Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China inatarajiwa kuikabidhi rasmi Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo Wilaya ya
Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba mara baada ya kukamilika ujenzi
wake Mwezi Oktoba mwaka huu.
Hospitali hiyo inayojengwa katika mfumo
wa Teknolojia ya Kisasa utakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma mbali mbali ikiwemo
zile za upasuaji mkubwa, uchunguzi wa maradhi mbali mbali itaweza kukidhi
mahitaji ya huduma za Kiafya kwa Wananchi walio wengi ndani ya Visiwa vya
Zanzibar pamoja na ukanda wa Mwambao wa Tanzania.
Mwakilishi wa Wahandisi wa ujenzi wa Hospitahi
hiyo Bwana Zhang Dou alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
wahandisi wa ujenzi huo kwa sasa wanaendelea kukamilisha majengo ya huduma
tofauti, kazi itakayofuatiwa na ufungaji wa vifaa ili kukamilisha kazi
hiyo kwa wakati uliopangwa.
Alisema harakati za ujenzi huo pia zinalenga
kuzirekebisha Nyumba za Timu za Madaktari wa Kichina wanaopangiwa kutoa huduma
mbali mbali za Afya katika Hospitali hiyo.
Bwana Zhang alisema Hospitali hiyo itakuwa na
uwezo wa kulazwa wagonjwa wapatao Mia Moja na Thamanini zikiwemo huduma zote
muhimu kama Vyumba Vitatu vya Upasuaji, Chumba cha wagonjwa Mahututi
{ICU}pamoja na Jengo la Msikiti litakalotumiwa naWagonjwa pamoja na
familia zao kwa ajili ya Ibada.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba Jamuhuri ya Watu wa China bado inaendelea
kuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kuunga mkono harakati za Maendeleo ya
Wananchi wa Visiwa hivi.
Balozi Seif alisema msaada huo mkubwa wa
kugharamia ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Kisiwani Pemba uliotolewa
na rafiki wa kweli China ni kielelezo kinachothibitisha ushirikiano
huo wa muda mrefu uliopo kati ya China na Zanzibar.
Alisema Wananchi wa Zanzibar wanaendelea
kufaidika na huduma za afya zinazotolewa na China kupitia Timu ya Madaktari
wake wanaobadilishana na kutoa huduma za afya katika kipindi cha miaka miwili
mfumo ambao umeanza kutekeleza kwa takriban miaka Hamsini sasa.
Ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee
Mkoani ambao ni msaada unaogharamiwa na Serikali ya Jamuhuri umekuja
kufuatia ziara za mara kwa mara zinazofanywa na Viongozi wa Juu wa Zanzibar na
Jamuhuri ya Watu wa China katika kuimarisha ushirikiano wa pande hizo
mbili.
Msimamizi wa ujenzi wa
Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani
kutoka China
BwanaZhang Dou akimpatia maelezo
Balozi Seif
juu ya harakati za ujenzi
zinavyoendelea kwa
ufanisi mzuri.
|
0 comments:
Post a Comment