Katika kukabiliana na Vifo vya Wajawazito na
Watoto Zanzibar Taasisi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kama KANGA imezinduliwa
rasmi ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo nchini.
Uzinduzi wa Taasisi hiyo umefanyika
katika Viwanja vya Hospitali ya Mnazi mmoja na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali
wa ndani na nje ya Zanzibar.
Akitoa ufafanuzi wa kuanzishwa kwake
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Dkt.Mohamed Hafidh amesema Serikali na Taasisi
binafsi zinawajibu wa kuzidisha mikakati ya kukabiliana na Vifo kwa akinamama
na watoto ili kuwa na taifa endelevu.
Amebainisha kuwa wapo baadhi ya watu
wenye uwezo wa kuchangia lakini wanashindwa kujua wapi watapeleka Misaada yao
ili kuokoa maisha ya watoto na akinamama.
Dkt. Mohamed ameongeza kuwa hata
Serikali kupitia Wizara ya Afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali za
matibabu nakwamba uwepo wa
Taasisi ya KANGA kutasaidia kwa kiasi kikubwa juhudi
za Serikali kukabiliana na tatizo hilo nchini.
“Ukweli nikwamba wapo wasamaria wema wanaguswa
na hali ya vifo vya Wajawazito na Watoto lakini wanashindwa wapi kwa kupeleka
misaada yao lakini kupitia Taasisi hii ya KANGA basi itakuwa ni sehemu muafaka
ya kupeleka misaada yao na bila shaka lengo litafikiwa”Alisema Dkt. Mohammed
Hafidh
Dkt Mohamed amesema hali ya Vifo nchini bado
inatisha na kufafanua kwamba kati ya Kinamama Wajawazito Laki moja,wastani wa
460 hupoteza maisha yao nchini ambapo kwa nchi za Ulaya Idadi kama hiyo ni
wastani wa watu sita wanaopoteza maisha.
Ameongeza kuwa Wastani wa Watoto 29 kati ya
Elfu moja wanaozaliwa hufariki dunia nchini Tanzania ambapo kwa nchi za Ulaya
ni Wastani wa watoto watatu wanaopoteza maisha miongoni mwa watoto Elfu moja.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika uzinduzi
huo Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Shekh
Abdallah Talib amewaomba Viongozi na wananchi kwa ujumla kuiunga mkono Taasisi
hiyo kwa kuchangia jitihada zake za kukabiliana na changamoto zinazowakabili
wazazi na Watoto katika kipindi cha ujauzito na kujifungua.
Amesema kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe
ameahidi kukwata kiasi Fulani cha Mshahara wake kila mwezi ili kuchangia
harakati za Taasisi ya KANGA.
“Kwa namna ambavyo nimeguswa na Malengo ya
Taasisi ya KANGA na kwa namna ambavyo Tatizo la Vifo kwa Wajawazito na watoto
linavyoendelea naahidi kukatwa Mshahara wangu kila mwezi kusapoti Taasisi
hii”Alisema Shekh Talib
Taasisi ya KANGA ambayo imezinduliwa imejikita
katika kujitolea kupambana na tatizo la Vifo kwa watoto na akinamama wakati wa
ujauzito ambapo pia malengo ya baadae itaratibu uwepo wa Madaktari Wanawake wa
kutosha ili taratibu za Uzazi zote Hospitalini zifanywe na Wanawake wenyewe
badala ya Wanaume kama ilivyo sasa.
Katika uzinduzi huo Taasisi mbalimbali
zilihudhuria na kutoa michango yao ikiwemo Mfuko wa Huduma za jamii Zanzibar
ZSSF, Bank ya Watu wa Zanzibar, Taasisi ya Daraja Faoundation.
Maelezo Zanzibar 23/01/2016
0 comments:
Post a Comment