Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Viongozi na Watendaji
wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel wanapaswa kuongeza kasi ya utendaji ili
waendelee kuwa watoa huduma bora hapa Nchini licha ya kasoro ndogo ndogo
zinazoweza kurekebishwa kwa wakati muwafaka.
Alisema
Zantel kwa kipindi cha miaka Minane mfululizo imekuwa ikitunukiwa zawadi ya
mlipa kodi bora katika kundi la walipa kodi wakubwa, zawadi ambayo
hutolewa kila mwaka na Mamlaka ya Kodi Tanzania { TRA }.
Balozi
Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma mpya ya
mtandao wenye kasi zaidi wa G Nne { 4G } kwa upande wa Zanzibar iliyofanyika
katika Bustani ya Mnara wa Kumbu kumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar
hapo Michenzani Mjini Zanzibar.
Alisema
ushindi huo ni fahari kubwa kwa Zantel pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar yenye hisa zake ambayo ilipata changamoto kubwa na hatimae kufanikiwa
kupata kibali cha kuanzishwa kwa Kampuni hiyo mwaka 1999.
Balozi
Seif alieleza kwamba kodi zinazolipwa na Zantel zilizofikia zaidi ya shilingi
Bilioni 18 kwa mwaka 2015 pekee zinasaidia Taifa katika kuweka urari wa nakisi
ya Bajeti yake.
“
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawakilishwa katika Bodi ya Wakurugenzi ya
Zantel, ambacho ni chombo kikuu cha Kampuni cha kuweka mikakati ya Sera. Tunao
Wawakilishi Wawili katika Bodi ya Zantel tokea kuasisiwa kwake mwaka 1999 ”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Kituo cha huduma kwa wateja pekee tayari kimeshatoa ajira kwa Vijana wasiopungua Mia Mbili.
Hata
hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba yapo matatizo yanayolalamikiwa na
Wananchi kuhusu kukatika kwa mawasiliano kwa baadhi ya wakati jambo ambalo
huleta usumbufu unaochangia baadhi ya wanandoa kutoaminiana.
Alisema
ni vyema tatizo hilo likazingatiwa hasa kipindi hichi ambacho Kampuni hiyo kwa
hapa Zanzibar tayari imeshaingia katika matumizi ya mtandao unaokwenda kwa kasi
wa 4G.Mapema Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umekusudia kuimarisha zaidi huduma zake ili kuhakikisha unapatikana mtandao wa kasi utakaorahisisha ukuaji wa teknolojia hapa Zanzibar.
Bwana
Benoit alisema tokea Kampuni ya Millicon iliponunua asilimia 85 ya hisa za
Kampuni hiyo kutoka Kampuni ya Etisalat, Zantel imejikita katika safari mpya ya
uwekezaji mkubwa katika kupanua na kuboresha mtandao na huduma kwa watumiaji wa
mtandao huo.
Alisema
matumizi ya teknolojia hiyo mpya ya mtandao wenye kasi zaidi wa G Nne {4G} utasaidia
watumiaji kupata huduma zenye ubora na uhakika pamoja na kuwepo kwa
ongezeko la kasi la matumizi ya mtandao kama vile huduma za skype, You Tube na
mitandao mengine ya Kijamii.
“
Kampuni ya simu ya Zantel mara zote imekuwa ya kwanza kuleta ubunifu mpya kwa
Wananchi wa Zanzibar, na kwa uzinduzi wa huduma hii ya 4G inadhihirisha dhamira
yake ya kuendelea kutoa huduma bora na za kipekee kwa wakaazi wa Zanzibar ”.
Alisema Bwana Benoit Janin.
Meneja
Mkuu huyo wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel alieleza kwamba sambamba na
uzinduzi wa huduma ya G4 Zantel imefanikiwa kupanua wigo wa mtanado wake kwa
upande wa Tanzania Bara na kuwapa fursa wateja wake wa Zanzibar kutumia huduma
hiyo katika mkoa wowote wa Bara.
Alisema
upanuzi huo utaendelezwa zaidi kwa lengo la kuwafaidisha hata wananchi wa
vijiji vya mbali ili wafaidike na kufurahia huduma za teknolojia hiyo
inayokwenda kwa kasi Duniani.
Alifahamisha
kwamba Mteja anayejiunga na Mtandao wa 4G kupitia hata simu yake ya mkononi
unamuwezesha kupokea au kupeleka taarifa kwa kasi zaidi, kuunganishwa na
mtandao wa Internet, wanaowasiliana kuonana { Video call au skype }, kuona
michezo ya sinema na Video pamoja na huduma ya TV.
Uzinduzi
huo wa Mtandao wa 4G ulishuhudiwa pia na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Aman Karume watendaji wa Wizara hiyo pamoja
na Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo.
Msanii
wa Bongo Flavour Banabas aliimba wimbo maalum wa uzinduzi huo ambapo wateja
pamoja na baadhi ya watu walioshuhudia hafla hiyo walipata muda wa kujimwaga
kwenye ukumbi maalum ndani ya Banda lililojengwa kwa shughuli hiyo.
0 comments:
Post a Comment