Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati
mbili za makubaliano na Serikali ya Japan itakayoiwezesha Tanzania kupata kiasi
Yen Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 116.4 za Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini
hati hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile
alisema mkataba wa kwanza utasaidia katika kukamilisha bajeti ya Serikali ya
mwaka 2016/17.
Dkt. Likwelile alisema kuwa msaada huo unalenga kuweka
mazingira rafiki ya kwa wafanyabiashara, kuboresha masoko na kuwezesha
mazingira ya ushindani katika utengenezaji wa ajira nchini.
Mkataba wa pili unahusu masuala ya kiufundi
yatakayotumika katika kufanya marekebisho ya mkataba uliosainiwa Octoba
20, 1966, kwa kuzingatia sheria nyingi zimebadilika, kusainiwa kwa hati hiyo ya
makubaliano itasaidia kutabadilisha baadhi ya vifungu vyenye jina Tanzania na
kuweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujumuisha pande zote mbili za
Muungano katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
Aidha, makubaliano hayo yatasaidia kubadilisha baadhi ya
vipengele vya mkataba uliopita ikiwemo kipengele cha usambazaji wa madawa ili
kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ya wataalamu kutoka nchini Japan kuweza kuja
kufanya kazi za kujitolea hapa nchini Tanzania.
Katibu Mkuu Dkt. Likwelile ameishukuru Serikali ya Japan na
kusisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa ili kuweza kuwa na tija
na kuwaletea maendeleo Watanzania.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida
amesema kuwa Serikali ya Japan ina imani kuwa ushirikiano uliopo baina ya nchi
hizi mbili utasaidia kukuza maendeleo ya uchumi na kijamii.
Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japani inaunga mkono
juhudi za Serikali inayo ongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika masuala ya
viwanda na mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji kuwekeza nchini
Tanzania.
Adha Balozi Yoshida amesema kuwa Japan itaendelea kuwaleta
vijana wanaojitolea katika sekta ya uchumii na ya kijamii jambo limekuwa
likitekelezwa tangu mwaka 1969 ambapo hadi sasa idadi ya vijana hao wa
kujitolea imefikia zaidi ya 1500.
0 comments:
Post a Comment