Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewashauri
wakulima kutumia teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji maji hasa katika maeneo
ya maweni ili kupata mazao yatakayokidhi katika soko la utalii nchini.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo Zanzibar, Juma Ali Juma katika ziara maalum ya kuwatembelea
wakulima wa kilimo cha maweni huko Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja.
Wakulima hao wanalima Tungule,
Matikiti maji, bilinganyi, pilipili boga, ndimu, Papai na vitunguu maji.
Amesema endapo wakulima watafanya kilimo
hicho kwa kufuata ushauri wa kitaalamu watapata mazao mengi na yanayokubalika
katika soko na kujikwamua kiuchumi.
Juma amesema lengo la serikali ni kuhakikisha
dhana ya mapinduzi ya kilimo inatekelezwa kwa vitendo kwa kuwapatia elimu ya
kitaalamu wakulima wanaolima kilimo mbali mbali kikiwemo cha maweni ili waweze
kuzalisha mazao bora na mengi yanayotosheleza soko la ndani ya nchi na
kupunguza uagiziaji mazao nje ya Zanzibar.
Naibu Katibu mkuu huyo emefafanua kuwa kilimo
hicho kinachostawi katika maeneo ya mawezi ni cha aina za mboga mboga, hivyo
wakulima wanatakiwa kuendelea kubuni mbinu za mbali mbali za uzalilishaji mazao
hayo kwa wingi ili kwenda sambamba na fursa ya masoko ya ndani.
Aidha amewasihi vijana nchini kujiajiri
wenyewe kupitia kilimo hicho kwa lengo la kupambana na changamoto ya ukosefu wa
ajira badala ya kukimbilia mijini wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi
vijijini.
Kwa upande wake Mkulima wa kilimo hicho kutoka
Shehia ya Bwejuu Mohamed Nuru Mohamed, amesema licha ya kilimo cha maweni
kujenga matumaini makubwa ya mafanikio bado wanahitaji msaada wa kitaalamu
utakaowasaidia kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji kupata mazao mengi zaidi
ya wanayopata hivi sasa.
Nae Hassan Ame Hassan, ambaye ni Mkulima wa mazao
mbali mbali ya Mboga mboga amekiri kilimo hicho kuwa na manufaa kwani mpaka
sasa ana uwezo wa kuhudumia familia yake vizuri yenye watu 17, ambapo kabla ya
kuanza kilimo hicho halikua anaishi maisha ya tabu.
Amesema uzuri wa kilimo cha kutumia teknolojia ya
umwagiliaji maji ni kuwa hakitegemei msimu wa mvua bali unalima wakati wote
kama una miundo mbinu mizuri ya upatikanaji wa maji na mipira imara ya
kusambazia maji hayo maarufu kama “Drip”.
Amezitaja changamoto zinazowakabili katika kilimo
hicho kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma ya umeme pamoja na miundombinu ya
barabara kwa ajili ya kusafirisha mazao yao kuyapeleka katika masoko.
0 comments:
Post a Comment