Mwakilishi
wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzaia Dkt. Rufaro Chatora amezishauri
taasisi za Serikali, taasisi za kiraia na watu
binafsi kila mmoja kutekeleza wajibu wake katika kukabiliana na maradhi
ya kipindupindu nchini.
Amesema
maradhi ya kipindupindu yanapotokea katika nchi moja yanagusa nchi nyingi
duniani kutokana na watu kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyengine katika
harakati zao za maisha.
Dkt.
Chatora ameeleza hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano na watendaji wakuu
wa Wizara ya Afya na waandishi wa Habari katika ziara yake ya kuangalia hali ya
maradhi ya kipindupindu Zanzibar tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka jana
hadi hivi sasa ambapo watu 2703 wamepata
ugonjwa huo.
Amesema
maradhi ya kipindupindu ni rahisi kutibika iwapo kila mtu atatimiza wajibu wake
na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia maji yasiyo salama ambayo ni moja ya
chanzo kikubwa cha kupata maradhi hayo.
Mwakilishi
huyo wa WHO amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya
Kimataifa litaendelea kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maradhi hayo ili
kuhakikisha yanamalizika.
Akieleza
hali ya kipindupindu ilivyo hivi sasa Zanzibar katika mkutano huo uliofanyika
Wizara ya Afya Mnazimmoja, Mkurugenzi Kinga na ELimu ya Afya Dkt. Mohd Dahoma
amesema hali bado sio nzuri na wanaendelea kupokea wagonjwa wengi katika kambi
ya Chumbuni.
“Tunapokea wagonjwa kati ya 10 hadi 15 kwa siku katika kambi ya Chumbuni,
kwa bahati mbaya jana tulipokea wagonjwa 20
na kambi moja mpya imefunguliwa
katika kisiwa cha Tumbatu,’’ alisema Dkt. Dahoma.
Amesema
jumla ya Kambi 17 za wagonjwa wa kipindupindu zimefunguliwa katika maeneo mbali
mbali ya Unguja na Pemba na kumi kati yao zimefungwa baada ya kukosa mgonjwa wa
maradhi hayo.
Ameongeza
kuwa kati ya wagonjwa 2703 waliogunduliwa na maradhi hayo 34 wamefariki ikiwa
ni sawa na asilimia 1.3 na vijana wenye
umri kuanzia miaka 17 ndio walioathirika zaidi.
Dkt.
Dahoma amesema kisiwa cha Unguja kimekuwa na wagonjwa wengi zaidi wa kipindupindu asilimia 52.3 na Pemba ni asilimia 47.3 huku
Mkoa Mjini Magharibi ukiongoza ukifuatiwa na Mkoa Kaskazini Pemba.
Mkurugenzi
Kinga na Elimu ya Afya amewashauri wananchi kuwawahisha mapema vituo vya afya watu wanaobainika na dalili za maradhi ya kipindupindu kwa vile
imeonekana wagonjwa wengi wanapopelekwa vituoni afya zao zinakuwa mbaya na
matibabu yanakuwa magumu.
MAELEZO Zanzibar
0 comments:
Post a Comment