Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi amesema kwa vile Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeshatangaza Tarehe ya
Kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yeye binafsi haoni umuhimu wa
kurejewa kwa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na
Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein .
Amesema mazungumzo hayo kwa sasa hayana tija
yoyote kwa vile Wananchi katika kipindi hichi wameanza kujiweka tayari
wakijiandaa kupiga kura kufuatia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC}
kufuta matokeo ya uchaguzi Tarehe 28 Oktoba mwaka 2015.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye
Uwanja wa ndege wa Pemba akijiandaa kurejea Kisiwani Unguja baada ya kumaliza
ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba kukagua shughuli mbali mbali za
Maendeleo akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali Balozi Seif Ali Iddi amesema iwapo
yapo malalamiko yoyote muhusika wake ana wajibu wa kwenda Mahakamani kwa hivi
sasa.
Balozi Seif amesema
mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi {CUF } Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu
yalifanyika kwa maombi ya Maalim Seif ambae yeye binafsi ndie aliyeamua
kujiondoa kwenye maendeleo ya vikao vya mazungumzo hayo.
Amesema kinacholikabili Taifa kwa wakati huu
ni suala la marejeo ya uchaguzi na kuwaomba watu walioamua kutoshiriki uchaguzi
huo wa marudio ni vyema wakabakia nyumbani ili kutoa fursa kwa wenzao
waliokubali kushiriki watumie haki yao ya Kidemokrasia kuwachaguwa Viongozi
wanaowataka.
Balozi Seif amefahamisha kwamba hata yeye
anaheshimu maamuzi ya Tume ya Uchaguzi ya Z anzibar ambayo haiwezi
kuingiliwa na chombo chochote licha ya kwamba tayari alikuwa ameshashinda na
kupewa cheti kinachothibitisha kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda.
“Tupo tuliokwishashinda kwenye chaguzi zetu za
Majimbo na kupewa vyeti vinavyothibisha ushindi huo lakini baadhi yetu kwa nini
tuendelee kushutumu maamuzi ya tume ambayo kutokana na sababu za msingi
ilizoeleza za kujitokeza kwa dosari kadhaa kwenye zoezi zima ikalazimika
kufuta matokeo na uchaguzi wote ? ”. ameuliza Balozi Seif.
Akizungumzia uvumi uliojitokeza wa
kuwepo kikundi cha Vijana wanaopiga watu katika badhi ya maeneo maarufu Mazombi
Balozi Seif amesema hana taarifa yoyote iliyomfikia akiwa kama Kiongozi wa Juu
wa Serikali kuhusu shutma hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa
agizo kwa vyombo
vya Ulinzi kufanya uchunguzi dhidi ya shutuma
hizo na pale itakapobainika kuwepo kwa shutma hizo vifanye juhudi ya kuwakamata
wahusika hao na kuwafikisha mbele ya Dola ili sheria ichukuwe mkondo wake.
Balozi Seif ameeleza kwamba nia ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Ile ya Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania ni kuiona
nchi inaendelea kubakia katika hali ya amani na utulivu wakati wote kabla
na baada ya uchaguzi.
Amewaasa na kuwaomba Wananchi wa maeneo mbali
mbali Kisiwani Pemba kuendelea kuishi kwa amani na upendo na kushirikiana
katika mambo yao bila ya kuendekeza zaidi itikadi zao za Kisiasa ambazo tayari
zimeshaonyesha muelekeo mbaya.
Ameeleza kwamba matokeo ya sasa
yaliyojichomoza katika hujuma za moto sambamba na baadhi ya watu kuanza
kuashiria vitisho dhidi ya wananchi wenzao walioamua kushiriki uchaguzi wa
marejeo kwa kuwatilia X nyumba zao yanaonyesha safari ya hatari katika maisha
miongoni mwa jamii.
0 comments:
Post a Comment