Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umewataka
vijana Zanzibar kutobabaishwa na mjadala au mazungumzo ya viongozi wa kisiasa inayoendelea
kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu uliofutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
UVCCM imesema mazungumzo hayo ni sehemu ya harakati za
kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini na hayawezi kubadilisha uamuzi wa
ZEC katika uchaguzi huo.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo jana
katika mkutano wake na wajumbe wa umoja huo na viongozi wengine wa CCM ngazi za
kata, majimbo na wilaya kwenye ukumbi wa CCM Dimani, katika Mkoa wa Magharibi
Unguja.
Alisema Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ni mchakato unaosimamiwa na
Sheria ya Uchaguzi, hivyo hakuna yeyote mwenye mamlaka wala madaraka ya
kuiingilia ZEC, kuipangia au kulazimisha ipindishe sheria kwa maslahi ya
wachache.
“Kukaa kwetu kimya haimaanishi kwamba sisi si weledi wa kusema
na kujipamba kwa sifa na majigambo yasiyo na maana katika jamii, tunataka
tutofautishwe kati ya wanaojua na kuheshimu nguvu ya sheria na wale wanaoropoka
hovyo bila kujali maslahi ya nchi,” alisema.
Katibu Mkuu huyo aliwaeleza wanachama hao wa CCM kwamba, tangu
ZEC itangaze kufuta matokeo ya uchaguzi huo, kumekuwa na kauli mbalimbali za
kibabaishaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa upinzani, akiwemo Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
“Hatushindwi kumjibu Maalim Seif, chama chake na wote wanaomuunga
mkono, tunachelea kuonekana mbumbumbu mbele ya waelevu,” alisema
Shaka.
Alisema sheria inampa mamlaka Mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi kama alivyofanya baada ya kugundua kukiukwa kwa taratibu.
Alisema sheria inampa mamlaka Mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi kama alivyofanya baada ya kugundua kukiukwa kwa taratibu.
Kwa mujibu wa Shaka, baada ya uamuzi huo anaepita mitaani na
kusema anasubiri aapishwe awe Rais wa Zazibar wakati Ikulu ipo chini ya rais
halali kisheria, huyo anaota mchana na anajiweka wazi jinsi alivyo na uchu wa
madaraka.
Aidha, alisema mivutano itokanayo na utata wa kisheria haitamalizwa
na vinywa vya wanasiasa wenye tabia ya kukanyaga sheria au kubeza matakwa ya
katiba. Kwa mujibu wa shaka, sehemu yoyote inayohitaji msaada wa mazungumzo, ni
jambo la kawaida kwa wanasiasa na viongozi kukutana, ingawa hatua hiyo
haihalalishi kuvunjwa kwa sheria na katiba ya nchi.
Shaka alisema uendeshaji wa nchi yoyote duniani, husimamiwa na
kulindwa kisheria na katiba, hivyo kinaweza kuwa kituko iwapo mwanasiasa
atadhani kwa kushinikiza jambo, anaweza kupewa nafasi ya uongozi wa juu wa
nchi.
“Iwapo ZEC imefuta
matokeo ya Uchaguzi Mkuu kutokana na uwezo wa kisheria walionao, sasa ni wajibu
wao tena kuwaeleza wananchi ni lini watapiga kura tena, ili watimize haki yao
ya kuchagua na kuchaguliwa kidemokrasia,” alisisitiza.
Aliwataka vijana wa CCM kuwa makini, wavumilivu na wenye ari ya
kudumisha mapinduzi yao, huku akiwataka kusahau wale wote wenye mawazo ya
kutaka kuyazika kwa kuwa hilo halitawezekana milele.
0 comments:
Post a Comment