Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema kwamba njia pekee ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto
zinazoukabili Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwemo kushuka kwa kiwango cha elimu,
ukosefu wa ajira kwa Vijana pamoja na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya
Watoto na Wanawake ni nguvu za pamoja kati ya Viongozi na Wananchi wenyewe wa
Mkoa huo.
Alisema Jamii yoyote ile isipokutana na
kupanga jinsi ya kuendesha mambo yanayowagusa kamwe jamii hiyo haitaweza
kupata mafanikio kwa jambo lolote lile mfano Elimu, afya au hata Kilimo.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati
akiizindua rasmi Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja {JMMK} hapo
katika Ukumbi wa Mikutano wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar.
Alisema Takwimu zinaonyesha wazi kwamba Mkoa
wa Kaskazini Unguja unaongoza kwa kushuka kwa kiwango cha Elimu, vitendo vya
udhalilishaji, uchafuzi wa mazingira na mpasuko wa Umoja unaosababishwa na
tofauti za Kidini na Kisiasa ambazo zimepelekea kudidimia kwa hadhi na heshima
ya Mkoa huo katika uso wa Zanzibar.
“ Mkoa wetu hivi sasa umevamiwa na watu ambao
wanatumia dini na siasa kwa lengo la kuwagawa wananchi mambo ambayo kama
hawakuwa makini watu hao wanaweza kuwaweka mahali pabaya Wananchi wa Mkoa
huo ”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kuwa kwa kipindi kirefu sasa
Skuli za Mkoa wa Kaskazini Unguja hazifanyi vyema katika Mitihani yao ya Kitaifa
hali inayotishia maendeleo ya Mkoa huo pamoja na Taifa kwa ujumla.
Balozi Seif aliitaka Jumuiya ya Maendeleo ya
Mkoa wa Kaskazini Unguja {JMMK} kujipanga vizuri kimpango na Kimkakati kwa
upande wa suala la kukuza kiwango cha Elimu ili Mkoa huo ujenge hadhi ya
kuongoza kielimu Tanzania nzima.
Alisema ili malengo hayo yafanikiwe vyema
Jumuiya hiyo inahitaji kuwa na mashirikiano ya hali ya juu na karibu zaidi kati
ya Viongozi wake, skuli zote zilizomo ndani ya Mkoa, wazazi, Taasisi za Kijamii
pamoja na wanafunzi wenyewe.
Balozi Seif alisema baadhi ya mambo ambayo
Jumuiya hiyo inaweza kufikiria kuyatekeleza ili kukuza kiwango cha elimu
ni pamoja na kuzifanyia kazi tafiti mbali mbali zilizoonyesha mapungufu
ya kielimu pamoja na kushajiisha vijana wa Mkoa huo wenye Elimu ya juu kutenga
muda wao wa Jumamosi na Jumapili kwa ajili ya kuwasaidia Vijana wenzao.
Akigusia suala la ajira hasa kwa Vijana
wanaomaliza masomo yao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri
Uongozi wa Jumuiya hiyo kushajiisha watu wenye mitaji kufungua vituo vya kazi
za Amali Mkoani huo ili kusaidia kupunguza wimbi kubwa la ajira katika eneo
hilo.
Alifahamisha kwamba Vituo hivyo vya kazi za
amali {Job Centre} vijengewe uwezo mkubwa wa utoaji wa mafunzo yatakayotoa
fursa pana kwa vijana wanaojifunza kuwa na uwezo mpana wa
kuajirika.
Alieleza kwamba Mkoa wa Kaskazini Unguja
umebarikiwa kuwa na Miradi mingi ya Hoteli za Kitalii ambazo iwapo
utakuwepo utaratibu mzuri wa mawasiliano kati ya Uongozi wa Jumuiya hiyo, Mkoa
na wamiliki wa Hoteli hizo uwezekano wa kupata ajira kwa vijana watakaomaliza
mafunzo ya vituo hivyo utakuwa mkubwa sana.
Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi na kuwaomba
Vijana wanaomaliza masomo yao kuacha tabia ya kuchagua kazi kwani huu si wakati
wa kufanya hivyo kutokana na tatizo hilo kubwa kwa hivi sasa limekuwa
likiyakumba na kuyaathiri mataifa mbali mbali Ulimwenguni yakiwemo pia yale
yaliyoendelea kiviwanda.
Kwa upande wa Dini na Siasa sehemu
zinazoonekana kutumiwa vibaya wakati huu na hatimae kuleta mtafaruku ndani ya
Jamii Balozi Seif aliwanasihi wanakaskazini wote kuendelea kuilinda hadhi ya
Mkoa wao unaooneka kuyumba kutokana na mavamizi ya watu wanaopenda kugawa
wananchi.
Alisema siasa na Dini sio mambo mageni ndani
ya Mkoa huo yaliyoonekana kutoa nafasi pana kwa kizazi kilichopita kushiriki
kikamilifu katika masuala yote mawili na kamwe hawakuwa tayari hata kidogo
kuvunja umoja wao.
Alisema kizazi cha nyuma kiliishi na kupendana
sambamba na kushirikiana katika mambo yao yote ya kijamii na hakukuwa na ndoa
zilizovunjwa kwa sababu ya kisiasa kama jamii inavyoshuhudia kufanyika kwa
vitendo hicho vibaya hivi sasa vinavyokwenda kinyume na Utamaduni pamoja
na maadili ya Dini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza
Uongozi Mzima wa Wana wa Kaskazini Unguja kwa wazo lao la kuunda Jumuiya ya
Maendeleo ya Mkoa wao kitendo kitakachosaidia chachu ya kupatikana kwa
maendeleo ya haraka ndani ya Mkoa huo.
Alisema Mikutano inayofanywa na kupatikana
ndani ya jumuiya zinazoundwa na watu kutoka upande mmoja wa nchi kwa lengo la
kujadili na kupanga mambo yatayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili ni
muhimu sana kwa maendeleo yao pamoja na hata kwa Taifa.
Akitoa muhtasari wa Jumuiya ya Maendeleo
ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Mjumbe wa Kamati Tendaji ya muda ya Jumuiya
hiyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Ndugu Ayoub Moh’d Mahmoud
Jecha alisema wazo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo limepata Baraka kutoka kwa
Viongozi wakuu wa Kitaifa wenye asili na uzawa wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Nd. Ayoub alisema Kamati tendaji ya muda
ililazimika kuunda kamati nyengine ndogo ndogo za Uchumi na Ustawi wa Jamii ,
Kamati ya Ustawi wa Jamii na ile ya Mkakati kwa dhamira ya kuurejeshea
heshima yake Mkoa huo wa Kaskazini Unguja.
Mapema Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Tano wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Wanakaskazini Unguja Mh. Haji Omar Kheir alisisitiza
umuhimu wa wanajumuiya hiyo kujitolea kwa nguvu zao zote ili lengo
lililokusudiwa la kuundwa kwake lifanikiwe vyema.
Akizitaja baadhi ya changamoto zinazoendelea
kuukumba Mkoa Huo Mh. Haji alisema kupotea kwa mila , silka na Utamaduni ndani
ya jamii za wanakaskazini Unguja ndio chimbuko la kubuniwa kwa Jumuiya
hiyo ya Maendeleo ya Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unaguja.
Mkutano huo wa Tano wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Mkoa wa Kaskazini Unguja ulifuatiwa na mada ya Uchumi na Ustawi wa jamii
iliyotolewa na Mjumbe wa Kamati Tendaji wa Jumuiya hiyo Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud
na kujadiliwa na walishiriki zaidi ya 980 kutoka Matawi yote 98 yaliyomo ndani
ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini
Unguja {JMMK} imeshateua Wajumbe Watano waliounda Bodi ya wadhamini ambao
ni Dr. Salmin Amour,Balozi Seif Ali Iddi, Bibi Fatma Bakari Moh’d, Mzee Ali
Ameir Mohammed pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dr. Ali Mohammed Shein aliyetunukiwa heshima hiyo na kukubali kuwa
mwanachama wa Jumuiya.
Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Mkoa wa
Kaskazini Unguja wakifuatilia Hotuba ya Mgeni rasmi kuizindua
Jumuiya
hiyo Balozi Seif hayupo pichani hapo Bwawani.
|
0 comments:
Post a Comment