Karafuu ni Zao la Kilimo linalotegemewa sana na Wakulima wa zao hilo na
Wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo kwa kukodi mashamba na vibarua
wanaoajiriwa kuchuma kwa makubaliano ya kulipwa ujira kwa ajili ya kuendesha
maisha yao.
Pia zao la karafuu ni zao kuu la Uchumi wa
Zanzibar kutokana na kuingiza fedha nyingi za kigeni ambazo hutumika katika
kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, kusambaza umeme, maji safi,
miundombinu ya bara bara na huduma nyengine muhimu.
Takwimu zinaonesha kuwa zao la Karafuu ndilo
linalochangia zaidi pato la Taifa kuliko mazao mengine ya biashara, ambapo
inakadiriwa kuchangia pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 20.5.
Kutokana na umuhimu wa zao hili, Serikali kupitia
Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Biashara
la Taifa (ZSTC) linaendesha mpango maalum wa kuongeza idadi ya mikarafuu na
kuongeza uzalishaji kwa kuotesha miche 1,000,000 kila mwaka na kuwagaia Wakulima
bila ya malipo.
Pamoja na jitihada hizo za Serikali za kuimarisha
zao la karafuu kwa maslahi ya Nchi na Wananchi wake lakini tukio la hivi
karibuni la watu wasiojuilikana kuchoma moto eka tisa za Mashamba ya Mikarafuu
linarudisha nyuma jitihada hizo.
Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea
Januari 22/2016 katika Shehia ya Mzambarauni Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba
mikarafuu 151 imeungua moto ambapo kati ya hiyo 36 haiwezi kuota tena kutokana
na athari hiyo ya moto.
Mikarafuu hiyo iliyoungua ni kutoka katika
mashamba matatu tofauti yaliyokuwepo katika sehemu moja ambapo kwa pamoja yana
ukubwa wa ekari tisa (9). Tukio hilo limesababisha hasara yenye
thamani inayokisiwa kufikia shilingi milioni 24.5.
Imeonyesha kuwa kitendo
cha kuchoma moto kwa mashamba hayo ni hujuma za makusudi kutokana na moto huo
kutokea katika maeneo tofauti. Kitendo hicho ni kibaya kwa sababu ni hujuma kwa
uchumi wa nchi na Wananchi wake.
Ni wazi kuwa kiitendo
hicho kimewaumiza sana Wakulima wa mashamba hayo kwa sababu Mkarafuu ni mti
unaohitaji huduma kubwa katika ukuaji wake, hata ukifikia hatua ya kuzaa
Mkulima huwa kafanya kazi kubwa. Sasa anapotokea mtu mwengine kufanya hujuma
huyo ni maumivu makubwa kwa Mkulima.
Mkarafuu mmoja una
uwezo wa kuzalisha zaidi ya pishi ishirini kulingana na ukubwa wa mkarafuu
wenyewe, kwa bei ya sasa ni zaidi ya shilingi laki nne hivyo mikarafuu 151
iliyoungua moto imesababisha
hasara kubwa ya kiuchumi na kimazingira.
Kutokana na umuhimu na thamani
ya zao la karafuu kwa uchumi wa Nchi na Wananchi wake Serikali ilipitisha
Sheria ya Maendeleo ya Karafuu, Namba 2 ya mwaka 2014 ili kuulinda Mkarafuu na
karafuu zenyewe.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo ni kosa kwa mtu yoyote
kuchoma moto mikarafuu. Kifungu cha 13(1) (a),kinakataza kuchoma au kutengeneza makaa, kuchimba mawe, udongo au mchanga kuangusha, kung’oa, kukata, kuharibu
au kuathiri mikarafuu kwa aina yoyote ile.
Waliofanya tukio hilo la uchomaji moto mashamba
ya mikarafuu wajue kuwa wamefanya kosa kwa mujibu wa Sheria ya Maendeleo ya
karafuu. Ni vyema Jeshi la Polisi likafanya uchunguzi wa kina kuwagundua waliofanya tukio hilo na kuwafikisha
katika vyombo vya Sheria.
Miongoni mwa madhumuni ya
kuundwa kwa Sheria hiyo ya Maendeleo ya Karafuu ya Mwaka 2014 ni kulinda na
kuweka ulinzi imara wa Mikarafuu na Karafuu zenyewe. Kuimarisha, kustawisha,
kuthaminisha na kuendeleza zao la karafuu Zanzibar, hivyo kuchoma moto
mikarafuu ni kwenda kinyume na Sheria hiyo.
Sheria hiyo pia inapiga marufuku kutumia mkarafuu kwa matumizi
ya aina yoyote, iwe kwa ujenzi wa nyumba, kuchonga mbao, kuchonga vinyago au
mapambo ya aina yoyote, hivyo Sheria hiyo inatoa ulinzi wa kutosha kwa sekta ya
karafuu. Linalotakiwa ni usimamizi wa utekelezaji wa Sheria hiyo.
Hujuma nyengine
inayokwaza jitihada za Maendeleo ya Sekta ya Karafuu ni kwa baadhi ya watu
kukata matawi na mikarafuu midogo kwa dhamira ya kuiba karafuu kutokana na
kuzoeleka kwa uuzaji na ununuzi wa karafuu kwa njia isiyokuwa rasmi ‘vikombe’.
Wakulima wengi wamekuwa
wakilalamika kukatiwa mikarafuu yao hasa wakati wa msimu wa uchumaji jambo
ambalo linachangiwa sana na kuwepo kwa baadhi ya watu wanaonunua karafuu mbichi
jambo ambalo ni kosa kwa vile Shirika la ZSTC ndio taasisi pekee iliyopewa mamlaka
ya kununua na kuuza karafuu.
Kwa mujubu wa Sheria hiyo
mtu atakaetiwa hatiani kwa kosa la kuuhujumu mkarafuu kwa aina yoyote ni kulipa
faini isiyopungua Shilingi Milioni tatu au kifungo kisichopungua miaka mitatu
(3) au vyote kwa pamoja kulingana na ukubwa wa kosa.
Shirika la ZSTC, taasisi
ambayo ni dhamana ya kuimarisha zao la karafuu kwa kushirikiana na wadau
wengine limekuwa likitoa elimu juu ya namna ya kuimarisha zao hilo na thamani
yake kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Mwezi Disemba 2011, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein alitia saini Sheria
mpya ya ZSTC Na. 11 ya mwaka 2011, inayoipa Mamlaka na uwezo Shirika la
ZSTC kulisimamia, kulihudumia, kuliimarisha zao la karafuu na kuhakikisha linakuwa
endelevu kwa maslahi ya wakulima, wananchi na Taifa kwa ujumla, kuchoma moto
mikarafuu kwa makusudi ni kurejesha nyuma jitihada za uimarishaji wa zao hilo.
Kutokana na uchumi wa Zanzibar kutegemea sana zao
la karafuu, Sera ya Serikali juu ya
zao la hilo ni kumnufaisha Mkulima zaidi, hivyo Serikali inaendelea na azma
yake ya kutekeleza uamuzi wake wa kuwapatia Wakulima bei ya karafuu ya asilimia
80 ya bei ya kuuzia nje ya nchi ili kuwahamasisha Wakulima kuimarisha zaidi zao
hilo.
Zao
la karafuu ninawanufaisha wengi kutokana na kutoa ajira kwa Wananchi wengi na
mzunguko wa fedha unaotokana na biashara ya zao hilo unajenga ustawi wa
Wananchi wengi na kuongeza pato la Taifa, hivyo kuichoma kwa makusudi ni
kuwakosesha kipato Wananchi wengi.
Pia kuna athari za kimazingira ambapo mikarafuu
kama ilivyo miti mengine huwa ni chanzo kikubwa cha mvua. Unapochoma moto
mikarafuu unakaribisha jangwa katika eneo hilo na kuondoa uwezekano wa kuwepo
kwa mvua. Kitendo hicho husababisha kukosekana kwa mvua na kupelekea ukame
katika maeneo husika.
Moshi mwingi ambao
hutolewa baada ya uchomaji wa Mikarafuu huleta athari katika mfumo wa hewa. Pia
uwepo wa mikarafuu ni kinga kwa mmongonyoko wa ardhi ambapo katika maeneo ya
mabonde ambapo mikarafuu hupandwa husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia mmongonyoko
wa ardhi.
Wito kwa Wakulima,
Wafanyabiashara na Wadau wote wa Zao la Karafuu na wananchi kwa
jumla kutokufanya makosa kama hayo ya uchomaji wa mashamba ya mikarafuu.
Kuchoma moto mikarafuu ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika
uimarishaji na uendelezaji wa zao hilo.
Ni vyema Wananchi wote
wakasaidia katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulinda mikarafuu yetu na ubora
wake ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuifanya Sekta ya karafuu kuendela
kuwa tegemeo katika kukuza uchumi na kujenga ustawi wa Wananchi.
:ZSTC
0 comments:
Post a Comment