TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watu wote
waliotelekeza Mashamba na Viwanda walivyouziwa na serikali, kuhakikisha
wanafufua mashamba na viwanda hivyo mapema iwezekanavyo, kabla serikali haijavinyang'anya
na kuwagawia wanaoweza kuviendesha.
Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliosimamisha
msafara wake njiani, wakati akisafiri kwa gari kutoka Dar es salaam kwenda
Dodoma.
Amesema
mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi na mashamba mengi makubwa ambayo kama
waliouziwa wangeyaendeleza, yangezalisha ajira na kuongeza uzalishaji wa bidhaa
za viwandani na Mazao ya kilimo, lakini waliouziwa mashamba na viwanda hivyo
wameamua kutekeleza ama kubadilisha matumizi, huku wengine wakitumia rasilimali
hizo kuombea mikopo katika mabenki jambo ambalo serikali yake haitalikubali.
"Kama
nilivyowaahidi wakati wa kampeni na leo narudia, wote walioamua kutumia
mashamba na viwanda walivyouziwa na serikali kwa ajili ya kuchukulia mikopo
kwenye mabenki badala ya kufanya uzalishaji wavifufue haraka, vinginevyo
tutawanyang'anya" amesisitiza Rais Magufuli huku akishangiliwa na
wananchi waliomsimamisha katika eneo la Msamvu Mjini Morogoro.
Rais
Magufuli pia amesimamishwa na kuwasalimu wananchi wa Wami Dakawa, Magole na Dumila
ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa atatekeleza ahadi yake ya kuwapa mashamba
atakayonyang'anya kutoka kwa walioyatelekeza, amewataka kuachana na migogoro
kati ya wakulima na wafugaji na badala yake watatue migogoro hiyo kwa kutumia
njia za kisheria.
Aidha,
amewataka viongozi wote wa Mkoa hadi vitongoji kushirikiana kutatua migogoro ya
wakulima na wafugaji kabla haijasababisha madhara, na ameonya kuwa migogoro
hiyo ikileta madhara itakuwa ni kigezo tosha kuwa viongozi hao wameshindwa
kutekeleza wajibu wao na wanapaswa kuachia ngazi.
Pamoja
na hayo Rais Magufuli amewahimiza wananchi hao kuchapa kazi kwa juhudi hasa
katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha, na pia wahakikishe kuwa watoto
wote wanaopaswa kuandikishwa shule wanapelekwa shule, hasa baada ya serikali
kuamua kutoa elimu bure ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
"Tumeamua
kutoa elimu bure na tutatoa elimu bure, na jambo hili limeonesha mafanikio
makubwa kwa kuwa hata shule zilizotarajia kuandikisha wanafunzi 45 zimejikuta
zikiandikisha hadi wanafunzi 600 kwa darasa moja" alibainisha Rais
Magufuli.
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli amekagua kipande cha barabara kuu ya Morogoro -
Dodoma kilichoharibiwa na maji ya mvua katika eneo la Kibaigwa Mkoani Dodoma,
na kujionea kazi za ukarabati zinazofanywa na wakala wa barabara nchini
(TANROADS).
Amemuagiza
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, kuongeza
wakandalasi wa kukarabati eneo hilo ili kazi ikamilike haraka badala ya
kusubiri mpaka baada ya miezi miwili ilivyopangwa na wizara.
Wakati
huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kesho
tarehe 06 Januari, 2016 atashiriki maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitakazofanyika katika uwanja wa Namfua, Mjini
Singida.
Gerson
Msigwa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
05 Januari,
2016
0 comments:
Post a Comment