September 07, 2016

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeshauriwa kuanzisha mitaala itakayowafundisha wanafunzi mbinu za kujiepusha na vishawishi vya ngono vinavyoweza kuwaletea madhara na mbimba za umri mdogo.
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Fatma Iddi Ali, amesema mafunzo hayo ni muhimu ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya watu waovu.
Akiwasilisha mada kwenye warsha ya mafunzo kuhusu vitendo vya udhalilishaji ametaja madhara yatokanayo na mimba za umri mdogo ikiwemo vifo vya mama na watoto na kuharibika kwa mfumo wa uzazi.
Ameeleza kuwa kuathirika kwa kizazi husababisha mama kutolewa fuko la uzazi na hivyo kumfanya asiweze kubeba ujauzito kabisa.
Aidha amewakumbusha wazazi wajibu wa kukaa na kuzungumzana watoto ili waweze kufahamu matatizo waliyonayo na kutafuta njia za kuyatatua mapema.
Mjumbe huyo wa ZAFELA pia amesisitiza jukumu la wazazi na wanajamii kurejesha malezi ya asili na kushirikiana katika kuwalea watoto ili wakue katika maadili mazuri. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Saada Salum Issa, amewahimiza wazazi kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao maskulini, hasa katika masomo ya ziada (Tuitions) kwani baadhi yao huitumia fursa hiyo kujiingiza katika vitendo viovu.
“Pamoja na hayo, wazazi pia wanapaswa kutowadekeza mno watoto wao kwani  kufanya hivyo kutawapa kiburi na kuvuka mipaka ya nidhamu,” amesema.




"MAELEZO

0 comments:

Post a Comment