Harakati za ujenzi wa Nyumba za
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} za kuwakopesha wanachama
wake pamoja na kuuzwa kwa wananchi zinaendelea vizuri katika eneo la Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Abdulwakil Haji Hafidh amesema mradi huo ulioanza
Septemba mwaka uliopita utakaokuwa na Majumba 18 kila moja lina Ghorofa
Saba lenye Fleti 252 utajengwa kwa awamu tatu tofauti unatarajiwa kugharimu
jumla ya shilingi Bilioni Arubaini na Sita { 46,000,000,000/- } hadi kukamilika
kwake.
Amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kuwa mipango
maalum imeshaandaliwa ya jinsi nyumba hizo zitakavyotoa huduma.
Amesema baadhi zitauzwa kwa wanachama na
wateja moja kwa moja, nyengine zitakodishwa kwa wateja ambao baadaye watakuwa
na uwezo wa kuzinunua.
Amesema utaratibu
mwengine utaandaliwa ili kuwapa fursa wanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii
wenye kipato kidogo kukopeshwa nyumba hizo kupitia udhamini wa Benki ya Watu wa
Zanzibar { PBZ } ambapo mteja anaweza kutumia kiinua mgongo chake kwa kulipia
nyumba atakayoihitaji.
Naye Meneja
Mipango,Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Khalifa
Muumin Hilal amesema majengo hayo yatajumuisha Maduka, sehemu za
burdani ya watoto pamoja na eneo maalum litakalotengwa kwa ajili ya maegesho ya
vyombo vya moto sambamba na eneo la michezo tofauti.
Kwa upande wake Msanifu
Majengo anayesimamia Mradi huo Mahsen Mahd amefafanua kuwa ujenzi wa majengo
hayo unazingatia taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ikiwemo
kuwashirikisha wataalamu wa Taasisi za ujenzi pamoja na watendaji wa Baraza la
Manispaa sambamba na vigezo vinavyotumika katika majengo ya Kimataifa.
Akielezea matumaini ya
mradi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameushauri Uongozi
wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar kuhakikisha viwango vya nyumba hizo vinakuwa
na fursa pana ya kuwafaidisha wanachama wa Mfuko huo wenye Vipato tofauti.
Balozi Seif alisema hatua
hiyo itasaidia kuleta faraja kwa wanachama wa ngazi zote watakaokuwa na nia ya
kutaka kununua, kukodi au kukopeshwa nyumba hizo kwa mujibu wa uwezo aliokuwa
nao muhusika.
0 comments:
Post a Comment