UTANGULIZI
Tangu
mwezi wa Septemba mwaka jana, Mripuko wa Kipindupindu bado unaendelea kuvikumba
visiwa vya Unguja na Pemba. Hadi kufikia sasa jumla ya wagonjwa 2391
wameshalazwa katika vituo 17 vya matibabu vilivyokwisha funguliwa Unguja na
Pemba. Wagonjwa 1363 kati ya hao wamelazwa katika vituo 7 vya Unguja na
wagonjwa 1028 wamelazwa katika vituo 10 vya Pemba. Jumla ya vifo 23 vimeripotiwa katika kipindi
hicho, 19 vilitokea Unguja na 10 vilitokea Pemba.
Vituo
vya matibabu vilivyofunguliwa kwa Unguja ni Chumbuni, Uzi, Muungoni, Uroa,
Ukongoroni, Fujoni na Gamba; na kwa upande wa Pemba ni Wete, Kojani, Mjinikiuyu,
Micheweni, Makangale, Maziwang’ombe, Kiuyumbuyuni, Chakechake, Mkoani, na
Vitongoji. Kambi mbili za Chumbuni na Gamba ndizo zinazoendelea kupokea
wagonjwa kwa sasa na 15 zilizobaki zimeshafungwa baada ya kutokua na wagonjwa,
zikiwemo kambi zote 10 za Pemba na 5 za Unguja
IDADI YA WAGONJWA KWA WIKI
Wastani
wa wagonjwa 10 hadi 25 walikua wakipokelewa kwa siku na 80 hadi 120 kwa wiki
katika wiki mbili (2) zilizopita. Hata hivyo idadi hii imeonekana kupungua
kidogo katika wiki hii iliyoishia Jumatatu ya tarehe 4/4/2016 ambapo wastani wagonjwa
sita (6) hadi 12 wamekua wakipokewa kwa siku na 73 walipokelwa kwa wiki. Kitakwimu,
upungufu huu bado hautoi dalili ya kupungua kwa mripuko kwani kuna kila dalili
za kuendelea kwa kasi kwa maambukizo katika maeneo mbalimbali.
Kati
ya wagonjwa 73 waliolazwa wiki hii wagonjwa 62 walilazwa chumbuni, wanene (8)
kituo cha Gamba na watatu (3) Kituo cha Fujoni, ambapo 42 kati yao walikua wanaume
na 31 wanawake. Asilimia 15 kati ya wagonjwa wote walikua watoto chini ya miaka
mitano (5)
Wilaya
za Maghribi A na B Unguja ndizo zilizoongoza kwa kutoa wagonjwa wengi zaidi
katika wiki 2 za hivi karibuni. Asilimia 62 ya wagonjwa wote walitokea wilaya
za Maghribi A na B hasa maeneo ya Mtoni, Mtoni kidatu, Mtopepo, Fuoni na Mwera;
ikifuatiwa na wilaya ya Mjini asilimia 29 hasa maeneo ya Malindi, Jangombe,
Makadara Amani na Kidongechekundu; Wilaya ya Kaskazini A asilimia 12 kutoka
maeneo ya Mkokotoni, Pwanimchangani, Kandwi, Matemwe na Kidoti Mvuleni; wilaya
ya Kaskazini B asilimia 4 kutoka maeneo ya Bumbwini misufini, Mahonda na
Fujoni; na wilaya ya Kati asilimia 2 kutoka maeneo ya Mwera, Kidimni na Koani.
Wilaya ya Kusini haikutoa wagonjwa katika kipindi hicho mbali na wagonjwa
watatu (3) wa kuharisha kutoka uzi na Kitogani ambao hawakuthibitishwa kuwa na
Kipindupindu.
Mbali
na mvua ndogondogo zinazoendelea katika kipindi hiki, sababu kuu zilizopelekea
ongezeko hili la wagonjwa ni wananchi kutokufata maelekezo yanayotolewa na
wataalam wa Afya juu ya kujikinga na Maradhi ya Kipindupindu. Wananchi wengi
bado wanaendelea na tabia hatarishi zinazopelekea maradhi ya kuharisha ikiwemo kutokuchemsha
maji ya kunywa, kutonawa mikono kwa maji na sabuni wakati wa kula na kutoka
chooni, kutokutumia vyoo ipasavyo, kutupa ovyo kinyesi na penpa pamoja na kuongezeka
uchafu katika mazingira tunayoishi na wafanyabiashara wa chakula kutokufuata
masharti ya usafi na usalama wa chakula katika biashara zao.
WITO
KWA WANANCHI
Kipindupindu ni ugonjwa unaoweza
kuepukwa kirahisi iwapo kila mtu atazingatia masharti ya kiafya yanayotolewa
kila siku na wataalam wetu wa Afya. Kila mmoja kati yetu ana jukumu katika
kupambana na maradhi haya yanayoendelea kuathiri afya na maisha yetu kila siku.
Taasisi zote za kiserikali za kiraia zikiwemo kamati za shehia, vikundi vya
kijamii na mashirika mbalimbali zinatakiwa kutoa mchaongo wao wa hali na mali katika
jitihada za kupambana na maradhi haya.
Kipindupindu kinaweza kuepukwa iwapo
tu kila mmoja wetu atazingatia masharti ya kiafya katika kuhifadhi mazingira na
usalama wa chakula na maji kwa kufanya yafuatayo:
1. Kunywa maji safi na salama kwa
kuyachemsha au kutia dawa.
2. Kuwa waangalifu na vyakula
unavyokula: Ni vyema kula vyakula vyenye uvuguvugu, matunda na mboga za majani
zioshwe vizuri kwa maji ya mtiririko.
3. Kutumia choo wakati wa kujisaidia
muda wote
4. Kuhifadhi kinyesi kwa usalama
ikiwemo kinyesi cha watoto, penpas na kadhalika na kuweka choo na msalani safi
muda wote.
5. Kuosha mikono kwa maji yenye
kutiririka na sabuni baada ya kutoka msalani, baada ya kumsafisha mtoto
aliyejisaidia, kabla ya kumlisha na kumnyonyesha mtoto, kabla ya kutayarisha,
kabla ya kupika na wakati wa kula.
6. Kwa mgonjwa anaeharisha na kutapika
anatakiwa kupelekwa haraka kituoni huku akipewa maji kwa wingi ili kurejesha
maji yaliyopotea.
7. Kuweka mazingira yetu safi kila
wakati ikiwemo kusafisha majaa, kutochafua mito na mitari ya maji,
KUMBUKA: KIPINDUPINDU
KINAZUILIKA, CHUKUA TAHADHARI ILI KUJIKINGA WEWE, FAMILIA NA JAMII
INAYOKUZUNGUKA, KWANI KINGA NI BORA NA RAHISI KULIKO TIBA.
0 comments:
Post a Comment