TAARIFA YA SIKU 100 ZA KWANZA ZA SERIKALI YA
AWAMU YA TANO ILIYOTOLEWA NA
BALOZI OMBENI Y. SEFUE, KATIBU MKUU KIONGOZI,
IKULU, TAREHE 12 FEBRUARI, 2016
__________________________
Utangulizi
Serikali ya awamu ya Tano imetimiza siku
100 tangu iingie madarakani tarehe 5 Novemba, 2015. Japo siku 100 ni chache
sana kufanya tathmini ya kina, zinatosha kuonesha muelekeo wa serikali na
kupata kionjo cha uthabiti wa dhamira yake ya kutekeleza ahadi zake kwa
wananchi.
Kumekuwa na shauku kubwa ya wananchi kujua
kilichofanywa na Serikali hii katika siku zake 100 za mwanzo. Ni shauku ya haki
ambayo sisi katika Serikali hii lazima tujaribu tuwezavyo kuikidhi. Ndio maana
kuanzia juzi Mawaziri mbalimbali wanazungumzia mafanikio katika hizo siku 100,
kila mmoja akienda kwa undani kwenye sekta yake. Nawaomba wananchi wafuatilie
kwa karibu yale ambayo Mawaziri hawa wanayatolea taarifa kwenu ikiwa ni sehemu
ya uwajibikaji wao kwa wananchi.
Mimi pia, kwa nafasi yangu ya Katibu
Mkuu Kiongozi, ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa
Umma, nimepokea maswali mengi ya waandishi wa habari na wananchi wengine kuhusu
siku 100 za kwanza za uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Maeneo yanayohusu sekta mbalimbali yatazungumzwa na Mawaziri wanaohusika.
Lakini nimeona baadhi ya maswali yanaweza kujibiwa tu na ofisi hii, yaani
Ikulu.
Nimeyaweka maswali hayo katika makundi
matano na nitayazungumzia kwa ujumla:
· Yapo maswali
yanayohusu uongozi wa Rais wetu;
· Yapo maswali
yanayohusu sifa binafsi za Rais wetu;
· Yapo maswali
yanayohusu utendaji wake;
· Yapo maswali
yanayohusu mahusiano yake na sekta binafsi kwenye utawala wake; na
· Yapo maswali
yanayohusu mwelekeo wake kwenye mambo ya nje na diplomasia ya Tanzania.
Uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Tano Ukoje?
Wahenga walisema, “Nyota njema
huonekana asubuhi.” Naam! Katika siku 100 za kwanza, Rais Magufuli
amethibitisha kwa uwazi zaidi kuwa yeye ni kiongozi bora na wa kupigiwa mfano.
Taarifa tunazoletewa na wananchi ni kuwa kwa kauli, matendo na dhamira yake,
wananchi wengi wamemwelewa, wamemkubali na wanamwamini. Katika hizi siku 100,
Rais amewathibitishia Watanzania kuwa yeye ni kiongozi, mwenye sifa muhimu za uongozi. Sifa hizo ni pamoja na:
· Kiongozi
bora lazima awe na dira, maono na malengo kuhusu anakotaka Taifa liende. Katika
siku 100 za kwanza Rais Magufuli amedhihirisha kuwa ana sifa hiyo.
· Lakini
dira bila mkakati ni ndoto. Kiongozi bora lazima awe na mikakati ya kutekeleza
dira na maono yake, pamoja na kufikia malengo katika vipindi tofauti. Katika
siku 100 za kwanza Rais Magufuli amedhihirisha anayo sifa hiyo.
· Kiongozi
bora lazima aheshimike na awe na mvuto wa kuwafanya wananchi wamwamini, na
kumfuata. Katika siku 100 za kwanza za utawala wake, Rais amewafanya hata ambao
hawakumpigia kura, wamwamini, wamwombee na kumfuata.
· Kiongozi
bora anagawa majukumu, na haogopi kufanya hivyo, lakini anafuatilia. Katika
siku 100 za kwanza Rais Magufuli amethibitisha kuwa anayo sifa hiyo.
· Kiongozi
bora anajua na haogopi kuweka vipaumbele na mpangilio wake wa utekelezaji na
kuvisimamia. Katika hizi siku 100 Rais Magufuli amethibitisha anayo sifa hiyo
muhimu ya uongozi.
· Kiongozi
bora haogopi kufanya maamuzi magumu. Hakuna mwenye shaka kuwa katika hizi siku
100, Rais wetu amedhihirisha kwa kauli na kwa vitendo kuwa, anapotetea maslahi
ya Taifa na wananchi, haogopi kufanya na kusimamia maamuzi magumu.
Rais ana Maono
na Mikakati pevu ya kutimiza maono yake
Kama nilivyosema, sifa mojawapo ya
kiongozi bora, ni kuwa na maono pevu na mikakati madhubuti inayotekelezeka, ya
kutimiza maono hayo kwa faida ya wananchi. Tumeona haya kwa Rais Magufuli na
Serikali yake katika siku 100 za kwanza. Tangu wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu, Rais Magufuli aliweka bayana maono ya Tanzania anayotaka kuijenga, na
nini kifanyike ili kutimiza azma hiyo. Maono na shauku yake, kama ilivyo kwetu
sote, ni kujenga Tanzania mpya yenye uhuru, haki, neema na fursa mbalimbali kwa
wananchi wote; Tanzania yenye amani na utulivu; Tanzania yenye uchumi imara
unaotegemea viwanda; Tanzania ambayo kila mtu ananufaika na rasilimali
tulizonazo; na Tanzania isiyo na rushwa, ufisadi na dhuluma.
Rais
anabadili utendaji wa Serikali
Mtakumbuka, kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano, iliahidi kuendeleza misingi imara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii
iliyojengwa na awamu zilizotangulia. Pia iliahidi kuwa, katika juhudi zake za
kuinua uchumi na kuondoa kero zinazowakabili wananchi, itazingatia vipaumbele
vifuatavyo katika kubadili na kuboresha utendaji Serikalini.
1. Kupunguza
urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali;
2. Kuongeza
kasi ya ukusanyaji mapato na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wenye maslahi
kwa Taifa, hususan katika sekta ya viwanda;
3. Kubana
matumizi, kwa kupunguza yale ambayo kwa kuzingatia hali yetu ya uchumi kwa
sasa, yanaweza kuepukika;
4. Kuimarisha
huduma za jamii, hasa katika maeneo yenye kero zaidi kwa wananchi;
5. Kuhimiza
na kusimamia utii wa sheria, kurejesha nidhamu ya Serikali, na uzingatiwaji wa
maadili kwa viongozi wa umma na watumishi wote wa Serikali, sekta binafsi na
watu wote kwa ujumla;
6. Kudumisha
ulinzi na usalama, na kuendeleza mahusiano mazuri na yenye tija baina ya
Tanzania na nchi za nje, mashirika na taasisi za kikanda na kimataifa, pamoja
na wabia wengine wa maendeleo.
Amiri
Jeshi Mkuu
Katika
siku hizi 100 za kwanza, Rais ametekeleza majukumu yake ya Amiri Jeshi Mkuu kwa
wepesi na uhodari kama vile samaki kwenye maji. Amekuwa karibu na Jeshi na
viongozi wake. Amekagua vifaa vya Jeshi na mazoezi ya kijeshi. Ameteua viongozi
wa Jeshi, na kutoa kamisheni kwa Maafisa Wapya. Ametoa maelekezo mahususi ya
kuimarisha Jeshi na utendaji wake.
Sifa Binafsi za
Rais Magufuli
Kundi la pili la maswali tuliyoletewa linahusu
sifa binafsi za Rais Magufuli ambazo zimedhihirika katika hizi siku 100 za
uongozi wake. Nitataja chache.
· Mkweli
Katika
hizi siku 100, Rais wetu amewadhihirishia Watanzania kuwa ni mkweli,
anayechukia ulaghai na unafiki. Anaposema, “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu”
anamaanisha hivyo kwa dhati. Wapo watu wanaofikiri kuwa siasa ni ujanja na
ulaghai. Rais wetu amethibitisha kuwa yeye si mwanasiasa wa aina hiyo. Hakuna
tofauti kati ya alivyokuwa akiwa mgombea na alivyojidhihirisha katika siku 100
za kwanza za Urais. Watanzania wana kila sababu ya kufurahi kuwa alivyojinadi
ndivyo anavyotawala.
· Anatekeleza ahadi
Katika
siku 100 Rais wetu amethibitisha kuwa anaheshimu ahadi zake na anazitekeleza
kadri iwezekanavyo. Tayari ipo mifano kadhaa. Aliahidi kupunguza ukubwa wa
Serikali, na amefanya hivyo kwa kupunguza idadi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri
kutoka 55 hadi 35. Amepunguza pia idadi ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu
Wakuu kutoka 56 hadi 50. Aliahidi elimu ya msingi (mpaka kidato cha nne) bila
malipo na ametekeleza. Alipoiahidi Mahakama kuwa atawapa fedha zao zote za
maendeleo, Sh.12.3 bilioni, ndani ya siku tano, ametekeleza hata kabla siku
hizo hazijaisha. Na mifano mingine ipo ya anavyotekeleza ahadi zake. Kwa ufupi,
aliahidi kuwa hatawaangusha Watanzania na kweli hajawaangusha katika hizi siku
100.
· Anajali kwa Dhati Shida
na Kero za Wananchi.
Katika
siku 100 za kwanza, Rais ameonesha namna anavyoumizwa na kufadhaishwa na kero
zinazowakabili wananchi. Pia amethibitisha dhamira yake ya dhati ya kuzipatia
ufumbuzi, hususan katika upatikanaji wa huduma za jamii ikiwamo huduma za afya,
elimu na maji.
Kasi
ya kutatua kero za wananchi imeongezeka sana. Ndani ya siku hizi 100, tuna
mifano mingi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kuondoa kero, zingine zikiwa
za muda mrefu sana. Mmemsikia Waziri wa Ardhi akizungumzia utatuzi wa mgogoro
wa muda mrefu wa shamba la Kapunga katika Wilaya ya Mbarali (Mbeya), ambapo
hekta 1,870 tayari zimerejeshwa kwa wananchi. Aidha, mmesikia urejeshwaji
kwenye miliki ya serikali, kiwanda cha chai cha Mponde, kilichopo mkoani Tanga,
ambacho kilikuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu. Kila Waziri ataeleza mifano
mingine mingi, kwenye kila sekta, kuonesha kasi mpya ya kumaliza kero na shida
za wananchi.
Usimamizi wa
Nidhamu bila Uwoga
Sifa nyingine ya Uongozi wa Serikali ya
Awamu ya Tano iliyodhihirika katika kipindi cha siku 100 za kwanza ni uwezo wa
kusimamia nidhamu bila upendeleo ama uwoga. Orodha ni kubwa ya viongozi na
watumishi waliochukuliwa hatua mbalimbali za kisheria na kinidhamu kwa
kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu
ya Tano zimepambanua wazi ni aina gani ya uongozi na utumishi wa umma unatakiwa
katika serikali hii. Imedhihirika wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitamvumilia
kiongozi au mtumishi yeyote wa umma atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake
ipasavyo, au kufanya maamuzi yanayolenga kumnufaisha yeye binafsi. Na tayari
mrejesho tunaoupata kutoka kwa wananchi ni kuwa nidhamu kwenye utumishi wa Umma
imeongezeka na wananchi wanahudumiwa kwa haraka zaidi, na kwa heshima zaidi.
Tumedhamiria kurejesha
nidhamu ya kazi na kutokomeza utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea na
kujinufaisha. Katika tafsiri pana zaidi, hatua hizo zinalenga kukuza utamaduni
wa uadilifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa uhodari, bidii na ufanisi mkubwa,
kunakoendana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Na ndio maana Rais aliwalisha
kiapo cha Uadilifu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote aliowateua.
Kamwe Watumishi wa Umma wasisahau kuwa wao ni watumishi, sio mabwana, wa
wananchi. Wawatumikie kwa ufanisi, kwa uaminifu na kwa heshima.
Ukaribu na
Wananchi na Uungwaji Mkono
Siku 100 za kwanza za Utawala wa Awamu
ya Tano zimethibitisha ukweli wa usemi usemao “imani, hujenga imani.” Ndani ya
siku hizi 100, Serikali imefarijika kuona namna wananchi wengi, bila kujali
itikadi zao, walivyoonesha imani kubwa kwa Mheshimiwa Rais na Serikali yake na
jinsi wanavyoiunga mkono. Kwa upande mwingine tumeshuhudia jinsi Mheshimiwa
Rais na serikali yake ilivyo karibu na wananchi na namna wananchi wanavyozidi
kumfurahia Rais wao.
Na wanafanya hivyo kwa vile wamemkubali
kama kiongozi wao, na wanamwamini. Hivyo moja ya mafanikio makubwa katika hizi
siku 100 ni vile ambavyo Rais ameweza kujijengea imani kubwa miongoni mwa
wananchi wenzake, na kuwaunganisha katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao
bila kuangalia vyama, dini, kabila na rangi zao.
Utekelezaji wa
Vipaumbele
Moja ya mambo makubwa tuliyojifunza kutoka
kwa Rais wetu katika siku 100 za kwanza za Serikali yake ni umuhimu wa
kupambanua na kuelekeza rasilimali zetu katika maeneo ya vipaumbele zaidi.
Serikali ya Awamu ya Tano imewawezesha wananchi wote kufahamu kuwa, nchi yetu
haiwezi kupiga hatua kubwa kimaendeleo, itakayotuwezesha kumaliza kero zinazotukabili
na kufikia hadhi ya nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025, bila ya kuwa na
vipaumbele. Si kwamba dhana ya vipaumbele ni mpya. La hasha. Tulikuwa
tunaizungumzia siku zote. Lakini Rais huyu ameitekeleza kwa namna iliyovuta
hisia za Watanzania na watu wengine wengi barani Afrika na duniani. Mifano ni
kama ifuatavyo:
· Badala
ya sherehe za Uhuru, tumefanya usafi ili kupambana na kipindupindu, na fedha
zilizookolewa zinajenga sehemu ya barabara iliyokuwa kero kubwa kwa wananchi.
· Badala
ya Rais na Wabunge kujipongeza kwa sherehe kubwa, fedha zilizookolewa zimetatua
tatizo la vitanda kwa wagonjwa.
· Badala
ya sherehe za siku ya UKIMWI, fedha zimekwenda kununua dawa za kufubaisha makali
ya UKIMWI.
· Badala
ya semina elekezi ya Mawaziri, fedha zake zitakwenda kutekeleza mradi wa
kufunga vifaa vya kisasa vya kuchunguza magonjwa katika hospitali 37 kote
nchini.
· Badala
ya safari za nje fedha zilizookolewa zitatumika kwenye miradi ya maendeleo.
Zaidi ya Sh.7 bilioni ambazo zingeweza kutumika kwa safari za nje zimeokolewa katika
siku 100 na zitatumika kwenye miradi hiyo ya maendeleo.
Hatua hizo, na nyingine nyingi, zimevuta
hisia za watu mbalimbali kote duniani. Mnaofuatilia mitandao ya kijamii mnajua
hivyo, na wapo wameonesha wazi kutamani tungewaazima Rais wetu kwa muda.
Mapato
Katika siku 100 za kwanza Serikali
imefanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi na mapato yasiyo ya kodi. Katika kipindi
cha siku 100 za kwanza, mapato ya kodi yameongezeka hadi kufikia Shilingi
trilioni 3.34, ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 2.59 kwa
kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2014/15, ikiwa ni ongezeko la Shilingi
bilioni 746.31. Hali kadhalika, kwa mapato yasiyo na kodi, makusanyo
yameongezeka hadi kufikia Shilingi bilioni 281.68, kutoka Shilingi bilioni
224.03 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2014/15, ikiwa ni ongezeko la
Shilingi bilioni 57.65. Nyote mmesikia, baada ya kashikashi pale Hospitali ya
Taifa Muhimbili, mapato yao yameongezeka maradufu na kuwapa uwezo mkubwa zaidi
wa kuhudumia wananchi. Hali ni hiyo pia kwenye Halmashauri.
Ukusanyaji huu wa mapato, umeiwezesha
Serikali kugharamia baadhi ya miradi yake kwa fedha za ndani, mathalan,
kuwalipa wakandarasi, kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji, miundombinu,
umeme, kilimo, uwezeshaji wa vijana na kadhalika. Naamini kasi iliyopo sasa
itaongezeka kwa siku zijazo na kutupatia uhuru zaidi wa utekelezaji wa mipango
yetu. Kwa msingi huo nawasihi wananchi wadumishe uzalendo kwa kulipa kodi kwa
kila bidhaa wanazonunua, kwani mapato hayo ni kwa ajili ya kuwahudumia. Pia
msisite kutoa taarifa za wakwepa kodi, ambao watashughulikiwa ipasavyo kwa
mujibu wa sheria.
Ushirikiano na
Sekta Binafsi
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria
kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi unaolenga kumnufaisha kila
Mtanzania. Aidha, inaamini kuwa sekta binafsi ni muhimili muhimu katika
kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, ukiwemo wa viwanda. Ndiyo maana, hata kabla
hajaunda Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Rais alikutana na wafanyabiashara na
wawekezaji wa sekta binafsi, katika juma la kwanza tu, baada ya kuingia
madarakani ambapo, pamoja na mambo mengine, aliwahakikishia utayari na dhamira
ya Serikali yake kuipa ushirikiano sekta hiyo.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali iko
tayari kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa ajili ya kuongeza kasi ya
uwekezaji endelevu na wenye tija kwa Serikali na Wananchi, mathalan miundombinu
ya nishati, reli na barabara, viwanja vya ndege, bandari, maji, mawasiliano na
upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda. Pia aliwataka wazingatie wajibu
wao wa kulipa kodi na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za nchi katika
shughuli zao za uwekezaji na biashara.
Vile vile katika hizi siku 100, Rais
amethibitisha nia yake ya kutoa fursa sawa kwa sekta binafsi. Ameonesha kuwa
wenye fedha wasiwe na kiburi cha fedha, wakifikiri wana leseni ya kufanya
watakavyo au kuonea wengine. Bali kila mfanyabiashara ambaye ni mtiifu,
anayetenda haki na kufuata sheria, atamwona Rais Magufuli kuwa ni mbia wake
katika kukuza uchumi wa Taifa letu.
Sera ya Mambo ya
Nje
Tanzania tunajivunia msingi imara wa
diplomasia na mahusiano mazuri ya kimataifa, uliowekwa na Viongozi wetu,
kuanzia Awamu ya Kwanza iliyojikita katika ukombozi wa Mwafrika na jamii
nyingine zinazotawaliwa duniani, hadi Awamu ya Nne iliyoendeleza diplomasia ya
uchumi.
Hata hivyo, Rais wa Awamu ya Tano,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, anatambua pia kwa nadharia ya
diplomasia na mahusiano ya kimataifa inabainisha kuwa sera ya mambo ya nje
inaakisi sera za ndani ya nchi. Foreign
policy is an extension of domestic policy.
Tofauti na wanaomlaumu Rais kwa
kutosafiri nje ya nchi, Rais wetu anafahamu na kushukuru sana kuwa Marais waliomtangulia
wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kujenga mahusiano yetu na nchi za nje na
kuimarisha diplomasia yetu. Lakini Rais anatambua kuwa ili ailinde sifa hiyo, na
kuikuza, lazima anyooshe mambo kadhaa ndani ya nchi. Iwapo Tanzania itabaki
kuwa maskini, yenye rushwa, ujangili, madawa ya kulevya, na kadhalika hiyo sifa
nzuri nje ya nchi itaporomoka. Hivyo ameamua kujipa muda kuimarisha uchumi na
maendeleo ndani ya nchi, na kupambana na matatizo mengine yanayoharibu sifa
yetu, ili iwe rahisi kudumisha sifa ya Tanzania nje ya nchi.
Wengi mtakubaliana nami kwamba hatua
anazochukua Rais Magufuli kuimarisha mifumo na utendaji wa humu ndani, umeipa
sifa kubwa Tanzania huko nje pamoja na kwamba yeye binafsi hajasafiri kwenda
nje ya nchi tangu achaguliwe kuwa Rais. Hii inadhihirisha wazi kuwa mambo yetu
ya ndani yasiposhughulikiwa ipasavyo, kusafiri tu kwa Rais nje siyo kigezo cha
kudumisha heshima na urafiki mwema.
Napenda niwahakikishie wananchi wote
kuwa dunia inafuatilia yanayotokea nchini, na wanashahuku ya kuona matokeo
yake. Kila kona hivi sasa, nchi zinazungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya
Tano ndani ya siku 100. Hili ni jambo la kujivunia katika mahusiano yetu na
nchi za nje na ni jambo kubwa kidiplomasia.Rais amefanya kazi ya kutangaza
Tanzania na kujenga sifa yake bila haja ya kusafiri. Atakapokuwa tayari
atasafiri tu.
Hitimisho
Siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu
ya Tano, zimethibitisha kuwa Serikali yetu ni makini na imedhamiria kutekeleza
ahadi zake kwenu. Katika kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi wote,
Serikali imezingatia msingi uliowekwa na serikali za awamu zilizotangulia. Na
imedhamiria kutekeleza wajibu wake kwa Taifa na wananchi. Ushindi ni lazima.
Nikitakiwa kuelezea kwa maneno machache
sana siku 100 za utawala wa Rais Magufuli nitasema, ametuletea aina mpya ya
uongozi, unaojenga juu ya msingi wa waliomtangulia, lakini unaoweka Tanzania
katika gia mpya (new trajectory)
kuelekea uchumi wa kipato cha kati ulioahidiwa na Dira ya Maendeleo 2025.
Tumuunge mkono. Hapa
Kazi Tu!
Asanteni kwa kunisikiliza.
SAUTI YA BALOZI SEFUE HAPO CHINI
0 comments:
Post a Comment