January 22, 2016

KAMPUNI ya simu ya Zantel, leo imeukabidhi uongozi wa skuli ya msingi Kisiwandui hundi ya shilingi milioni 20, kwa ajili ya kununulia vifaa vya wanafunzi wenye uoni hafifu.
Hundi hiyo ilikabidhiwa kwa mwalimu mkuu wa skuli hiyo Bi. Taifa Ahmed Khamis, na Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Bw. Benoit Janin, katika hafla fupi iliyofanyika skulini hapo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Janin alisema msaada huo ni sehemu ya mikakati ya kampuni yake, katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu bora bila kujali tofauti za kimaumbile.   
Alieleza kuwa, ni wajibu wa kampuni hiyo kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata msaada kama wanavypata watu wengine, na pia kuweza kuwaandaa kwa ajili ya kuweza kufikia malengo yao kama walivyokusudia.
“Kama sehemu ya jamii, tumedhamiria kuwasaidia kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu kwa kuwapatia vifaa wanavyovihitaji ili waweze kupata elimu bora,” alieleza Mkurugenzi huyo.
Aidha, alisema kuanzia leo, kampuni yake imeamua kuwa mlezi wa darasa la wanafunzi wenye uoni hafifu katika skuli hiyo, kwa kuwapatia mahitaji yao ili waweze kusoma bila matatizo.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Bi. Taifa Ahmed Khamis, akiushukuru uongozi wa Zantel, alisema msaada huo ni wa kipekee na utarahisisha ufundishaji kwa wanafunzi hao wenye matatizo ya uoni, na hivyo kuwawezesha kupata elimu bora kama ilivyo kwa wengine.
“Tunawashukuru Zantel kwa kuziona changamoto zinazotukabili, na hakika msaada huu utatusaidia katika kuwafundisha wanafunzi hawa na pia kuwawezesha kufikia malengo yao,” alifafanua.
Alitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni mashine za nukta nundu, karatasi za kuchapishia, miwani pamoja na fimbo maalumu kwa watu wasioona (white canes).
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maandalizi na Msingi Bi. Safia Ali Rijali, pamoja na kuishukuru Zantel katika kusaidia jitihada za serikali kuleta maendeleo, alisema elimu ni muhimu kwa kila mwananchi hata wenye ulemavu.
Aliwasisitiza wazazi na walezi kutowatenga watoto wenye ulemavu kwa kuwakosesha haki ya kusoma, kwani wakipewa fursa wanaweza kufanya makubwa na kuwa mfano kwa wengine.
Alitoa mfano wa mwanafunzi mmoja asiyeona aliyekuwa akisoma Kisiwandui, kwa namna alivyokuwa mahiri hata akaweza kuchukua digrii ya sheria.
Mkurugenzi huyo ameziomba taasisi na kampuni nyengine kuiga mfano wa Zantel kujikita katika kusaidia jamii kwa mahitaji mbalimbali, yakiwemo ya kielimu, kiafya na mengine.
Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Benoit Janin akisaini
barua ya kampuni yake kwa ajili ya kuwa mlezi wa
darasa la wanafunzi wenye ulemavu wa uoni wa skuli
ya  msingi Kisiwandui mjini Zanzibar




Habari Maelezo-Zanzibar

0 comments:

Post a Comment