Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mbunge wa Ubungo (CHADEMA) Saeed Kubenea
kifungo cha nje cha miezi mitatu kutokana kosa la kutumia lugha ya matusi dhidi
ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ambaye sasa ni Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam.
Akisoma
hukumu hiyo leo Jijini Dar es Salaam Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Thomas
Simba amesema kuwa mahakama imeamua kumpa mshitakiwa adhabu ya kifungo hicho
kwa kuwa ndilo kosa lake la kwanza, hivyo Mshatakiwa anastahili kupata adhabu
ya huruma.
Chini
ya adhabu hiyo iliyotolewa chini ya kifungu no 89 kifungo kidogo cha kwanza Mhe. Kubenea hatakiwi kufanya kosa la aina yoyote ambalo
litamsababisha arudishwe tena mahakamani na endapo itatokea akafanya hivyo
mahakama itampa adhabu ya kifungo cha kwenda jela.
Awali
kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo mshtakiwa Said Kubenea mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba alipewa nafasi ya kujitetea ni kwanini asipewe
adhabu kali kwa kosa alilolitenda ambapo alieleza Mahakama hiyo kuwa hakuwa na
nia mbaya ya kwenda kufanya fujo eneo la tukio ambapo kulikuwa na mgomo wa
wafanyakazi wa kiwanda cha nguo cha TOOKU cha jijini Dar es salaam bali alikwenda
kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgomo huo akiwa kama mwakilishi wa wananchi wa
jimbo la Ubungo.
Ikumbukwe
kuwa Jalada la kesi hiyo na 320 ya mwaka lilifunguliwa na Jamhuri dhidi ya Said
Kubenea kwa kosa la kutumia lugha ya matusi kwa aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda, Aidha upande wa washtakiwa wameonyesha kutoridhishwa na
hukumu hiyo na wameomba kukata rufaa.
0 comments:
Post a Comment