STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
17 Aprili, 2014
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumla
ya kampuni 160, alama za biashara 430, majina ya biashara 280, jumuiya za
kiraia 67 na nyaraka 583 zimesajiliwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa
fedha 2013/2014.
Akiwasilisha
taarifa ya Utekelezaji Mpangokazi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kipindi cha
Julai 2013 hadi Machi 2014 jana Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Assaa Ahmad Rashid
alieleza pia kuwa katika kipindi hicho Wizara imesajili vizazi 27,445 kote
nchini.
Alibainisha
kuwa kati ya vizazi hivyo 13,742 ni wanaume na 13,703 ni wanawake huku vifo
vilivyosajiliwa vikiwa ni 1,648 kati yake wanawake ni 760 na wanaume 888.
Katika
kikao hicho Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa katika kuimarisha utoaji huduma
za Zakka na Wakfu Wizara katika kipindi hicho imeendelea na jitihada za
kuelimisha waumini kuhusu masuala hayo ambapo mikutano 24 iliyokusanya wadau
mbalimbali ilifanyika na miongozo ya zakka, mirathi na Wakfu iligawiwa Unguja
na Pemba pamoja na kutoa vipindi vya elimu kwa njia ya redio na televisheni.
Katika
hatua nyingine taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara imo mbioni kukiimarisha Kituo
cha Utafiti na Mafunzo ya Sheria Zanzibar ambapo hivi karibuni kinatarajiwa
kupata hati ya utambulisho(accreditation) ili kuanza kutoa mafunzo ya sheria
katika ngazi ya cheti na Stashahada kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
Kwa
upande wa hakimiliki taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara kwa mara ya kwanza
imeweza kugawa mirahaba kwa wasanii na wabunifu 726 ambapo jumla ya shilingi
milioni 36 ziligawiwa. Katika kipindi hicho Wizara imeweza pia kusimamia mapito
ya Sheria ya Hakimiliki.
Kuhusu
ukusanyaji wa mapato katika Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa hadi mwisho wa robo
tatu ya mwaka wa fedha Wizara imekusanya shilingi milioni 345.1 ikiwa ni sawa
na asilimia 79 ya lengo la kukusanya shilingi milioni 435.
Katika
kikao hicho kilichofanyika Ikulu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi DK. Ali Mohamed Shein amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali zilizo
na jukumu la kukusanya mapato kuongeza juhudi ili Serikali iweze kupata mapato
zaidi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alibainisha
kuwa mwenendo wa ukusanyanji mapato kwa upande wa Bodi ya Mapato Zanzibar- ZRB
na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA unakwenda vizuri kwa makusanyo kuongezeka
mwaka hadi mwaka lakini alisisitiza kuwa wizara na Taasisi nyingine zinapaswa
kuiga mfano wa taasisi hizo.
Mhe
Rais alizikumbusha Wizara kuzingatia utaratibu wa Bangokitita kwa kuwa ni
utaratibu endelevu unaokwenda sambamba na mfumo wa ukusanyaji mapato na
matumizi ya Serikali pamoja na utekelezaji wa kazi za Serikali ambao unategemea
bajeti iliyopangwa.
Katika
kikao hicho alihimiza uwekaji wa kumbukumbu za Serikali kwa kuanzisha na kuimarisha
maktaba katika wizara na taasisi za serikali ili kutoa fursa kwa watumishi
kuongeza taaluma zao na kujifunza mambo mbali yanayofanyika katika Wizara na
taasisi pamoja na duniani kwa jumla.
Kikao
hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria,katika kikao cha utekelezaji Mpango kazi kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar |
0 comments:
Post a Comment