April 24, 2016

Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni Zanzibar, wametakiwa kujenga tabia ya kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuepuka maradhi ya kipindupindu yanayoathiri maeneo mbali mbali nchini.
Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Mbunge wa jimbo la Kikwajuni, Muandisi Hamad Yussuf Masauni alipokuwa akifanya usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo Mjini hapa.
Alisema maeneo mengi ya jimbo hilo hasa katika Majumba ya Maendeleo ya Michenzani ni machafu sana  hali inayoweza kusababisha maradhi ya miripuko yakiwemo kipindupindu na kichocho.
Masauni ambaye pia ni Naibu Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, alieleza kuwa wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na kupelekea uharibifu wa miundombinu ya kusafirisha maji taka ikiwemo mitaro kuziba.
“ Nachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi wa kikwajuni kuwa suala la usafi wa mazingira halina itikadi za kisiasa ni lazima wananchi sote tuungane bila ya kujali tofauti za kisiasa.
Pia nakuombeni wananchi hasa mnaoishi katika majumba ya michenzani mbadilike kwa kujali mazingira yenu kwani mjue kuwa endapo eneo hili litapata maradhi ya mripuko kuna hatari ya wananchi wengi kupoteza maisha kwa maradhi ambayo tuna uwezo wa kuyazuia.”, alisema Masauni huku akisisitiza umuhimu wa kufanya usafi wa mara kwa mara katika maeneo hayo.
Alisema viongozi wa jimbo hilo kwa sasa wanapanga kuanzisha kikundi maalum cha vijana wa kufanya usafi katika maeneo ya jimbo hilo, ambapo kila kaya(nyumba) watakuwa wanachangia kiasi cha shilingi 200 kila siku ili fedha hizo ziweze kuwasaidia watu wanaofanya usafi huo.
 “Aibu kubwa kuona ndani ya jimbo la kikwajuni panaanza kupatikana wagonjwa wa maradhi ya kipindupindu kwani ni jimbo lenye sifa ya usafi na ukaribmu toka enzi na enzi tena lipo mjini, lazima tushirikiane kufanya usafi katika maeneo yetu.” Alisema Masauni.
Aidha aliishauri Manispaa ya Zanzibar kuanza mara moja utafti wa kubaini mifumo ya maji machafu na masafi inayoingiliana katika maeneo hayo ili kuifanyia matengenezo kwa haraka kabla hapajatokea maafa ya maradhi ya miripuko na kusababisha athari kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo hilo, Nassor Salum Ali(Jazeera) aliwapongeza wananchi wa jimbo hilo waliojitokeza kufanya usafi wa mazingira kwa lengo la kuweka maeneo yako katika hali ya usafi.
Jazeera alisema kwamba kinga ya maradhi ya mripuko hasa kipindupindu ni usafi wa mazingira hivyo kila mwananchi anatakiwa kutekeleza wajibu wake bila ya kulazishwa na mtu.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Zanzibar, Aboud Hassan Serenge alisema kila mwananchi ana jukumu la kufanya usafi wa mazingira katika maeneo anayoishi kwa lengo la kuweka mji wa Zanzibar katika hali ya usafi.

 Serenge alifafanua kwamba kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakichafua mazingira ya mji kwa makusudi huku wakidai kuwa Manispaa ipo na ndiyo yenye dhamana ya kufanya usafi jambo ambalo sio sahihi kwani kila mtu suala la usafi linamuhusu.




0 comments:

Post a Comment