SALAMU ZA PONGEZI ZA CCM
KWA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA
BARAZA LA MAPINDUZI MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN
KWA HOTUBA YAKE ALIYOITOA KATIKA UZINDUZI WA
BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR
TAREHE 05 APRILI, 2016.
CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kwa moyo mkunjufu kinampongeza
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed
Shein, kutokana na hotoba yake nzuri na dira kwa maendeleo ya Zanzibar na
wananchi wake, aliyoitoa jana Aprili 05, mwaka huu, wakati akizindua Baraza la
Tisa (9) la Wawakilishi Zanzibar.
Ni hotuba iliyosheheni mambo kadhaa ya maendeleo kiuchumi,
kisiasa na kiustawi wa jamii, mambo ambayo wananchi wanatarajia kuyaona
yakitekelezwa na Viongizi wao wa Kitaifa kwa mustakbali wa Taifa na Wazanzibari
wote.
Chama Cha Mapinduzi, kimeelezea kufarajika kwake kutokana na
hotuba ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt.
Shein, alipoihakikishia jamii nzima ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla
wake kwamba Serikali yake imekusudia kuwaleta maendeleo endelevu wananchi ndani
ya maendeleo yao, na hivyo kuondokana na umasikini hasa wa kipato.
Kupitia hotuba yake hiyo, wananchi walio wengi hasa wapenda
amani, utulivu na maendeleo, wamejenga matumaini makubwa kutokana na kauli ya
Mhe. Rais, na hasa pale alipowaahidi kwa kusema Serikali yake iliopo
madarakani na kupitia Mkuza II, itafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na ustawi
wa jamii, ili kuwawezesha Wazanzibari kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo
mwaka 2020.
Akifafanua zaidi, Dkt. Ali Mohamed Shein, alisema huo
miongoni mwa mikakati Serikali ya kuimarisha na kukuza uchumi wa nchi yetu na
pia kukuza pato la Taifa. Ili kufika azma hiyo, kipaumbele cha mwanzo cha
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kukuza uzalishaji kupitia sekta za kilimo,
utalii, viwanda vidogo vidogo, pamoja na kuimarisha raslimali watu, ubora wa
huduma za jamii ikiwemo Elimu, Afya, Mazingira, Utawala bora, nk, jambo ambalo
linapaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo wa Taifa hili.
Akizungumzia kuhusu uimarishaji wa sekta ya biashara, Mhe.
Dkt. Shein, amewataka Wazanzibari kutambua umuhimu wa zao la karafuu ambalo ni
uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar na kutoa wito kwa wananchi kuthamini juhudi
zinazochukuliwa na Serikali yao za kuimarisha zao hilo, ili liweze kuwaletea
tija zaidi.
Kama hiyo haitoshi, kauli ya Rais wa Zanzibar Mhe.
Dkt. Ali Mohamed Shein, ya kukubali kuwalipa wakulima wa karafuu kwa asilimia
80 ya bei ya zao hilo kwenye soko la dunia, inatoa matumaini mapya kwa wakulima
wa zao hilo wa Unguja na Pemba.
Kuhusu suala la uwekezaji, Mhe. Dkt. Shein, amewaeleza
Wazanzibari kuwa Serikali anayoiongoza imekusudia kushajiisha vyema wawezeshaji
wa nje kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza hasa ujenzi wa hoteli za kisasa za
kitalii na utoaji wake wa huduma ya fani hiyo, jambo ambalo kila Mzanzibari
anatakiwa kuliunga mkono kwa nguvu zote.
Kauli ya Mhe. Rais wa Zanzibar ya kuwahakikishia
wananchi kutekeleza ahadi mbali mbali alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wa kima cha chini
nchini kufikia Tsh. 300,000 kwa mwezi, pamoja na Idara Maalum za SMZ ndani ya
kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani, sio tu imeleta faraja kwa
wananchi, bali pia itainua utekelezaji wa majukumu yao na kuleta tija kubwa kwa
Taifa letu.
Sambamba na hilo, kauli ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuanza kutekeleza kwa vitendo mpango wa kuwapatia pencheni maalum wazee
wote waliofikia umri wa miaka 70 bila kujali historia ya kazi walizokuwa
wakizifanya, nayo CCM linaunga mkono kwani zitawapunguzia kwa kiasi fulani
ugumu wa maisha kwa wazee wetu hao pamoja na walio karibu na wazee hao.
Kauli ya Rais wa Zanzibar kuendeleza na kuimarisha sekta ya
michezo nchini, kwa kuimarisha mashindano mbali mbali Maskulini, Wilayani,
Vikundi vya Mazoezi, pamoja na kukamilisha Ujenzi wa Uwanja wa Mao Tse Tung, ni
jambo jema kwa wananchi hasa wanamichezo wa Taifa hili.
Wazanzibari walio wengi wamefarajika kwa kiwango cha juu na
kauli ya Rais wao mpendwa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuwaahidi tena bila ya kigugumizi kwamba wakati
umefika kwa Serikali yake wa kutumbua majipu kwa viongozi na watendaji
wote wanaoonekana kuwa ni majipu kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake.
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, kinachukua nafasi hii
kumpongeza tena Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa uongozi wake
mzuri ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tangu alipoingia madarakani
(Awamu ya Kwanza) hapo Novemba 03, 2011.
Kwa mnasaba huo, katika Awamu ya Pili ya Uongozi wake, CCM
inajenga matumaini makubwa yafuatayo :-
·
Mhe. Dkt. Shein, ataweza
kuwaunganisha vyema Wazanzibari Ndani ya Serikali na Nje ya Serikali kwa
kutekeleza kikamilifu Katiba na Sheria za nchi.
·
Mhe. Dkt. Shein, ataweza kusimamia
kwa kiwango kikubwa na kuwaletea maendeleo ya haraka Wazanzibari jambo ambalo
litawezesha kuimarisha ukuaji wa uchumi na huduma mbali mbali za jamii.
·
Mhe. Dkt. Shein, katika kipindi
kijacho cha uongozi wake, ataweza kusimamia suala zima la amani na utulivu
ndani ya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba, jambo ambalo litawawezesha
Wazanzibar wote kufanya shughuli zao za kisiasa, kiuchumi na kijamii, bila ya
kuwa na hofu yoyote.
·
Mhe. Dkt. Shein, ni kiongozi
anayependa watu wa rika na jinsia zote na hana chembe ya ubaguzi, anawapenda
watu wote na atawatumikia wananchi kwa umakini na uadilifu mkubwa sana.
Mwisho, Chama Cha Mapinduzi kinatoa pongezi za pekee kwa
Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuunda Tume
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, itakayosimamia masuala ya maadili ya
viongozi na nidhamu makazini.
Mwisho kabisa, Chama Cha Mapinduzi kinatoa wito kwa Jamii
nzima ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla wake, wawe tayari kumpa kila aina
ya mashirikiano, ili aweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake aliyokabidhiwa
na Taifa.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
(Vuai Ali Vuai),
Naibu Katibu Mkuu wa CCM,
ZANZIBAR.
06/04/2016.
0 comments:
Post a Comment