February 13, 2016

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonya vikali kwamba vyombo vya Dola havitakuwa tayari kuona Watu wachache wanatumia hila na vishawishi vya kutaka kuharibu uchaguzi wa marejeo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Mwezi ujao.
Onyo hilo amelitowa Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Wanachama wa CCM na wananchi wa Kijiji cha Kengeja mara baada ya kulikagua Tawi la CCM la Kijiji hicho lililochomwa moto na watu wasiojuilikana usiku wa kuamkia jumatano.
Balozi Seif amesema ametahadharisha kuwa fujo zozote zitakazotokea kabla na baada ya uchaguzi huo wakukamatwa  na kupelekewa  kwenye vyombo vya Dola pamoja na Kiongozi atakayehusika na kuandaa vurugu hizo.
Amewaonya watu walioandaliwa kujihusisha na vitendo vya vurugu ikiwemo kufanya hujuma dhidi ya mali na vifaa vya Wananchi yakiwemo majengo ya Kisiasa kuacha mara moja tabia hiyo itaayowasababishia kutiwa na baadaye kuchukuliwa hatau za kisheria.
Balozi Seif amesema vitendo vya hujuma vinavyoonekana kuibuka nyakati hizi ni vibaya kwa vile vinaathiri maisha ya jamii kutokana na athari za hujuma hizo kuharibu miradi ya wananchi kama mashamba, Majengo ya Skuli na yale ya Raia pamoja na huduma za  Maji safi na salama.
Amesema Vyombo vya Dola bado vinaendelea kufanya uchunguzi wa kuwabaini watu waliohusika na vitendo hivyo wakiwemo wale watu wanaoendeleza kauli za chuki, hujuma na na kutaka kuleta vurugu hapa Nchini.
Balozi Seif amewahakikishia Wanachama na Wananchi hao kuwa Serikali itajizatiti kuongeza ulinzi wa kutosha utakaoleta faraja kwa Umma hasa katika kipindi cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi wa marudio wa mwezi ujao wa machi.
Amesema uhuru wa Jamii utalindwa ili kumpa fursa  kila Mwananchi kuitumia haki yake ya Kidemokrasia kumchagua Kiongozi anayestahiki amtumikie katika uchaguzi huo wa marejeo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai amesema Wanachama  wa CCM  wanasubiri kupiga kura ya marejeo ifikapo Tarehe 20 mwezi ujao.
amewataka wanachama hao wa Chama cha Mapinduzi  kuzipa mgongo hila zilizozoeleka kufanywa na baadhi ya wanasiasa za kudanganya wananchi hali ya kisiasa inavyokwenda nchini na tayari zimeshafikia ukingoni.
Amefahamisha kuwa CCM muda mwingi ilikuwa tayari kuridhia kila kitu katika kuiona nchi inaendelea kubakia salama na hatimae kufikia suluhu ya kuundwa kwa Serikali na Umoja wa Kitaifa Zanzibar  lakini upande mwengine wa upinzani unashindwa kufahamika hasa unataka nini.
Amevitaka vyombo vya Dola kutosubiri kutokea maafa wakati watu wanaoashiria matamshi ya shari wanaeleweka katika maeneo mbali mbali Nchini.
Ameeleza kwamba vyombo hivyo vina wajibu na haki ya kuwadhibiti watu wenye tabia hiyo.
Hadi sasa athari ya gharama zilizotokea kutokana na janga hilo la moto ulioathiri baadhi ya sehemu za paa, mlango na Boriti katika Tawi hilo la CCM  Kengeja bado hazijafahamika.


0 comments:

Post a Comment