January 05, 2016

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema kukosekana ushirikiano katika kutoa ushahidi Mahakamani dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya kumesabisha kufutwa kesi nyingi hali inayodumza juhudi za Serikali katika vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo.
Amesema suala la Dawa za kulevya hivi sasa limekuwa janga la Dunia na limeathiri watu wengi hasa Vijana hivyo udhibiti wa matumizi yake unahitaji maamuzi magumu ya Serikali pamoja na ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Dunia kwa ujumla.
ameeleza kuwa kwa sasa wakati umefika kwa wananchi kulazimika kutoa ushirikiano ili kusaidia kufanikisha azma ya Serikali ya kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya Nchini.
Balozi Seif amefahamisha kuwa licha ya changamoto zilizopo za utekelezaji wa sheria na kanuni katika kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na matumizi ya dawa hizo Zanzibar lakini Serikali imefanikiwa kuwakamata wahusika wa biashara hiyo kiasi 48 na Kilo 354.7 za dawa za kulevya zikiwemo bangi na heroin katika kipindi cha mwaka 2015.
 Aongeza kuwa kati ya  watuhimiwa hao baadhi wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria na wawili wawili walifutiwa makosa yao baada ya kukosekana ushahidi, na mashtaka 18 yanaendelea kusikilizwa mahakamani na mengine 28 yaliyobakia yanaendelea na kufanyiwa uchunguzi.
Ameitaja moja ya kikwazo ni suala la rushwa alilodai kwa kiasi kikubwa kinakwamisha mafanikio dhidi ya vita vya dawa za kulevya licha ya juhudi kubwa inayochukuliwa na katika kupambana nayo Zanzibar.
“Wananchi wako karibu na maeneo yanayolimwa na kuzwa bangi, Polisi na uhamiaji wanayo nafasi kubwa ya kuwatambua wanaoingiza na kuuza dawa za kulevya, Ofisi ya Mkurugenzi mashtaka inayo wajibu wa kutayarisha hati zisizokuwa na kasoro na mahakama ina jukumu la  kuharakisha  kutoa hukumu stahiki kwa mujibu wa sheria “. Amesema Balozi Seif.
Amesema hayo alipokuwa akiweka jiwe la msingi jenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya Tabia kwa Vijana wanaoacha Dawa za kulevya huko Kidimni, Wilaya ya Kati Unaguja ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 Mapema katika akitoa taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr.Omar Dadi Shajak amesema ujenzi wa kituo hicho unagharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa zaidi ya Shilingi Bilioni  4.2 hadi kukamilika kwake kitakuwa na uwezo wa kuhudumia Vijana wapato 200 ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwa na mafunzo ya kazi za amali, michezo na huduma nyengine za kurekebisha tabia.
                            



 

0 comments:

Post a Comment