STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
14.4.2016
JAMHURI
ya Korea Kusini imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
miradi mbali mbali ya maendeleo kwa kutambua juhudi kubwa zinazochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi
wake.
Akizungumza
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
Makamo wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea ya Kusini (KOICA), Bwana Kwon
Taemyon aliyasema hayo leo huko Ikulu Mjini Zanzibar akiwa ameambatana na
ujumbe wake kutoka Shirika hilo.
Katika
mazungumzo hayo viongozi hao walitumia fursa hiyo kuzungumza na kutilia mkazo
juu ya ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Korea ya Kusini na Tanzania
ikiwemo Zanzibar na viongozi wote hao kwa pamoja waliahidi kuuimarisha uhusiano
na ushirikiano huo.
Bwana
Taemyon alimueleza Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Korea inathamini uhusiano na
ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na itaendelea kuiunga mkono katika
kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya kilimo, ufugaji,
uvuvi, mifugo pamoja na sekta nyenginezo iliyopo sambamba na kuanzisha miradi
mengine mipya hapa Zanzibar.
Makamo
huyo wa Rais wa Shirika hilo la Maendeleo la (KOICA), alisema kuwa miongoni mwa
nchi katika bara la Afrika ambazo nchi hiyo imeziwekea kipaumbele katika
kuimarisha miradi ya maendeleo na kuanzisha miradi mengine mipya ni Tanzania
ambapo na Zanzibar nayo itafaidika kwa kiasi kikubwa katika kipaumbele hicho.
Aidha,
katika mazungumzo hayo Makamu huyo wa Rais wa (KOICA) alimueleza Dk. Shein azma
ya Shirika hilo la kusaidia mradi mkubwa wa ufugaji wa samaki ambao utawasaidia
kwa kiasi kikubwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu pamoja na kusaidia
nyenzo nyengine muhimu za ufugaji huo hatua ambayo itaongeza soko la
ajira sambamba na kipato kwa wananchi na Taifa kwa jumla.
Kiongozi
huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Serikali ya nchi yake pamoja na wananchi wa
nchi hiyo wako Tayari kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na watu wake.
Nae
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa
upande wake alitoa shukurani na pongezi kwa Serikali ya Korea ya Kusini kwa
mashirikiano makubwa sambamba na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha miradi yake mbali mbali ya maendeleo.
Dk.
Shein alisema kuwa pande mbili hizo zina historia kubwa katika mashirikiano na
uhusiano wake hatua ambayo imeweza kusaidia na kuimarisha sekta mbali mbali za
maendeleo ikiwemo kilimo, ufugaji wa wanyama, uvuvi, mazingira na ufugaji wa
samaki, elimu pamoja na sekta nyenginezo.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein aliipongeza Jamhuri ya Korea kwa kusaida miradi kadhaa
ukiwemo mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji maji na kuimarisha eneo la hekta
2,105 za miundombinu ya umwagiliaji maji katika mabonde ya Cheju, Kilombero na
Chaani kwa Unguja na Mlemele na Makwararani kwa Pemba, hatua
itakayosaidia katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi hapa nchini.
Aidha,
Dk. Shein alieleza juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza
katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji ambacho mafanikio yake yatasaidia
kwa kiasi kikubwa katika kuharakisha ukuaji uchumi wa Zanzibar.
Katika
mazungumzo hayo, Dk. Shein hakuchelea kumueleza Makamo huyo wa Rais wa (KOICA)
azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uvuvi wa bahari kuu
ambapo juhudi maalum zimekuwa zikichukuliwa katika kutafuta wawekezaji na
tayari wapo walioonesha nia ya kuekeza huku akipongeza azma ya (KOICA) ya
kuanzisha mradi mkubwa wa ufugaji samaki hapa Zanzibar.
Sambamba
na hilo Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo azma ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ya kuaanzisha viwanda vya uvuvi hatua ambayo itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuinua kipato cha wananchi pamoja na kukuza pato la taifa.
Dk.
Shein alilipongeza Shirika hilo katika juhudi zake za kuunga mkono kilimo
hicho cha umwagiliaji maji hapa Zanzibar ambapo lengo kubwa la Serikali ni
kuhakikisha kiwango cha uagiziaji wa mchele kutoka nje ya nchi kinapungua kwa
kuzalisha nusu ya mchele unaoagiziwa kutoka nje kuazia mwaka 2018 hadi 2019.
Ujumbe
huo wa Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA) uliofika
Ikulu kufanya mazungumzo na Rais pia, uliongozana na Waziri wa Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid Mohammed pamoja na viongozi wa
Wizara hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
0 comments:
Post a Comment