TAARIFA FUPI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA VIETNAM NCHINI TANZANIA
9-10 MACHI 2016
Utangulizi
Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa
Truong Tan Sang anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini tarehe 9 Machi 2016.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza uhusiano baina ya Vietnam na
Tanzania mbao umedumu kwa zaidi ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja
Kufungua maeneo mapya ya Ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Vietnam.
Hii ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo Barani Afrika tangu aingie madarakani
mwaka 2011, ambapo nchi nyingine anayotarajiwa kutembelea ni Mozambique. Rais
Truong anatarajiwa kufuatana na mke wake Bi Mai Thi Hahn, mawaziri 4
wanaoshughulika na sekta za Kilimo,
Mawasiliano Uwekezaji, Afya Viwanda na Biashara. Aidha mgeni huyo atafuatana na ujumbe wa
wafanyabiashara 30 kutoka Vietnam.
Shughuli
za msingi zitakazofanyika kwenye ziara
·
Wakati
wa ziara hiyo Rais Truong Tang San atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini
Dar-es-Salaam.
·
Aidha,
Rais Truong pia atapata fursa ya kutembelea eneo la EPZ la Ubungo kuangalia
viwanda mbalimbali vinavyozalisha bidhaa za kuuza nje ya nchi.
·
Baada
ya kutembelea EPZA Rais Truong atahudhuria mkutano wa biashara na uwekezaji
katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na taasisi za umma na sekta binafsi
kutoka Tanzania na Vietnam.
·
Rais
Truong atamaliza ratiba yake kwa kuhudhuria dhifa ya Taifa itakayoandaliwa kwa
heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk.John Pombe
Joseph Magufuli.
Wasifu wa Rais wa Vietnam
·
Mheshimiwa
Truong Tan Sang amezaliwa tarehe 21 January 1949 katika Jimbo la Long An nchini
Vietnam. Amepata Elimu ya Juu kutoka taasisi ya national Academy of Public
Administration ya Vietnam ambako alipata Shahada ya kwanza ya Sanaa na Sheria.
·
Kutokea
mwaka 1966 hadi 1996 Mheshimiwa Truong ameshika nafasi mbalimbali za utendaji
katika Chama Tawala cha kikomunisti cha Vietnam.
·
Mwaka
1996 Mhe Truong alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Tawala na
Katibu wa Chama hicho katika Jimbo la Ho Chi minh hadi mwaka 2000 ambapo
aliachia wadhifa wa katibu Mkuu wa Jimbo na kuendelea na nafasi ya ujumbe wa
Kamati kuu ya Chama tawala hadi tarehe 25 Julai 2011 apochaguliwa na Bunge la
Vietnam kuwa Rais wa Vietnam.
·
Mhe
Truong amemuoa Bi mai Thi Hanh na wamejaaliwa mtoto mmoja.
Taarifa Muhimu Kuhusu Vietnam
Historia fupi ya Vietnam
·
Vietnam
ilifanya mapinduzi tarehe 14 Agosti 1945 na hatimaye kupata uhuru tarehe 2
Septemba 1945 ikijulikana kwa jina la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Vietnam. Pamoja na kupata uhuru nchi hiyo iliendelea
kuwa na migongano baina ya Vietnam ya Kaskazini na Kusini iliyopelekea vita
iliyodumu kwa muda mrefu na kuhusisha mataifa ya nje.
·
Kufuatia
kumalizika kwa vita, Vietnam ya Kaskazini na Kusini ziliungana tena na kuunda
Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam tarehe 2 Julai 1976. Nchi hiyo yenye
kilomita za mraba 329,560 iliyopo kusini mashariki mwa Asia ina watu milioni
91.7 na inaongozwa na Chama cha Kikomunisti cha Vietnam.
Mafanikio ya
Uchumi ya Vietnam
·
Vietnam
ni moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo barani Asia. Mwaka 1986
Serikali ya Vietnam ilianzisha mageuzi makubwa ya uchumi yaliyopelekea kuitoa
nchi hiyo kwenye kundi la nchi masikini yenye kipato cha Dola za Kimarekani 100
kwa kila mtu hadi kufikia kuwa nchi yenye uchumi wa kati yenye kipato cha Dola
za kimarekani 2000 kwa kila mtu mwaka 2014. Katika mageuzi hayo,Vietnam
imefanikiwa kupunguza umasikini wa wananchi wake kwa asilimia 50.
Mafanikio
katika Sekta ya Kilimo
·
Sifa
kuu ya Vietnam ni uthubutu na uwezo wa kusimamia mipango yake. Mfano mwaka 1980
nchi hiyo iliamua kuingia kwenye uzalishaji mkubwa wa kahawa. Ndani ya miaka 10
iliweza kufikia uzalishaji wa tani 300,000 kwa mwaka na hatimaye kuwa nchi
inayoongoza ulimwenguni katika uzalishaji na uuzaji wa kahawa aina ya Robuster.
Vilevile miaka ya 1990, Vietnam ilikuwa ikiagiza mchele kutoka nje, kufuatia
hatua madhubuti walizochukua mwaka 2004 ilishika nafasi ya pili duniani katika
uzalishaji wa mchele kwa kuwa na misimu mitatu ya mavuno.
·
Hivi
sasa Vietnam imejiwekea malengo ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa
sukari duniani ambapo mwaka 2015 uzalishaji wake umefikia tani milioni 2 kwa
mwaka. Mbali na mazao hayo, Vietnam inaongoza ulimwenguni kwa kuuza korosho na
pilipili manga. Vilevile,Vietnam ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwenye
kilimo cha muhogo na mpira.
·
Mafanikio
makubwa ambayo Vietnam imeyapata katika kuongeza uzalishaji katika sekta ya
kilimo, yamekuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo kwa sasa ndio
imeshika hatamu ya uchumi wa Vietnam.
·
Mkakati wa Mageuzi ya Kijamii na Kiuchum 2011-2020
·
Aidha,
Vietnam inatekeleza mkakati wake wa kuwezesha mageuzi ya kijamii na kiuchumi wa
mwaka 2011-2020 ambao umejikita kwenye kuwapatia wananchi elimu na stadi
za ufundi kwa ajili ya kufanya kazi kwenye viwanda vinavyotumia teknolojia ya
kisasa na ubunifu; kuboresha taasisi zinazoshughulika na masoko; na kuendelea
na ujenzi wa miundombinu.
·
Mkakati
huo unaendana na utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa nchi hiyo ambao kwa sasa
umelenga kufanya mageuzi makubwa katika taasisi za kibenki ili kuwezesha wananchi
kupata mitaji ya kufanya shughuli za uchumi na maendeleo; na mageuzi ya
makapuni ya biashara ya Serikali ili yaweze kushindana katika uchumi wa soko
ndani na nje ya nchi pasipo kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.
·
Ni
dhahiri kwamba yapo mambo ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka Vietnam
katika safari yake ya kuwa nchi ya uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025. Tanzania
inayo nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji katika mazao ya miwa,mpunga na uvuvi
kwa kupitia ushirikiano na Vietnam.
Mahusiano ya Vietnam na Tanzania
·
Mahusiano
ya Tanzania na Vietnam yaliyojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Kiongozi wa Vietnam Ho Chi Minh mwaka 1960 na kupelekea kuanzishwa
rasmi kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1965.
Kwa muda mrefu mahusiano hayo yalikuwa ya kisiasa zaidi ambapo Tanzania
iliunga mkono harakati za Vietnam za kupinga uwepo wa majeshi ya kigeni kwenye
ardhi yake.
Ziara
za Kukuza Mahusiano za Viongozi Wakuu
·
Aidha
katika kipindi cha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya Vietnam na
Tanzania, viongozi wa kitaifa wa nchi hizi mbili wamefanya ziara za kudumisha
mahusiano baina ya nchi hizi mbili.
Tarehe 25 Septemba 1973, Rais wa Vietnam Mheshimiwa Nguyen Huu Tho
alifanya ziara nchini Tanzania.
·
Kwa
upande wa Tanzania, viongozi waliofanya ziara nchini Vietnam ni pamoja na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa (2004);
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (2014),
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohamed Shein
(2012); Mawaziri Wakuu wa Serikali ya
Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano Mhe.Edward Lowassa (2006); na Mhe. Mizengo
Kayanza Pinda (2010).
Mikataba
ya Mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam
Katika jitihada za kuimarisha mahusiano, mwaka 2001 Tanzania na Vietnam
zilisaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kuichumi na ufundi. Mkataba huo uliainisha maeneo ya ushirikiano
yafuatayo:
1)
Kubadilishana
uzoefu katika sekta ya kilimo na maendeleo vijijini;
2) Kubadilishana uzoefu katika matumizi ya sayansi na
teknolojia katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na misitu;
3) Kupeana taarifa za fursa za masoko ya bidhaa za kilimo
4) Vietnam kuipata Tanzania utaalam na teknolojia ya
uvunaji na utunzaji wa maji
·
Mwaka
2014 Tanzania na Vietnam zilisaini Mkataba wa ushirikiano katika sekta ya
mawasiliano ambapo kupitia mkataba huo kampuni ya Vietel inayomilikiwa na
Jeshi la Vietnam imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya mawasiliano nchini
na kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa watanzania 1600 na fursa za kujiajiri
kwa watanzania 20,000. Vilevile,kampuni hiyo kupitia mkataba uliosainiwa,itatoa
huduma za internet bure kwenye mashule na mahospitali ya Serikali vijijini.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Dar es Salaam
03 Machi, 2016
0 comments:
Post a Comment