August 24, 2016

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA  UFUNGUZI WA KONGAMANO LA  TATU LA  DIASPORA-
ZANZIBAR BEACH RESORT- MBWENI ZANZIBAR
24 AGOSTI, 2016

Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dk. Salim Ahmed Salim; Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid; Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Omar Othman Makungu; Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Issa Haji Ussi (Gavu); Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dk. Augustine Mahiga (MB); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Mheshimiwa Said Hassan Said; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 
Ndugu Salim Said Baghressa,
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Waheshimiwa Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar,
Ndugu Wanadiaspora na Wageni Waalikwa,

Assalamu Aleikum,


Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaaliya uhai na uzima tukaweza kukutana hapa kwa ajili ya Kongamano hili la Tatu la  Watanzania wanaoishi nje ya nchi yetu yaani Wana “Diaspora” ambapo mara hii linafanyika hapa Zanzibar. Mtakumbuka kuwa Makongamano mawili ya awali, yalifanyika Tanzania Bara na  yote mlishiriki kwa wingi na  yalifana sana. Hongereni sana. Nakupongezi kwa kufanikisha makongamano hayo na kwa kushiruiki kwa wingi.
Natoa shukurani zangu kwa  uongozi wa Ofisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa  kuandaa  Kongamano hili na  kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi. Sote tunashuhudia kuwa Kongamano hili limefana sana, kwa sababu limeandaliwa vizuri. Nimeisoma ratiba na nimeiona kuwa nayo imeandaliwa kwa namna yake. Nimefurahi kuona kuwa katika ratiba yenu mtafanya safari ya  Sunset cruising’, ili kuona mandhari na mazingira ya mji Mkongwe wa Zanzibar katika nyakati za jioni pamoja na kuitembelea  miradi mbali mbali ya maendeleo. Kadhalika, mtapata fursa ya kuyaona mambo ya kale na ya sasa, fursa hii ya kuangalia mambo ya kale ni muhimu sana.  Mtaweza kuona jinsi mchanganyiko huo maalum unavyovutia. Mtayaona mambo yalivyo murua “Wahenga walisema, ukiona vinaelea vimeundwa”. Nawapongeza kwa dhati waandalizi wa Kongamano hili kwa ubunifu huo kwa ajili yenu - Hongereni sana.

Kadhalika, nachukua nafasi hii kutoa shukurani na pongezi kwenu  Wana “Diaspora” ambao ndio walengwa wa Kongamano hili, kwa kujitokeza kwa wingi sana. Ni dhahiri kwamba kuukubali mwaliko huu ni  ithibati ya mapenzi makubwa mlionayo kwa  nchi yenu ya asili, licha  ya kuwa baadhi yenu  hivi sasa mna uraia  wa mataifa mengine. Hata hivyo mmekubali mwaliko huu kwa kutambua ule usemi usemao,  ‘Mtu Kwao ndio ngao’; na ule usemi wa wazungu usemao “A people without the knowledge of their past history, origin and culture, is like a tree without roots.”  Tafsiri yake ni kuwa, watu wasioijua na kuithamini  historia yao, asili pamoja na utamaduni  wao ni mithili ya mti usiokuwa na mizizi.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Serikali  zetu zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinaandaa aina hii ya Makongamano haya kwa  kuwa zinatambua na kuthamini haki na wajibu wa Wana “Diaspora” wa  kushiriki katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo nakupongezeni. Ahsanteni kwa kujitokeza kwa wingi na karibuni nyumbani.  Kwa wale Wana “Diaspora” ambao hawajawahi kufika Zanzibar, nakukaribisheni Zanzibar kwa kusema karibuni nyumbani. Imani na ukarimu wa watu wa Zanzibar unathibitishwa kwa msemo maarufu uliosemwa na Marehemu bibi Siti bint Saad aliyekuwa Mwimbaji Maarufu wa Zanzibar na kuipatia sifa kubwa Zanzibar katika moja kati ya nyimbo zake.  Sehemu hio ya nyimbo yake imesema  Zanzibar ni njema atakaye aje’. Kipande hiki cha nyimbo alituelezea Mzee wetu, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hivyo, Karibuni sana.

Napenda mfahamu kwamba Makongamano haya ya Watanzania wanaoishi Nchi za Nje,  tunayoyafanya kila mwaka, hivi sasa tumeyapa umuhimu mkubwa. Nataka nikuthibitishiyeni kwamba Makongamano haya yatakuwa endelevu.  Kwa hivyo, nakushaurini kuwa  mnapopanga ratiba zenu za kuja Tanzania kwa mapumziko  kila mwaka, zingatieni tarehe za kufanyika Makongamano haya ili mpate fursa ya kushiriki.

Mtakumbuka kuwa nilibainisha dhamira yetu ya kuandaa Kongamano hili Zanzibar kwenye hotuba yangu ya kufunga Kongamano la mwaka jana iliyosomwa kwa niaba yangu na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Mheshimiwa Dk. Mwinyihaji Makame. Kadhalika dhamira hiyo niliielezea tena katika hotuba yangu niliyoitoa tarehe 5 Aprili, 2016 wakati nikilizindua Baraza la Tisa la Wawakilishi  la Zanzibar, kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni. Leo tunatekeleza dhamira na ahadi hiyo kama wahenga walivyosema ‘ahadi ni deni’ na ‘ahadi  ya muungwana ni neno lake’ na ‘ahadi zetu ndizo pingu zetu’.  

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Suala la kuwashirikisha Wana “Diaspora” katika kuimarisha maendeleo  ya nchi zao za asili limepewa umuhimu  mkubwa na mataifa mbali mbali pamoja Jumuiya za Kimataifa. Umoja wa Afrika kwa wakati mbali mbali umekuwa ukipitisha maazimio na kufanya mikutano mbali mbali inayohusu masuala ya “Diaspora”.

Takwimu zilizotolewa na  Umoja wa Taifa zimebainisha kuwa  idadi ya watu wanaoishi nje ya nchi zao imeongezeka zaidi ya mara tatu; kutoka idadi ya watu milioni 75 iliyokisiwa katika miaka ya sitini hadi watu milioni 232, katika mwaka 2013. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 3 tu ya idadi watu wote duniani.  Vile vile, taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2011 ilibainisha kuwa  kiasi cha watu milioni 30.6 wa Bara la Afrika wanaishi nje ya nchi zao za asili. Kwa upande wa hapa Tanzania,  kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Watanzania milioni moja wanaishi nje ya nchi wakiwa ni Wana “Diaspora”.

Makundi haya ya watu wanaoishi nje ya nchi zao za asili yamekuwa yakituma kiwango kikubwa cha fedha katika nchi wanazotoka.  Inakadariwa kuwa zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 40 zilitumwa na Wana “Diaspora” katika mwaka 2010.  Kiwango hicho kilikuwa kikubwa kuliko kiwango cha misaada rasmi ya maendeleo iliyotolewa katika mwaka huo kwa bara la Afrika. Nimeamua kutoa takwimu hizo kwa ufupi, ili muone umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti  ya kuimarisha mashirikiano na kuwashirikisha kikamilifu Wana “Diaspora” katika mipango ya maendeleo yetu.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Juhudi za kuwashajiisha na kuwashirikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali za awamu zilizopita katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Dhana ya “Diaspora” ilianza kupata  nguvu zaidi katika uongozi wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Uongozi wa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Ni vyema, tukaelezana kuwa,  mwamko huo wa Serikali ya Awamu ya Nne, ulikwenda sambamba na vuguvugu la kimataifa la kuwahamasisha Wana “Diaspora”, hasa baada ya tafiti nyingi zilizofanywa kuthibitishwa kuwa michango ya Wana “Diaspora” imeleta mabadiliko makubwa  ya kimaendeleo katika baadhi ya nchi zao za asili.

Vuguvugu hilo liliambatana na mikutano na makongamano ya kimataifa ya Wana “Diaspora” kama huu tunaofanya leo hii. Kwa  upande wa Afrika, juhudi maalum zilichukuliwa kuwahamasisha watu wenye asili ya Afrika kuitambua asili yao na kuungana na wananchi wenzao walioko Afrika katika kuinua maendeleo ya bara hili.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Wakati nilipokuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilipata fursa ya kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, katika Mkutano wa Pili wa Wasomi wa Afrika na Wana “Diaspora” wenye asili ya Afrika uliofanyika nchini Brazili, mwezi Julai 2006 kutokana na mualiko wa Rais De Lula wa Brazili wakati ule kwangu. Baadae,  nilimwakilisha tena Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete, kwenye mkutano wa kwanza wa Wana “Diaspora” wa Tanzania uliofanyika London mwezi wa April, 2008, ambao ulifanikiwa sana kwa kuwa uliishirikisha sekta ya umma na sekta binafsi. Kwa hakika mkutano ule ulileta hamasa kubwa kwa Watanzania waliohudhuria na kufikiria zaidi masuala ya maendeleo ya nchi yetu. Katika mkutano huo baadhi ya makampuni yaliyokuwepo Tanzania, yalieleza fursa za ajira muhimu kwa Watanzania wenye ujuzi na ambao wangependa kurejea nyumbani kushiriki katika kujenga nchi yetu. Ushiriki wenu katika mikutano kama hii ni kielelezo thabiti cha dhamira yenu katika kuitikia wito wa serikali na viongozi wa nchi yetu wa kuwataka muwe washirika katika kuijenga nchi yetu.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Kutokana na kutambua umuhimu wa Watanzania wanaoishi nchi za nje, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Awamu ya Nne iliunda Idara maalum kuyashughulikia masuala ya Watanzania wanaoishi Nchi za Nje (Diaspora), katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 2010 ili kuitekeleza kwa vitendo azma yetu ya kuwashirikisha Wana “Diaspora” katika kuiendeleza nchi yetu.

Kwa umuhimu huo huo wa kuyapa nguvu mambo ya “Diaspora”, nami mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mwaka 2010, nilianzisha, katika Serikali niliyoiunda, kitengo kinachoshughulikia mambo ya Wana “Diaspora”, ndani ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.  Nilikiweka kitengo hicho katika Ofisi yangu ili kuhakikisha kuwa kinatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kushirikiana na  Wizara ya Mambo ya Nchi za nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati ule. Tangu wakati huo, nimekuwa nikifuatilia kwa karibu zaidi utekelezaji wa kazi zake na ukuaji wa kitengo hicho ambacho hivi sasa nimekifanya kuwa  Idara kamili, inayoshughulikia mambo ya  Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari Wanaioshi Nchi za Nje. Kadhalika, katika kipindi chote tangu Idara hio ilipoanzishwa Wana “Diaspora” au vikundi vyao, ambavyo vimekuwa vikitembelea Zanzibar kushiriki katika shughuli za maendeleo na vile vinavyotoa huduma kwa jamii.  Baadhi yenu mtakumbuka hafla ya chakula cha mchana niliyoiandaa Jumamosi  ya tarehe  9 Agosti, 2014 kwa ajili ya Wana “Diaspora” katika viwanja vya Ikulu - Zanzibar. Hafla ile nayo ilifana sana na naamini kwamba nanyi  bado imo katika kumbukumbu zenu.

Kwa hivyo Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari Wanaioshi Nchi za Nje kwa upande wa Zanzibar ndiyo inayosimamia masuala ya “Diaspora” na nimekuwa nikiwaelekeza viongozi wake  kufanya ziara za kujifunza katika nchi zinazofanya vizuri katika kuwashirikisha Wana “Diaspora” katika mipango ya maendeleo. Nchi hizo ni pamoja na Ghana, Brazili, Ethiopia na India. Wito wangu kwenu Wana “Diaspora”, muitumie vizuri Idara hii kwani ipo kwa ajili yenu.

Natoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kumteua Mheshimiwa Dk. Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ambayo ina jukumu kubwa katika kusimamia na kushughulikia masuala yote yanahusu Wana “Diaspora”.  Mheshimiwa Balozi Augustine Mahiga ambaye ametumia kipindi kirefu cha utumishi wake serikalini akiwa nje ya nchi, amepata uzoefu mkubwa, hivyo anayafahamu kwa kina masuala muhimu yanayowagusa Wana “Diaspora”. Ninaamini kwamba ataiendeleza vizuri kazi iliyoanzishwa na viongozi wa Awamu zilizopita. Kwa upande wa Zanzibar, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, itaendelea kushirikiana na wahusika wote kwa lengo la kukuza na kuimarisha ustawi wa Wana “Diaspora”.

Vile vile, nachukua nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Ofisi za Kibalozi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  katika nchi mbali mbali kwa kufanya kazi kwa karibu na kwa kushirikiana na Wana “Diaspora” katika nchi na kanda ambazo ofisi hizo zimepewa jukumu la kuwatumikia. Vile vile, natoa shukurani kwenu Waheshimiwa Mabalozi kwa juhudi zenu za kushiriki katika makongamano haya ya “Diaspora” kila mwaka yanapofanyika. Nawahimiza Wana “Diaspora” kuzitumia vizuri Ofisi hizi za kibalozi  kwa kutafuta ushauri, kupata nasaha, na misaada mbali mbali kila mnapohisi inafaa kuleta hapa nyumbani. Hizo ni Ofisi zenu na  mjisikie mpo nyumbani wakati mnapozitembelea.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Nimefurahi kuona kwamba Taasisi nyingi za binafsi zimekubali kwa ushindani mkubwa kuudhamini  Mkutano huu, ili kupata fursa  ya kuonana na kuzungumza  nanyi Wana “Diaspora”  kwa karibu zaidi.  Napenda kutoa shukurani kwa wadhamini wote waliojitokeza kulidhamini kongamano na wale wote ambao waliotaka kushiriki lakini wakakosa fursa hiyo kwa sababu mbali mbali. Nakuhimizeni  Wana “Diaspora”  muyatembelee  mabanda ya maonesho  ya Taasisi mbali mbali zilizopo hapa pamoja na vituo vya wajasiriamali  ili mpate fursa ya kununua bidhaa mbali mbali walizotutayarishia.  Hongereni Wajasiriamali wetu.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Nafahamu kwamba, kama ilivyofanyika katika makongamano yaliyotangulia, mada  mbali mbali ambazo zimechaguliwa kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo na ustawi wa Wana “Diaspora” na  nchi yetu kwa jumla, zitawasilishwa hapa. Nasaha zangu kwenu ni kuwa fuatilieni kwa umakini mkubwa, ulizeni maswali, toeni duku duku lenu kwa utaratibu mzuri kwa kuzingatia maudhui na kanuni zinaongoza mikutano ya aina hii. Nawaahidi kwamba Serikali zetu zitayafanyia kazi mapendekezo na maazimio yatakayopitishwa katika Kongamano hili.  Natanguliza pongezi zangu za dhati kwa watoa mada na wasimamizi wote wa mijadala waliochaguliwa na kukubali kuja hapa kuifanya kazi hiyo.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kongamano hili limelenga katika kuwahamasisha na kuwashajiisha Wana “Diaspora” kushiriki katika kuendeleza sekta ya Utalii nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kukuza uwekezaji nchini mwetu. Kwa msingi huo kauli mbiu ya Kongamano hili imeamuliwa kuwa ni “Bridging Tanzania Tourism and Investment: A new Outlook”, yaani Kuiunganisha Sekta ya Utalii na ya Uwekezaji: Mtazamo Mpya.

Natoa pongezi kwa waandaaji wa Kongamano hili kwa umahiri na umakini wao katika kuchagua kauli mbiu za makongamano yetu. Kauli mbiu hii imekuja wakati mzuri ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungno wa Tanzania  na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeelekeza nguvu kubwa katika kuikuza  sekta ya utalii na sekta ya uwekezaji, ili ziwe na  mchango mkubwa katika kukuza ajira na  kuimarisha uchumi wetu. Kwa upande wa Zanzibar,  sekta ya utalii hivi sasa ndiyo sekta kiongozi na imekuwa ikichangia zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa  na asilimia 27 katika Pato la Taifa la Zanzibar. Dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuongeza idadi ya wageni wanaoitembelea Zanzibar hadi kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020, lakini kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa hivi sasa, utekelezaji wake unaashiria kulivuka lengo hilo ifikapo mwaka huo. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010 watalii 132,836 walitembelea Zanzibar na mwaka 2014 watalii 311,801 walitembelea Zanzibar, ikiwa ni ongezeko la asilimia 134. Kwa hivyo hatuko mbali katika kufikisha watalii hao 500,000.

Ndugu Wanadiaspora, Ndugu viongozi na Wananchi,
Katika sekta ya uwekezaji, Serikali zetu zote mbili zimekuwa zikipanga na kutekeleza mikakati mbali mbali ya kukuza uwekezaji kwa kuweka mazingira mazuri  yanayowavutia na kuwashajiisha wawekezaji wa  ndani na nje ya nchi, mkiwemo nyinyi Wana “Diaspora”. Serikali zimepanua fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii, biashara, viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi wa bahari kuu, ujenzi wa nyumba, na sekta nyengine mpya zinazoibuka katika uchumi wetu ikiwemo sekta mpya ya gesi na mafuta kwa hapa Zanzibar kwa miaka michache ijayo. Hizi ni fursa zilizopo hapa kwenu na tunataka mzielewe kwa kina, ili mje na mikakati imara ya kuzitumia kwa faida ya nchi yetu na kwa faida yenu. Muendelee kuwa na ujasiri,  na muwe tayari kuzichangamkia fursa hizi kama wanavyofanya Wana “Diaspora” wa baadhi ya nchi, ambao wameweza kuleta mabadiliko makubwa katika nchi zao, ikiwemo  Ghana, Brazil, Ethiopia na India.  Hapa Zanzibar maeneo ya Fumba na Micheweni yapo tayari kwa kuwekezwa na kazi za ujenzi zimeanza katika maeneo hayo Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Bwana Baghresa ambapo kazi tayari imeanza, katembeleeni Fumba.  Kwa hivyo, hapana shaka nanyi mtashiriki katika kuyatumia  vilivyo.

Fursa hizi zipo kwa wenye mitaji mikubwa na  wenye mitaji midogo midogo. Kwa kuwa hapa ni kwenu,  mnaweza kujipanga kwa kadri hali inavyoruhusu.  Msisubiri hadi muwe na fedha nyingi au mitaji mikubwa, jambo ambalo katika mtiririko wa maisha  ya sasa  ni gumu.  Kwa wale wenye kuwekeza kwenye biashara ndogo ndogo na  ujenzi wa nyumba, nakushaurini mtafute wasimamizi waaminifu na waadilifu ili kuepukana na udanganyifu ambao baadhi ya wakati hutokezea na kukuvunjeni moyo.   Jengeni utamaduni wa kuja nyumbani mara kwa mara kwa ajili ya kufuatilia mambo yenu na fursa zilizopo. Msipende kuagiza. Zingatieni ule usemi maarufu wa lugha yetu kuwa. “Kuagiza ni kufyekeza”

Katika utekelezaji wa dhamira ya kuunganisha  utalii na uwekezaji, Serikali zenu zimekuwa zikipanga mikakati imara ya kuendeleza miundombinu kwa kuzingatia ukweli kuwa miundombinu ndiyo daraja bora la kuziunganisha sekta zote za kiuchumi ikiwemo sekta muhimu ya utalii. Juhudi kubwa zinaendelea kufanywa  katika kuiendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara mbali mbali, viwanja vya ndege na bandari katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania.  Kwa upande wa Zanzibar hivi sasa tunakamilisha kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume, tumeanza kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Pemba na hivi karibuni tutaupanua na kujenga jengo jipya la abiria, tutaanza ujenzi wa bandari ya Mpigaduri ambayo itajengwa kwa awamu tatu.

Ndugu Wanadiaspora,  Ndugu viongozi na Wananchi,
Kadhalika, nakushaurini mzitumie fursa zilizopo za kitaalamu katika sekta mbali mbali. Nchi yetu inahitaji wataalamu katika nyanja nyingi hasa katika maeneo mapya ya kiuchumi yanayoibuka na yale yaliyopewa kipaumbele  na Serikali zetu hivi sasa. Tunahitaji wahandisi kwa ajili ya kuendeleza viwanda,  kuimarisha sekta ya mafuta na gesi na utekelezaji wa mipango miji. Najua nyote mnatamani kuona mabadiliko ya haraka ya ujenzi wa miji yetu ili iwe ya kisasa na  ifanane na miji mikubwa iliyo katika baadhi ya nchi mnazoishi, lakini lazima mfahamu kuwa nanyi mnawajibu na jukumu kubwa la kuleta mabadiliko hayo tunayokusudia ili na sisi tupendeze kama wenzetu. Vile vile,  tunahitaji madaktari kwa ajili ya kuendeleza hospitali zetu na wahadhiri katika vyuo vikuu ili kukuza sekta ya elimu ambayo ndio msingi  katika  kujenga sekta nyengine. Sina shaka kwamba fursa hizi mtazichangamkia fursa hizi na mtakuwa tayari kuja nyumbani kufanya kazi katika sekta hizo.

Ndugu Wanadispora,  Ndugu viongozi na Wananchi,
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali imo katika hatua za mwisho za kutayarisha Sera ya “Diaspora” ambayo tutaipitisha wakati wowote kuanzia sasa.  Sera hiyo, itakapokamilika, pamoja na mambo mengine,  itafafanua  na kuweka wazi  dira na dhamira zetu  katika utekelezaji wa masuala muhimu yanayokuhusuni nyinyi  Wana “Diaspora” na njia bora za kushirikiana katika kutekeleza masuala mbali mbali ya maendeleo.

Sera itaainisha fursa zilizopo katika sekta zote za kiuchumi, na kijamii nilizozieleza kabla.  Kadhalika, Sera itaelekeza njia bora za kutuma na kupokea fedha pamoja na kuiimarisha misaada ambayo mmekuwa mkiitoa kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Kadhalika, Sera hii itabainisha sheria na wahusika muhimu katika kuyashughulikia na kuyatekeleza  masuala ya “Diáspora”. Natoa wito kwenu nyote mje kuisoma vizuri Sera itakapokamilika na kwamba nimeshaagiza kwamba mara tu itakapomalizika iwekwe  katika  tovuti ya Ikulu ya Zanzibar, ili kila mmoja aweze kuisoma popote alipo na aweze kutumia na pale na pale ambapo tutahitajia kutunga sheria basi tutafanya hivyo.

Ndugu Wanadiaspora,  Ndugu viongozi na Wananchi,
Kwa niaba ya viongozi wenzangu, napenda  kutoa shukurani kwenu kwa mapokezi mazuri mnayotupa wakati  tunapozitembelea nchi mnazoishi. Natoa shukurani kwenu, vile vile, kwa jitihada mnazozifanya  za kuhudhuria mikutano ambayo huwa tunaiandaa makusudi kwa ajili yenu wakati tunapozitembelea nchi mnazoishi. Nasaha zangu kwenu ni kuwa muendeleze utamaduni na ukarimu huo.  Napenda mfahamu kwamba sisi tunathamini sana juhudi zenu na naahidi kwamba tunaendelea kukutana na nyinyi kila tutakapopata nafasi ya kufanya ziara katika nchi mnazoishi.

Kwa mara nyengine tena, nakunasihini sana muendelee kuwa mabalozi  wazuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi mnazoishi.  Endeleeni  kuwa mfano wa tabia njema ili muendeleze sifa ya ukarimu, urafiki na usalama ambayo nchi yetu na raia wake wamejijengea na inatambulika katika mataifa yote duniani.  Zielezeeni sifa nzuri za nchi yetu pamoja na watu wake. Endeleeni kuishi kwa kuzingatia misingi ya urafiki, na udugu huku mkiwa na mapenzi makubwa baina yenu pamoja na nchi yenu ya asili.  Imarisheni jumuiya zenu na zitumieni kama nyenzo muhimu katika kuzilinda na kuzifuatilia haki zenu pamoja na kuimarisha mshikamano na umoja mlionao miongoni mwenu. Endelezeni utamaduni wa kujiwekea malengo kwa kuzingatia hekima na usemi maarufu wa lugha yetu ya kuwa “mchumia juani  hulia kivulini”

Nakunasihini mzingatie suala la utii wa sheria za nchi na sehemu mnazoishi  jambo ambalo mnalifanya vizuri bila shuruti kama ni siri kubwa  ya mafanikio katika maisha ya binaadamu popote anapoishi. Endelezeni utamaduni wa kuja kutembea nyumbani kila baada ya muda, jambo ambalo ni muhimu na linaimarisha mapenzi baina yenu na ndugu, jamaa na wazazi wenu. Mkija nyumbani mnapata fursa nzuri ya kujikumbusha zaidi mila na desturi zetu pamoja na  kupima fursa zilizopo. Mkija nyumbani, fanyeni jitihada za kuja na watoto wenu ili nao wapate fursa za kuyaona mambo mbali mbali ili waweze kuyathamini mambo ya nchi yao ya asili.  Mnatambua fika kuwa vizazi vyenu ni watu muhimu katika mipango yetu ya kuendeleza dhana hii ya “Diaspora”. Kwa hivyo, ninaamini kwa jambo hili mtalitia mkazo na mtalipa umuhimu unaostahiki. Kumbukeni kwamba hivi sasa  baadhi ya nchi, ikiwemo India zinafaidika na michango mbali mbali inayotolewa na kizazi cha pili na cha tatu cha “Diaspora”; hasa katika suala zima la uhaulishaji wa taaluma na teknolojia pamoja na mitaji.  Endeleeni kuzifuatilia kwa karibu taarifa za nyumbani kwa kutumia vyombo vya habari vinavyoaminika.  Kwa mara nyengine tena, nakuhimizeni mzitumie vizuri Ofisi zetu za Kibalozi na kutafuta ushauri kwa mabalozi na maofisa wa balozi hizo kwa masuala mbali mbali.

Ndugu Wanadiaspora,  Ndugu Viongozi na  Wananchi,
Kabla ya sijamaliza hotuba yangu,  kwa mara nyengine tena natoa shukurani maalum kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuandaa Kongamano hili na kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi. Vile Vile, natoa shukurani zangu kwenu Wana “Diaspora” na wageni wote waalikwa kwa kujitokeza kwa wingi katika Mkutano huu. Nakutakieni usikilizaji na ushiriki mzuri katika programu zote zilizotayarishwa  kwa  ajili ya Kongamano hili muhimu na la kihisotria. Naamini kuwa mijadala ya Kongamano hili itafanyika kwa umakini mkubwa, utaalamu, uzoefu na nidhamu inayolingana na utamaduni wetu, kama ilivyokuwa katika makongamano yaliyopita.  Kongamano hili litazidi kuimarisha uhusiano wetu na kujenga daraja imara la uhusiano na ushirikiano miongoni mwetu na washirika wa maendeleo; kwa lengo la kuifanya nchi yetu kuwa imara zaidi kiuchumi na kijamii. Kwa wale wanaoendelea kuwepo hapa Tanzania kwa mapumziko baada ya Kongamano hili nawatakia mapumziko mema na wale wanaosafiri kurejea nchi mbali mbali mnazoishi, nakutakieni safari njema. Mategemeo yetu ni kuwa sote tutakuwa pamoja katika Kongamano la mwakani, na Inshaallah, Mwenyezi Mungu atayajaaliya yote hayo yawe. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aizidishie baraka na neema nchi yetu na  adumishie hali ya amani na utulivu tuliyonayo.

Baada   ya  kusema hayo, napenda kutamka kwamba Kongamano hili la Tatu la “Diaspora” limefunguliwa  rasmi.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment