February 16, 2016

Chama Cha National Reconstruction Alliance (NRA) kutoka Zanzibar kimethibitisha kushiriki uchaguzi wa marudio wa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu baada ya kikao kilichofanyika Februari 15.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Tanzania Bara Hassan Almasi Kisabya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa Chama hicho kitashiriki uchaguzi wa marudio na kusisitiza kuwa tamko lililotolewa na mgombea wao la kutoshiriki uchaguzi wa marudio lipuuzwe kwani ni tamko lake binafsi na sio msimamo wa chama.
“Tamko lililotolewa tarehe 14/02/2016 Si Tamko la chama cha NRA bali ni tamko binafsi na wale waliomuagiza kwani yeye hana mamlaka ya kukisemea chama wala wagombea wengine wa chama pasipo Baraka na vikao halali vya chama” alisema Kisabya.
Amesisitiza kuwa maamuzi ya chama ni sharti yatoke katika chama na sio kwa mgombea na ikiwa yeye amejitoa anatakiwa afuate taratibu za kisheria katika kujitoa kama alivyofuata sheria katika kugombea nafasi hiyo.
Aidha, Chama kinatoa taarifa kwa wagombea wote Zanzibar kujiandaa na wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu ili kutimiza haki yao kikatiba na kuchagua viongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Maelezo DSM

0 comments:

Post a Comment