STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
12.4.2016
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Issa Haji Ussi Gavu ameeleza haja kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo
kuendeleza mashirikiano ya pamoja katika utendaji wao wa kazi ili kufikia lengo
la Serikali la kuwatumikia na kuwahudumia wananchi wote.
Hayo aliyasema
mara baada ya makabidhiano ya Ofisi hiyo yaliofanyika kati yake na aliyekuwa
Waziri wa Ofisi hiyo Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, hafla iliofanyika
katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi iliopo Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na baadhi ya
viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Aidha Mhe. Gavu
alieleza kuwa mashirikiano ya pamoja yatafikia lengo katika kumsaidia
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein la
kuwaletea maendeleo wananchi wote.
Waziri huyo
alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein kwa kumteua kushika wadhifa huo na kuahidi
kwa mashirikiano ya pamoja na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo
lengo la Rais la kuiletea maendeleo Zanzibar litafikiwa.
Mhe. Gavu
alieleza kuwa hakuna kubwa litakaloshinda iwapo kutakuwa na mashirikiano ya
pamoja katika kutekeleza majukumu na wajibu sambamba na kufuata taratibu na
sherika kwa kila mfanyakazi.
“Nimekuja hapa
kwa ajili ya kufanya kazi hivyo sote tujiandae kwa kufanya kazi na kuendeleza
mashirikiano yetu ili tumsaidia Mhe. Rais...” alisema Waziri Gavu.
Katika maelezo
yake, Waziri Gavu alisisitiza haja wka wafanyakizi na viongozi wa Wizara hiyo
kuwepo kwa mashirikiano na kuahidi kwa upande wake atatoa mashirikiano makubwa
na kufanya kazi kwa kuelekezana na kushirikiana huku akiahidi kufanya kazi kwa
taratibu na sheria za nchi zilizopo.
Waziri Gavu
alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Dk. Mwinyihaji Makame kwa kuendelea
kuwa na mashirikiano nae na kuahidi kuendelea kuchota mawazo na busara sambamba
na hekima kutoka kwake.
Mapewa Mhe. Dk.
Mwinyihaji Makame alitoa pongezi kwa Waziri Gavu kwa kuteuliwa kuwa Waziri
katika Wizara hiyo na kueleza kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na utendaji wake
wa kazi mzuri alioufanya katika Wizara yake ya zamani na imani yake ni kuwa
katika wadhifa wake huo mpya atazidisha juhudi.
Dk. Mwinyihaji
ambaye pia, ni Mwakilishi wa Jimbo la Dimani aliwataka wafanyakazi na viongozi
wa Wizara hiyo kumpa mashirikiano makubwa Waziri huyo mpya kama walivyompa yeye
wakati akiwa Waziri katika Wizara hiyo ambapo katika uongozi wake ilikuwa ni
Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora.
Aidha, Dk.
Mwinyi alisisitiza haja kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa juhudi
kubwa kama wanavyosisitiza viongozi wakuu hapa nchini akiwemo Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dk. Johm Pombe Magufuli pamoja na Dk. Shein ili kuendelea
kuiletea maendeleo Zanzibar.
Dk. Mwinyi
alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi
mkuu uliopita na kutoa pongezi za pekee kwa Ofisi ya Faragha ya Mhe. Rais kwa
mashirikiano waliyompa huku akimuomba Waziri huyo mpya kuwatumia wafanyakazi wa
Ofisi hiyo katika utendaji wake wa kazi.
Akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara hiyo, Katibu wa Rais Haroub Shaib
Mussa alitoa pongezi kwa viongozi hao wote katika utendaji wao wa kazi sambamba
na kuwa karibu na wafanyakazi pamoja na wananchi wa Majimbo yao.
Katibu Shaibu
alimuahidi Waziri Gavu kuwa wafanyakazi wa Wizara hiyo wataendelea kumpa
mashirikiano makubwa na kuendelea kumuunga mkono katika utendaji wake wa kazi
kwa lengo moja la kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendneleo endelevu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
0 comments:
Post a Comment