March 23, 2016

Waziri wa mambo ya ndani Tanzania  Charles Kitwanga amesema doria za ulinzi  zitaendelea Zanzibar hadi hali ya usalama itakapozidi kuimarika.
Amesema lazima shughuli hizo ziendelee ili wananchi waweze kuishi bila ya wasiwasi na kuwataka kujiepusha na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani kwani watachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya jeshi la polisi Zanzibar  Kitwanga amefahamisha  kuwa vikosi vyote vipo katika hali ya tahadhari katika kambi zao kwa ajili ya hali hiyo.
Akizungumzia kuhusu watu 31 waliokamatwa kwa matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyotokea mapema mwezi huu amesema baadhi yao wameachiwa na wengine wamefikishwa mahakamani.
Amewasifu wazanzibar kwa kudumisha amani katika kipindi chote cha kabla na baada ya uchaguzi tofauti na baadhi ya taarifa zinavyosambazwa nje ya visiwa vyao.

Kuhusu ulinzi siku sherehe za kuapishwa rais wa zanzibar hapo kesho amesema ulinzi upo imara na kuwaomba wananchi kusherehekea siku hiyo kwa amani bila ya ghasia ili wasikumbwe na mkono wa sheria.

0 comments:

Post a Comment