiwango
kilichowekwa Kitaifa au Kimataifa.
Alisema
idadi ya kawaida ya wanafunzi ndani ya darasa moja inahitajika kuwa watoto
wasiozidi arubaini wakiwa na vikalio pamoja na vifaa vyote wanavyohitajika kuwa
navyo wanafunzi hao darasani.
Balozi
Seif alisema hayo mara baada ya kukabidhiwa na kuvizindua rasmi vyoo 18 vya
Skuli za Kijitoupele za Msingi A na B pamoja na ile ya Sekondari hafla
iliyofanyika katika Skuli hiyo na kuhudhuriwa na Wanafunzi, Walimu pamoja na
Wazazi wa Wanafunzi wa Skuli hizo.
Balozi
seif alisema msongamano wa watoto wengi Darasani mbali ya kwenda kinyume na
mfumo, taratibu na maadili ya ufundishaji ndani ya darasa lakini pia unabebesha
mzigo mkubwa walimu kuweza kuhudumia wanafunzi hao kwa wakati mmoja.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kamati ya Skuli
ya Kijitoupele kwa uamuzi wao wa kukubali Wanafunzi wao kuhamishwa kwenda
kupata taaluma skuli nyengine ili kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi
ndani ya Skuli hizo.
“
Walimu wetu wamekuwa wakiendelea kupata mzigo mkubwa kuwasomesha watoto wetu
kutokana na wingi wa idadi yao darasani. Inasikitisha sana kuona Darasa moja la
Skuli hii lina wastani wa wanafunzi 240 jambo ambalo pia ni hatari kwa afya ya
wanafunzi wenyewe “. Alifafanua Balozi Seif.
Alisema
katika kukabiliana na tatizo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi
kuangalia maeneo mengine ya wazi ndani ya Wilaya ya Magharibi ili kutoa fursa
ya ujenzi wa Skuli nyengine Mpya zitakazosaidia kukidhi mahitaji ya wanafunzi
wa maeneo hayo.
Balozi
Seif aliwasihi Wanafunzi hao kuendelea kuvitunza vyema vyoo hivyo ili vidumu
kwa muda mrefu pamoja na kuwakumbusha kupenda masomo yao kwa lengo la kushika
nafasi za Uongozi na Taaluma kwa Taifa hili hapo baadaye.
“
Nawajibu wa kuwapongeza Walimu na Kamati ya Wazazi wa Skuli hii kwa juhudi zao
za usimamizi mzuri wa wanafunzi wao na kupelekea kutoa wanafunzi wengi
wanaofaulu vizuri kuingia katika skuli mbali mbali za Michepuo hapa Nchini “.
Akisoma
Risala kwa niaba ya Wanafunzi, Walimu na Wazazi wa Skuli hizo Mwalimu Hidaya
Haji Mkema alilipongeza Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa {
UNICEF } kwa msaada wa vyoo hivyo ambavyo lilikuwa na uwezo wa kuvijenga Skuli
nyengine.
Mwalimu
Hidaya alisema Skuli za Kijitoupele bado zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa
wanafunzi changamoto ambayo iko katika hatua ya kutafutiwa ufumbuzi wake
ifikapo mwaka 2015.
Alisema
uandikishaji wa wanafunzi wapya katika skuli hizo za Kijitoupele A na B
umefikia idadi ya watoto 800 kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa kupindukia
mfumo na utaratibu uliowekwa wa sera ya Elimu.
Akitoa
salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto { UNICEF } Mwakilishi
wa Shirika hilo hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini alisema watoto wana haki
ya msingi ya kupata elimu inayoambatana na usafi wa mazingira.
Bibi
Francesca alisema utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na Serikali ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika
suala la huduma za usafi wa mazingira maskulini umethibitisha hasara ya zaidi
ya shilingi Bilioni 300 kwa mwaka.
Mwakilishi
huyo wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar alieleza
kwamba Taasisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar tayari wameshatengeneza muongozo wa ujenzi wa vyoo katika maskuli
mbali mbali unguja na Pemba.
Alisema
muongozo huo una lengo la kuwajengea mazingira rafiki wanafunzi na tayari
umeshazinufaisha skuli nane za Pemba naTano kwa Unguja wakati awamu ijayo
itahusisha skuli nyengine Sita hapa Zanzibar.
Naye
kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar { WEMA
} Bibi Mwanaid Saleh alisema mradi huo uliohusisha Skuli 13 Unguja na Pemba kwa
ufadhili wa Unicef umegharimu Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tatu na
Ishirini na Tano { 325,000,000/- }.
Katibu
Mkuu Mwanaidi alizitaja Skuli zilizofaidika na mradi huo kuwa ni pamoja na
Makombeni, Vitongoji, Wingwi,Kwale,Pujini, Mabatini na Konde kwa Pemba na Kijitoupele,
Nyerere Msingi,Tunguu, Bububu na Mtopepo kwa Unguja.
Akimkaribisha
Balozi Seif katika hafla hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh.
Ali Juma Shamhuna alisema Madarasa 40 yanahitajika kujengwa ndani ya Wilaya ya
Magharibi ili kukidhi mahitaji yaliyopo ndani ya Wilaya hiyo.
Waziri
Shamhuna alifafanua kwamba upo mradi maalum wa ujenzi wa Skuli kumi za
Sekondari katika Wilaya zote za Zanzibar mradi ambao utatoa upendeleo wa kwanza
kwa wilaya ya Magharibi ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi
katika Skuli za Wilaya hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza mwakilishi wa UNICEF hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini kwa uamuzi wa shirika lake kusaidia ufadhili wa ujenzi wa vyoo vya skuli ya Kijitoupele iliyopo Wilaya ya Magharibi. |
Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment